1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine: Zelenskiy awafuta kazi wafanyakazi 28 wa ujasusi

Daniel Gakuba
19 Julai 2022

Siku moja baada ya kuwatimua mkuu wa idara ya ujasusi na mwendeshamashitaka mkuu wa serikali, Rais wa Ukraine Volodymir Zelenskiy amewafukuza maafisa 28 wa ujasusi, akiwatuhumu kutofanya kazi kwa ufanisi.

Präsident Selenskyj nimmt  am NATO-Gipfel teil
Rais wa Ukraine, Volodymir ZelenskiyPicha: UKRAINIAN PRESIDENTIAL PRESS SERVICE/REUTERS

Rais wa Ukraine Volodymir Zelenskiy amewafuta kazi watumishi 28 wa shirika la ujasusi la nchi hiyo, SBU, siku moja baada ya kumfungisha virago mkuu wa masuala ya ujasusi, Ivan Bakanov.

Katika hotuba yake kwa taifa ya kila jioni, Zelenskiy amesema kuwa waliofukuzwa wanatoka katika ngazi mbali mbali za shirika hilo, na kuongeza kuwa kwa ujumla, sababu za wao kuondolewa ni zile zile, kutokuwa na ufanisi wa kutosha kazini.

Hivi karibuni rais huyo alielezea kufadhaishwa kwake na ukweli kuwa mawakala zaidi ya 60 wa kijasusi na wale kutoka ofisi ya mwendeshamashitaka mkuu wa Ukraine wamesalia katika maeneo yaliyokamatwa na Urusi, kitendo ambacho serikali yake inakichukulia kama uhaini. Mwendeshamashitaka mkuu Iryna Venediktova pia ameachishwa kazi.

Mamluki wa Wagner watumiwa kwenye mapambano

Wakati huo huo wizara ya ulinzi ya Uingereza imesema Urusi imekuwa ikiwapeleka mamluki kutoka kampuni ya ulinzi ya binafsi ya Wagner kuwasaidia wanajeshi wake katika vita nchini Ukraine.

Maafisa wa Uingereza wamedai kampuni ya Wagner imeshusha viwango vya sifa kwa watu inaowaajiri na kujumuisha wahalifu na watu ambao siku za nyuma walikuwa hawakubaliki.

Taarifa ya wizara ya ulinzi ya Uingereza limesema ukweli kuwa mkuu wa kampuni hiyo Yevgeniy Prigozhin hivi karibuni alipewa tuzo ya juu ya heshima ya taifa kutokana na umahiri wake wa kijeshi, unaweza kuleta misuguwano baina ya jeshi la Urusi na kampuni hiyo ya mamluki.

tj/dj, jsi (Reuters, dpa)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW