1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yawahimiza washirika wake kupatiwa silaha zaidi

4 Juni 2024

Serikali ya Ukraine imesema Italia itaipatia nchi hiyo mfumo mwingine wa ulinzi wa anga silaha ambazo maafisa wakuu wa Ukraine wamekuwa wakiwahimiza washirika wake kutuma ili kukabiliana na mashambulizi ya Urusi

Ukraine
Wafanyakazi wa zima moto nchini Ukraine wakisaidia kuzima moto kwenye nyumba iliyoshambuliwa na UrusiPicha: Sergey Bobok/AFP/Getty Images

  
Serikali ya Ukraine imesema Italia itaipatia nchi hiyo mfumo mwingine wa ulinzi wa anga silaha ambazo maafisa wakuu wa Ukraine wamekuwa wakiwahimiza washirika wake kutuma ili kukabiliana na mashambulizi ya Urusi.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema nchi yake kwa sasa inahitaji msaada wa haraka wa mifumo saba zaidi ya ulinzi, ikiwa ni pamoja na miwili ili kulinda eneo la mashariki la Kharkiv, eneo ambalo Moscow imeanzisha upya mashambulizi.

Soma zaidi. Italia kuipatia Ukraine mfumo wa ulinzi wa anga na silaha

Katika taarifa iliyotolewa na ikulu ya Ukraine ni kwamba Italia kupitia Waziri wake wa mambo ya kigeni Antonio Tajani imethibitisha kuwa itaipatia Ukraine mfumo wa pili wa ulinzi wa anga.

Taarifa hizo zinakuja wakati ambapo maafisa wa eneo la Ukraine la Dnipropetrovsk wakisema watu wanane wamejeruhiwa katika mashambulizi ya usiku wa kuamkia jana yaliyofanywa na vikosi vya Urusi.

Raia wa Ukraine wakiwa nje ya nyumba ambayo imeshambuliwa na shambulizi la UrusiPicha: Andrii Marienko/AP/picture alliance

Soma zaidi. ICC na wafanyakazi wake walengwa na visa vya ujasusi

Mashambulizi ya leo kwenye kituo cha umeme cha Ukraine cha Ukrenergo yamepelekea kukatika kwa umeme katika miji kadhaa ikiwemo mji mkuu wa Kyiv na miji mingine.

Ihor: Ulinzi wa anga bado ni changamoto

Akizungumza na waandishi wa habari Gavana wa mji wa Kharkiv Ihor Terekhov amesisitiza kupatikana kwa vifaa vya ulinzi wa anga katika eneo hilo.

‘’Leo, swali kuu ni, kwa nini anga juu ya Kharkiv  haijafungwa, kwa nini hakuna ulinzi wa anga, kwa nini kuna mashambulizi ya anga ya mara kwa mara? Hili ndilo swali kuu la wakazi wa jiji, lakini ni vigumu sana kujibu. Ingekuwa jiji lilikuwa na fursa ya kuvipata vifaa vya kupambana na ndege, niniamini, tungefanya hivyo. Kungekuwa na uwezekano wote wa kufanya kila linalowezekana na lisilowezekana, kuchukua mkopo na kuhusisha wafadhili wote wanaowezekana. Lakini hii yote ni suala la makubaliano kati ya nchi. Hatuwezi kununua teknolojia hii leo.’’amesema Ihor Terekhov.

Gavana wa Kharkiv, Ukraine Ihor Terkhov amesema bado suala la kupatiwa ulinzi wa anga limekuwa gumuPicha: Vyacheslav Madiyevskyy/Avalon/Photoshot/picture alliance

Soma zaidi. Ujerumani watoka sare ya kutofungana na Ukraine huku Mbappe akijiunga na Madrid

Mashambulizi ya hivi majuzi ya makombora ya Urusi na ndege zisizo na rubani, likiwemo shambulio kubwa mwishoni mwa juma, yameongeza mwito wa Ukraine kwa washirika wake juu ya kupatiwa uwezo zaidi wa ulinzi wa anga.

Kwa upande mwingine Urusi imeionya Ufaransa juu ya mpango wake wa kuwapeleka wakufunzi wa kijeshi nchini Ukraine kutoa mafunzo ya kijeshi kwa wanajeshi wa Ukraine, Urusi imesema ikiwa wakufunzi hao watakumbana na mashambulizi ya Urusi nchini Ukraine basi itakuwa halali kwao.

Mashambulizi kati ya mataifa haya mawili bado yanaacha maswali yasiyo na majibu ya lini hasa mzozo huu uliodumu kwa zaidi ya miaka mwili sasa utamalizika.