Ukraine:Hatuhusiki na hujuma dhidi ya mabomba ya gesi
8 Machi 2023Uchunguzi uliofanywa na mashirika ya utangazaji ya umma ya Ujerumani ya ARD na SWR pamoja na gazeti la Die Zeit uliihusisha Ukraine na milipuko ya mwezi Septemba 2022 kwenyemabomba mawili ya kusafirisha gesi kati ya Urusi na Ujerumani.
Maafisa nchini Ujerumani, Sweden, Denmark, Uholanzi na Marekani walihusika na uchunguzi, limeripoti gazeti la Die Zeit. Kwa mujibu wa vyombo vya habari, ikiwemo gazeti la New York Times, wachunguzi mpaka sasa hawajapata ushahidi wa nani aliamuru hujuma hiyo.
Vikiwanukuu maafisa mbalimbali ambao hawakutajwa majina, vyombo hivyo vya habari viliripoti kwamba wanaume watano na mwanamke walitumia boti iliyokodishwa na kampuni inayomilikiwa na raia wa Ukraine aishiye nchini Poland kufanya shambulio hilo.
Soma zaidi:Marekani: Mripuko wa mabomba ya Nord Stream ilikua hujuma
Gazeti la New York Times liliripoti pia Jumanne kwamba maafisa wa Marekani walipitia taarifa za ujasusi zilizoashiria kuwa kundi linaloiunga mkono Ukraine ndilo lililohusika na milipuko hiyo. Lakini waziri wa ulinzi wa Ukraine, Oleksiy Reznikov, amekana kuhusika kwa serikali.
Kwangu mimi, ni hadithi ya kushangaza kidogo" alisema na kuongeza kwamba taarifa hiyo haihusiki chcochote na Ukraine.
Aliongeza kuwa "nadhani uchunguzi wa mamlaka rasmi utaelezea kwa undani."
Pistorius:Tusubiri ripoti rasmi ya uchunguzi
Akizumgumza kwenye mkutano wa waandishi habari mjini Stockholm, waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius, amezungumzia juu ya ripoti hiyo.
Amesema baadhi ya wataalamu wamezungumzia pia uwezekano kwamba shambulizi hilo lilikuwa operesheni ya uongo iliyofanywa na kundi linalojifanya kuwa la Waukraine.
Soma zaidi:Scholz, Biden waahidi kuendelea kuisaidia Ukraine
Amesema lengo la mpango huo ni kuiharibia sifa Ukraine, na kuongeza kuwa hii haitokuwa mara ya kwanza katika historia ya matukio kama hayo.
"Nasita kutoa tathmini ya wazi kuhusu utafiti huo." Alisema
Ameongeza kwamba kilicho muhimu zaidi, kwa sasa ni NATOna nchi zinazozunguka Bahari ya Baltic, bahari ya kaskazini,kulinda usalama.
"Tuje pamoja na kufanya kila kitu kulinda miundombinu yetu muhimu katika bahari." Alisisitiza
Urusi yaishutumu Marekani dhidi ya shambulizi hilo
Msemaji wa Baraza la Usalama la Taifa la Ikulu ya White House John Kirby alikataa jana kuzungumzia ripoti ya New York Times,akibainisha kuwa uchunguzi wa Denmark, Ujerumani na Sweden bado unaendelea.
Soma zaidi:Guterres alaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov Jumatano hii amezitaja ripoti hizo kuwa ghiliba iliyoratibiwa yenye nia ya kuwaficha wapangaji halisi wa shambulio hilo.
Rais wa Urusi Vladimir Putin na maafisa wake wameituhumu Marekani kupanga milipuko hiyo, ambayo waliielezea kama shambulio la kigaidi.