1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yawarejesha nyuma Warusi eneo la Donbas

15 Mei 2022

Vikosi vya Ukraine vimeanza operesheni ya kuurejesha mikononi mwao mji wa mashariki wa Izium, hatua inayomaanisha mapambano ya kuwarejesha nyuma wanajeshi wa Urusi katika eneo la Donbas imeanza.

Ukraine | Russische Soldaten | Der Seehafen von Mariupol
Picha: AP/picture alliance

Kwa sasa, vikosi vya Urusi vinaonekana kuelekeza nguvu zake zaidi kwenye mkoa huo wa Donbas wenye utajiri wa viwanda katika kile Kremlin inachosema ni "awamu ya pili" ya uvamizi wake iliyotangazwa Aprili 19, baada ya kushindwa kuuchukuwa mji mkuu, Kyiv, kutokea upande wa kaskazini katika wiki za mwanzo za vita.

Lakini vikosi vya Ukraine vimekuwa vikiyarejesha mikononi mwake maeneo ya kaskazini mashariki na kuwafurusha wanajeshi wa Urusi kutoka mji wa pili kwa ukubwa wa Kharkiv.

Kwa kuendelea kuweka shinikizo lake kwenye mji wa Izium na kukata njia ya usafirishaji vifaa na bidhaa ya Urusi, kutafanya iwe shida kwa vikosi vya Moscow kuvizunguka vikosi vya Ukraine kutokea upande wa mbele wa jimbo la Donbas.

Urusi yadai kuuwa wanajeshi 100 wa Ukraine

Majengo yaliyobomolewa kwa mashambulizi ya Urusi katika viunga vya mji mkuu wa Ukraine, Kyiv.Picha: Hiroto Sekiguchi/AP/picture alliance

Hata hivyo, wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema vikosi vyake viliyashambulia maeneo kadhaa ya kijeshi ya Ukraine, yakiwemo ya Donbas, na kuwauwa "wanazi" 100 wa Ukraine. Taarifa hiyo haikuweza kuthibitishwa na vyanzo huru vya habari.

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine alisema kwamba hali katika eneo la Donbas bado ni ngumu, akiongeza kwmaba vikosi vya Urusi bado vinajaribu kujipatia aina fulani ya ushindi licha ya kukabiliwa na upinzani mkali wa Ukraine.

"Hawajaacha juhudi zao," alisema.

Ukraine yashinda Eurovision

Kundi la Muziki la Kalush lililoshinda shindano la Eurovision.Picha: MARCO BERTORELLO/AFP/Getty Images

Usiku wa siku ya Jumamosi (Aprili 14), kundi la muziki la Kalush kutoka Ukraine lilishinda mashindano ya Eurovision nchini Italia, ushindi unaotazamwa kama ishara ya jinsi hisia za umma barani Ulaya zilivyoelemea upande wa Kyiv tangu uvamizi wa Urusi dhidi yake ulipoanza mwezi Februari.

Ukraine ilikuwa inashikilia nafasi ya nne kwa mujibu wa jopo la majaji lakini uungaji mkono wa watazamaji ulilipandisha kundi hilo hadi nafasi ya kwanza.

"Ujasiri wetu unauvutia ulimwengu, muziki wetu unaikombowa Ulaya! Mwakani, Ukraine itakuwa mwenyeji wa shindano la Eurovision," alisema Zelensky kupitia ujumbe wa mtandaoni.

Kawaida, mshindi wa Eurovision ndiye anayekuwa na nafasi ya kuandaa shindano linalofuatia.

Uungaji mkono zaidi wa kimataifa

Katika ishara nyengine ya mshikamano wa kimataifa, maseneta wa chama cha Republican cha Marekani wamefanya ziara ya kushitukiza mjini Kyiv. Ujumbe huo wa Republican ulijadili hatua zaidi za kuongeza vikwazo dhidi ya Urusi, alisema Zelensky.

Ujumbe wa maseneta wa Republican kutoka Marekani wawasili Kyiv.Picha: Ukrainian Presidency/abaca/picture alliance

Wachambuzi wa Kimagharibi wanadai kuwa Rais Vladimir Putin wa Urusi alishindwa kukisia upinzani mkali wa kijeshi wa Ukraine na hatua kali za dunia dhidi yake, wakati alipoamuru uvamizi wa tarehe 24 Februari.

Mbali ya kupoteza idadi kubwa ya wanajeshi na vifaa vya kijeshi, Urusi pia imeathirika vibaya kwa vikwazo vya kiuchumi. 

Kundi la mataifa saba tajiri yanayoongoza uchumi wa Magharibi liliahidi kwenye taarifa yao ya pamoja siku ya Jumamosi kwamba lingeliendelea na "kuongeza shinikizo la kiuchumi na kisiasa dhidi ya Urusi" na kuipatia Ukraine silaha zaidi.