1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine: Zelenskiy atembelea vikosi vya msitari wa mbele

Daniel Gakuba
6 Juni 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ameitembelea miji miwili ya mashariki iliyo karibu kabisa na uwanja wa mapambano dhidi ya uvamizi wa Urusi, ambapo jeshi la Ukraine linaarifiwa kuwa chini ya shinikizo kubwa.

Ukraine | Präsident Wolodymyr Selenskyj gedenkt der gefallenen Soldaten
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy (kulia) akisalimiana na mwanajeshi wa nchi yakePicha: Ukraine Presidency/ZUMSPRESS/picture alliance

Mkanda wa vidio uliotolewa na Ikulu ya rais Volodymyr Zelenskiy usiku wa kuamkia leo umemuonyesha rais huyo akizungumza na wanajeshi katika mji wa Lysychansk, na baadaye katika mwingine wa mashariki wa Soledar.

Soma zaidi: Rais Zelensky asema ushindi utakuwa wao dhidi ya uvamizi

Katika mkanda huo, Zelenskiy anawaambia wanajeshi hao kuwa wanachostahili kukipata ni ushindi, ambao lakini si kwa gharama yoyote.

Tangu nchi yake ilipovamiwa na Urusi tarehe 24 Februari, ni nadra sana rais huyo kutoka katika ngome yake mjini Kiev.

Ziara yawaongezea ari wapiganaji

Baada ya ziara yake katika miji hiyo, Zelenskiy alisema ameshuhudia kwa macho yake madhila yanayowakumba watu wa eneo hilo, na kupongeza ushujaa wao.

Mapigano katika mji wa Sievierodonetsk ni miongoni mwa makali zaidi tangu kuanza kwa uvamizi wa UrusiPicha: picture-alliance/AP Photo/D. Lovetsky

''Kwa kila niliyekutana naye, niliyesalimiana naye, niliyezungumza naye, niliona fahari,'' amesema Zelenskiy na kuongeza kuwa ziara yake imewaongezea ari na uthabiti wanajeshi wa Ukraine. 

Mji wa Lysychansk uko jirani na ule wa Sievierodonetsk ambao hivi sasa unakabiliwa na mapigano makali.

Soma zaidi: Vita vya Urusi na Ukraine vyaingia siku 100

Taarifa za jana zilieleza kuwa vikosi vya Ukraine vilikuwa vimepata mafanikio, kwa kuwarudisha nyuma wanajeshi wa Urusi na kuidhibiti nusu ya mji huo muhimu.

Hata hivyo, gavana wa mkoa wa Luhansk ulipo mji huo, Serhiy Gaidai amesema kupitia televisheni ya taifa ya Ukraine kuwa mkondo wa mambo ulibadfilika ghafla na vikosi hivyo vya Ukraine vilikuwa vikijikuta chini ya shinikizo kubwa.

Maeneo mengi ya ukanda wa Donbas mashariki mwa Ukraine yameharibiwa vibayaPicha: Nina Lyashonok/Avalon/ Photoshot/picture alliance

Ingawa hakutoa taarifa za kina, gavana huyo ameongeza kuwa wanajeshi wa Ukraine walikuwa wanasimama kidete kulinda eneo la viwanda katika mji wa Sievierodonetsk, wakati makabiliano makali kuwahi kushuhudiwa katika mji huo yakiendelea.

Urusi kuruhusu usafirishaji wa nafaka

Sambamba na mzozo huo wa vita kati ya Urusi na Ukraine, shirika la habari la Izvestia lenye mafungamano na serikali ya Urusi, limemnukuu afisa wa serikali mjini Moscow aliyesema kuwa Urusi itaruhusu usafirishaji wa nafaka kutoka bandari ya mji wa Odessa kusini mashariki mwa Ukraine, baada ya makubaliano ya pande tatu, ambazo ni Urusi, Ukraine na Uturuki.

Soma zaidi:Urusi yadhibiti karibu asilimia ishirini ya ardhi ya Ukraine

Hatua hiyo inajiri wakati bei ya bidhaa hiyo ikipanda sana kwenye soko la kimataifa.

Na wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov ameahirisha ziara aliyotarajiwa kuifanya nchini Serbia, baada ya mataifa jirani na Serbia kuinyima ruhusa ndege yake kupita katika anga yao.

 

-dpae, afpe, rtre

 

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW