1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine,Bajeti na Hoeneß magazetini

12 Machi 2014

Uwezekano wa kujiunga Crimea na Urusi baada ya kura ya maoni ya jumapili ijayo,bajeti ya serikali kuu ya Ujerumani,na hatima ya mwenyekiti wa timu ya Bayern Munich Uli Hoeneß ni miongoni mwa mada magazetini

Maandamano ya wapinzani wa kura ya maoni ya Crimea huko SimferopolPicha: Reuters

Tunaanzia lakini Ukraine ambako kila kitu kinaashiria mzozo kati ya wale wanaoelemea Urusi na wengine wanaoelemea nchi za magharibi unazidi makali.Gazeti la "Saarbrücker Zeitung" linaandika:"Kwa sasa kila kitu kinaonyesha kwamba matakwa ya wale wanaopendelea kujiunga na Urusi yataitikwa.Nchi za magharibi hazitoweza kuweka vikwazo milele.Na kila wakati unapopita ndipo nao uwezekano wa kurejea Crimea Ukraine utakapozidi kupungua.Kwa upande mwengine,mbinu hizi hizi ndizo zilizowafanya wale wanaounga mkono utawala wa Ukraine katika Ghuba ya Crimea na hasa watu wa jamii ya tatar,wawe wakijuliza kuhusu uhalali wa kuunganishwa na Urusi.Kwa namna hiyo mvutano wa kisiasa hautamalizika ,badala yake utazidi makali.

Waziri wa Fedha Wolfgang Schäuble Atabasamu

Gazeti la "Lausitzer Rundschau linamulika hali namna ilivyo nchini Ujerumani ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita na kuandika:"Wolfgang Schäuble anaweza kutabasamu:Anakurubia kukifikia kile ambacho mawaziri 12 waliomtangulia katika kipindi cha miaka 40 iliyopita hawakufanikiwa kukifikia:kusawazisha bajeti ya serikali kuu.Serikali itakapopitisha mswaada wa bajeti ya mwaka huu wa 2014 ikijumuisha miradi yote inayopangwa kugharimiwa katika kipindi kinachokuja,watakuwa na kila sababu ya kufurahikia.Furaha itakuwa kubwa zaidi kwakuwa hii sio tena ile ndoto ya kufikia bajeti iliyosawazika na ambayo baadae hufifia wakati ukweli unapowadia.Ukweli lakini ni kwamba ufanisi wa Schäuble umeambatana na werevu.Na werevu huu ndio chanzo cha kupatikana bajeti bila yn nakisi.

Waziri wa fedha wa serikali kuu ya Ujerumani Wolfgang SchäublePicha: DW/B. Riegert

Uli Honeß Matatani

Kesi dhidi ya mwenyekiti wa akilabu mashuhuri ya bayern Munich,Uli Hoeneß inafichua mepya kia siku zinapopita.Yepi mengine yatachomoza? Linajiuliza gazeti la "Kieler Nachrichten:"Euro milioni 15,Euro milioni 18 na Euro milioni 27:Viwango vya fedha ambazo Uli Hoeneß amekwepa kulipia kodi ya mapato vinazidi kupanda takriban kila wakati tangu kesi hiyo ilipoanza jumatatu iliyopita.Kiwango gani hasa cha fedha mwenyekiti huyo wa kilabu ya FC Bayern Munich amekichezea kamari,ikiwa wachunguzi wanahoji hivi vilivyotajwa hadi sasa ni vya chini?Na katika shughuli zipi nyegine amewekeza mamilioni hayo?Bia ya shaka sio katika shughuli za shirika dogo la kutengeneza soseji la Hoeneß.Na pengine sio pekee katika masoko ya hisa.Ndo kusema mengi mengine yatafichuliwa?

Uli Honeß akizungukwa na mawakilishi wake katika ukumbi wa mahakama mjini MunichPicha: Getty Images

Daniel:

Na kwa ripoti hiyo ya gazeti la "Kieler Nachrichten " ndio na sisi tunazifunga kurasa za magazeti ya Ujefumani kutoka Bonn...................

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW