Ukraine yazima mashambulizi ya Urusi
29 Aprili 2024Jeshi la Ukraine limesema limefanikiwa kuzima mashambulizi yapatayo 55 ya Urusi katika vijiji kadhaa vya kaskazini na magharibi mwa Novobakhmutivka, kijiji ambacho Moscow imedai kukidhibiti.
Mapambano makali yaliripotiwa mwishoni mwa juma katika eneo la mashariki mwa Ukraine, ikiwa ni pamoja na kijiji cha Ocheretyne, ambapo mapigano makali yameripotiwa jana Jumapili.
Soma pia: Jeshi la Ukraine lawarejesha nyuma wanajeshi wa Urusi
Vijiji hivyo vinapatikana kaskazini mwa mji wa Adviivka, ulionyakuliwa na wanajeshi wa Urusi mwezi Februari. Vikosi vya Moscow vimekuwa vikipata mafanikio zaidi katika mkoa wa Donetsk, lakini huko pia Ukraine imesema inaendelea kupambana vilivyo na adui.
Kamanda mkuu wa jeshi la Ukraine Oleksandr Syrsky amesema hapo jana kuwa wanajeshi wake wamerejea kwenye safu mpya za ulinzi katika maeneo ya magharibi, huku Kyiv ikionya pia kwamba Urusi itajaribu kushinda baadhi ya mapambano kabla ya sherehe yake ya Mei 9.
Kamanda Syrsky amekiri kwamba hali ya nchi hiyo kwenye uwanja wa vita imezidi kuwa mbaya baada ya vikosi vya Urusi kuteka kijiji kingine cha mashariki cha Novobakhmutivka.
Ziara ya rais wa China na mazungumzo ya kibiashara kati ya UAE na Ukraine
Rais wa China Xi Jinping anatarajiwa kufanya ziara nchini Ufaransa kuanzia Mei 6 huku vita nchini Ukraine na Mashariki ya Kati vikitarajiwa kuwa kwenye ajenda ya majadiliano na mwenzake Emmanuel Macron. Baadaye rais Xi ataelekea katika nchi za Serbia na Hungary. Kuhusu ziara hiyo Lin Jian, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema:
"Ziara hii ni ya kwanza ya rais wa China barani Ulaya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Ina umuhimu mkubwa katika kukuza mahusiano ya China na Ufaransa, Serbia na Hungary pamoja na maendeleo jumla ya uhusiano kati ya China na Ulaya. Pia ziara hii itafufua ari mpya katika maendeleo ya kuwa na dunia yenye amani."
Wakati huo huo, Ukraine na Umoja wa Falme za Kiarabu wamekamilisha mazungumzo ya kufikiwa makubaliano ya kibiashara, hii ikiwa ni kulingana na taarifa ya pamoja iliyotolewa leo Jumatatu kabla ya kusainiwa rasmi mkataba huo.
Soma pia: Ukraine yasema nusu ya misaada ya washirika wake inachelewa kupelekwa
Mkataba rasmi wa Ubia wa Kiuchumi (CEPA) utasaidia kuondoa au kupunguza malipo ya ushuru wa bidhaa mbalimbali, kuondoa vikwazo vya kibiashara na kurahisisha ufikiaji wa soko kwa wauzaji wa bidhaa kutoka kutoka pande zote mbili.
Aidha mkataba huo utasaidia kufufua uchumi wa Ukraine na kupiga jeki ujenzi wa viwanda muhimu pamoja na miundombinu mbalimbali, lakini pia kusaidia kuimarisha mifumo ya ugavi kwa nchi za Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini hasa kwa mauzo makubwa ya nje ya Ukraine kama vile nafaka, mashine na madini ya chuma.
(Vyanzo: DPAE, AFPE,RTRE)