Ukraine yawasukuma nyuma wanajeshi wa Urusi Kharkiv
11 Mei 2022Urusi imeelekeza nguvu eneo la mashariki la Donbas ambako waasi wamekuwa wakipigania kutaka kujitenga tangu mwaka 2014, baada ya kushindwa kuuteka mji mkuu Kyiv. Afisi ya rais wa Ukraine imesema kitovu cha mapambano kimehamia Bilogorivka katika eneo la Lugansk huko Donbas, eneo lililoshambuliwa kutokea angani na Urusi Jumapili iliyopita ambapo watu 60 waliuliwa.
Mashambulizi ya makombora pia yameendelea katika ngome za mashariki katika miji ya Severodonetsk na Lyasychansk. Rais wa Ukraine Volodymr Zelensky amesema vikosi vya Urusi vinasukumwa nyuma kutoka mji wa Kharkiv, lakini ameghadhabishwa na ufichuzi wa gavana wa eneo hilo kwamba maiti 44 za raia zimepatikana chini ya kifusi cha jengo lililoharibiwa katika mji wa mashariki wa Izyum, ambao sasa uko chini ya udhibiti wa Urusi. Gavana wa Donetsk amesema raia watatu wameuawa katika eneo hilo jana Jumanne.
Mapambano hayo yametokea huku Marekani ikionya rais wa Urusi Vladimir Putin yuko tayari kwa vita vya muda mrefu. Ubashiri huo wa Marekani unakuja baada ya Ukraine kusema uanachama wake katika Umoja wa Ulaya ni suala la vita na amani kwa bara zima huku ikiikabili Urusi, zaidi ya miezi miwili tangu uvamizi.
Ukraine pia imepongeza kile ilichosema ni Ujerumani kubadili msimamo kuhusu kikwazo cha mafuta dhidi ya Urusi na kwa kupeleka silaha nchini Ukraine. Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba ameishukuru Ujerumani pia kwa kubadili msimamo kuhusu kupeleka silaha Ukraine wakati alipozungumza na waandishi habari akiwa na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock. Baerbok alifanya ziara ya kushtukiza katika mji wa Bucha, ulio nje ya mji mkuu Kyiv, ambako wanajeshi wa Urusi wametuhimiwa kwa kufanya uhalifu wa kivita. Kuleba ameusisitizia Umoja wa Ulaya uiruhusu Ukraine kuwa mwanachama.
Biden akutana na Draghi mjini Washington
Wakati haya yakiarifiwa rais wa Marekani Joe Biden na mwenzake wa Italia, Mario Draghi, wamekutana katika ikulu ya Marekani jana Jumanne. Draghi anazuru Marekani katika ziara inayonuiwa kuonesha umoja dhidi ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na pia kutoa fursa ya kutafuta njia pana za kuutafutia ufumbuzi mzozo huo.
Draghi amesema viongozi wanapaswa kufanya kazi kwa bidii kuelekea uwezekano wa kutafuta usitishwaji wa mapigano na kuanza upya mashauriano ya maana. Draghi aidha amedokeza kwamba nchini Italia na barani Ulaya watu wanataka mauaji ya kiholela na machafuko Ukraine yakomeshwe.
Rais Biden hakuzungumzia matamshi ya Draghi na maafisa wa Marekani wanaonekana kuwa na mashaka kwamba kuna kuna njia ya kuyaanzisha tena mazungumzo wakati huu. Avril Haines, mkurugenzi wa Biden anayehusika na usalama wa taifa alizungumza awali Jumanne akisema kwamba Ukraine na Urusi zinaamini zinaweza kupata mafanikio katika uwanja wa vita kwa wakati huu kwa hiyo hawaoni mwanya wa mazungumzo yakisonga mbele angalau katika kipindi kifupi kijacho. Haines pia alisema rais wa Urusi Vladimir Putin amejiandaa kwa mzozo wa muda mrefu.
Kauli hizo tofauti kuhusu Ukraine zinadhihirisha ukaribu wa Italia kijiografia na vita hivyo na mahusiano ya karibu ya kiuchumi na Urusi, ambayo inatoa asilimia 40 ya gesi asili ya Italia. Pia kuna hali ya wasiwasi inayoongezeka nchini Italia kuhusu kupeleka silaha nchini Ukraine.
Biden na Draghi wamesisitiza juu ya uhusiano wa karibu baina ya nchi zao na kazi yao Ukraine.
afp, ap, reuters