1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukuaji wa miji nchini Kenya unaongezeka kwa kiwango kikubwa

15 Juni 2023

Kongamano la kwanza nchini Kenya kuhusu ukuaji wa miji, Kenya Urban Forum, linaendelea mjini Naivasha ambapo wito wa uwekezaji zaidi kwenye miji unatolewa, ili kukidhi idadi ya watu inayoongezeka.

Kenia Wohnungsbaustelle
Picha: Michael Utech/Pond5/IMAGO

Ukuaji wa miji unapoendelea kushuhudiwa, ongezeko la watu katika maeneo ya miji nchini Kenya pia linashuhudiwa, na hivyo kuibua hitaji la kubuni mipango kuhakikisha haki za kibinadamu zinazingatiwa.

Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini Ragini Dallal ameitaja hii kama hatua muhimu ili kuyakabili majanga ya kimazangira, kibinadamu na kiuchumi alisema kuwa "Umasikini na mabadiliko ya tabia nchi yameendelea kuiathiri miji. Uboreshaji wa miundombinu na kuwepo kwa makaazi ya bei nafuu inahitajika kwenye miji nchini kenya. Ili kuangazia changamoto hizi, tunahitaji kuweka mikakati ya kuzuia na pia kusuluhisha.”Kenya kuwajengea nyumba wanajeshi wake

Kongamano la kwanza nchini Kenya kuhusu ukuaji wa miji, linaendelea mjini Naivasha, kaunti ya Nakuru, ambapo limewaleta pamoja wadau wa sekta binafsi na ya umma kutoka kote nchini na kimataifa. Gavana wa kaunti ya Siaya James Orengo, ambaye alimwakilisha mwenyekiti wa baraza la magavana, amehimiza uwekezaji zaidi kwenye maeneo ya miji.

"Uwekezaji kwenye miradi ya miji utahitajika kuongezeka. Tunapendekeza kuundwa kwa hazina ya kitaifa ya miji ili kuangazia mapungufu haya.”

Mtaa wa mabanda wa Kibera jijini NairobiPicha: Donwilson Odhiambo/SOPA Images/ZUMA Press Wire/picture alliance

Akilifungua rasmi kongamano hilo, Rais William Ruto ametetea hatua za kiuchumi ambazo amechukua licha ya kwamba watu wengi hawaziridhii. Amesema lazima maamuzi muhimu yafanyike ili kuboresha hali ya maisha ya watu.

"Kwa sasa miji ya Kenya inakuwa kwa kiwango cha asilimia tano kila mwaka, ambacho ni kiwango cha juu sana. Na kufikia mwaka 2050 asilimia 50 ya Wakenya watakuwa wakiishi mijini. Ni changamoto, lakini pia ni fursa tukichukua hatua zinazofaa.”

Soma: Joto kali linalosababishwa na ukuaji wa miji, linatishia maisha ya mijini

Maimunah Shariff mkurugenzi mkuu wa kitengo cha makaazi cha Umoja wa Mataifa, UN-Habitat, amesema zaidi ya asilimia 32 ya Wakenya wanaishi mijini kwa hiyo ni muhimu kuambatanisha kasi ya ukuaji wa miji na mahitaji ya idadi hii kubwa ya wakaazi mijini.

"Tunapaswa kuhakikisha kuna usawa kati ya mahitaji ya watu walio mijini na vijijini. Tayari Kenya inaongoza katika utekelezaji wa mfumo wa ugatuzi. Tunachohitaji sasa ni kusaidiana ili tuboreshe mfumo wa ukusanyaji wa rasilimali na tuunde njia za kipekee za kiuchumi.”

Rais Ruto ameagiza kuwepo na ushirikiano kati ya baraza la mawaziri na baraza la magavana nchini ili kujadili na kuambatanisha kwa haraka sera za serikali za kitaifa na serikali za kaunti kuhusu mipango ya maendeleo kwenye miji. Kongamano hilo la siku tatu litakamilika hapo kesho.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW