1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukuta wa kisiasa ni nini?

6 Septemba 2026

Vyama vya mrengo wa wastani nchini Ujerumani vinakataa kushirikiana na AfD, ambayo baadhi ya matawi yake yamethibitishwa kuwa ya siasa kali. Lakini sera hii, inayojulikana kama ukuta wa kisiasa, inazidi kushinikizwa.

Ujerumani Berlin 2025 | Maandamano makubwa dhidi ya AfD na kuunga mkono maadili ya kidemokrasia
Muda mfupi kabla ya uchaguzi mkuu wa Ujerumani mwaka 2025, maandamano makubwa yalifanyika kuipinga AfD na sera kali ya CDU kuhusu uhamiaji iliyotetewa na kiongozi wa upinzani wa wakati huo, Friedrich Merz.Picha: Christian Mang/Reuters

Ukuta wa kuzuia moto hujengwa ili kuzuia moto usisambae kutoka nyumba moja kwenda nyingine.

Katika siasa za Ujerumani, neno Brandmauer, yaani ukuta wa kuzuia moto, linatumika kuelezea msimamo mkali wa kutoshirikiana na vyama vinavyochukuliwa kuwa vya siasa kali. Kama ukuta wa moto unavyolinda majengo, ukuta huu wa kisiasa unakusudiwa kuilinda demokrasia.

Hadi sasa, mahakama haijatoa uamuzi kuhusu iwapo chama cha Alternative for Germany, AfD, kinapinga demokrasia. Ingawa Idara ya Ulinzi wa Katiba imeyataja baadhi ya matawi yake ya majimbo kuwa yenye siasa kali zilizothibitishwa za mrengo wa kulia, ni Mahakama ya Katiba pekee inayoweza kuamua iwapo chama hicho kinakwenda kinyume na Katiba kupitia mchakato wa kukipiga marufuku.

Pendekezo la kuwasilisha ombi la kuipiga marufuku AfD limejadiliwa mara kwa mara, lakini hadi sasa halijawasilishwa.

Moto unapozuka katika nyumba moja, kuta maalumu zinazostahimili joto kali husaidia kuzilinda nyumba jirani.Picha: Bernhard Kuh/Zoonar/picture alliance

Merz sasa halipendi neno Brandmauer

Haijulikani wazi ni nani aliyeanzisha dhana ya ukuta wa kisiasa. Hata hivyo, Friedrich Merz ndiye aliyechangia kwa kiasi kikubwa kuenea kwake.

Alipoanza kuhudumu kama mwenyekiti wa CDU Desemba 2021, Merz aliliambia jarida la Der Spiegel: "Chini ya uongozi wangu kutakuwa na ukuta dhidi ya AfD.”

Lakini sasa akiwa Kansela wa Ujerumani, Merz huepuka kutumia neno hilo na hukerwa anapoulizwa kuhusu hilo. Hata hivyo, anaendelea kuunga mkono maana yake: CDU haitaki kushirikiana na AfD wala chama cha mrengo wa kushoto cha Die Linke.

Katika mkutano wake mkuu wa mwaka 2018, CDU ilipitisha azimio la kutoshirikiana na vyama hivyo. Azimio hilo linakataa "miungano na aina nyingine zinazofanana za ushirikiano” na AfD au Die Linke.

Msimamo huo hauishii katika kukataa miungano rasmi na AfD. Wakati mwingine CDU imeunda makusudi wingi wa kura bila kutegemea AfD, huku wanasiasa wake wakikataa kuchaguliwa katika nyadhifa kwa kura za chama hicho.

Chama cha kiliberali cha FDP kilipitisha azimio kama hilo. SPD na chama cha Greens pia hufuata msimamo huo, ingawa havina maazimio rasmi.

Sahra Wagenknecht, mwanzilishi wa chama cha BSW, ana msimamo tofauti. Anapinga kutengwa kwa AfD na yuko tayari hata kuruhusu kuundwa kwa serikali inayoongozwa na chama hicho katika jimbo la Saxony-Anhalt, ambako uchaguzi unafanyika Septemba 6.

Kiongozi mwenza wa AfD, Alice Weidel, mara nyingi huwakosoa vikali bungeni Kansela Friedrich Merz wa CDU (katikati) na Makamu wa Kansela Lars Klingbeil wa SPD.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Katika serikali za mitaa hakuna ukuta madhubuti

Hata wanasiasa wa vyama vinavyodai kuulinda ukuta huo hawafuati kila wakati sera ya kuitenga AfD. Mifano miwili inajulikana zaidi.

Mwaka 2020, mwanasiasa wa FDP Thomas Kemmerich alichaguliwa kuwa waziri mkuu wa jimbo la Thuringia kwa msaada wa kura za AfD. Kansela wa wakati huo Angela Merkel alishtushwa na uchaguzi huo na, akiwa katika ziara ya nje, alitaka "ubatilishwe.” Kemmerich alijiuzulu siku chache baadaye.

Januari 2025, Bunge la Ujerumani liliidhinisha pendekezo la CDU la kuwazuia waomba hifadhi kuingia nchini, likisaidiwa pia na kura za AfD. Wakati huo Merz alikuwa kiongozi wa upinzani, muda mfupi kabla ya uchaguzi mkuu. Hadi leo, anakosolewa kwa kuvunja ukuta wa kisiasa.

Katika ngazi ya miji na manispaa, ukuta huo si madhubuti. Kuna mifano mingi ya wanasiasa wa vyama vingine kupiga kura pamoja na AfD katika mabaraza ya mitaa.

Hoja inayotolewa mara nyingi ni kwamba, kwa mfano, mpango wa kujenga kituo cha kulelea watoto hauwi mbaya kwa sababu tu AfD pia inauunga mkono.

Wakosoaji hata hivyo wanaonya kuhusu mchakato wa taratibu wa kuzoea kushirikiana na chama hicho. Wanasema hali hiyo inaweza kuifanya AfD ikubalike kisiasa, kabla ya ushirikiano wa ngazi ya manispaa kuhamia kwenye siasa za majimbo au serikali ya shirikisho.

Kuvunjwa kwa ukuta wa kisiasa: Kiongozi wa AfD jimboni Thuringia, Björn Höcke (kulia), akimpongeza Thomas Kemmerich wa FDP baada ya kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa jimbo hilo bungeni Februari 2020 kwa msaada wa kura za AfD.Picha: Star-Media/IMAGO

Je, inawezekana kuwapuuza asilimia 40 ya wapiga kura?

Maoni yanatofautiana kuhusu umuhimu wa ukuta huo. Vyama vya wastani—CDU, SPD na Greens—vinauona kama njia ya kulinda afya ya kisiasa na kidemokrasia. AfD inavituhumu vyama hivyo kwa kutumia sera hiyo kumdhoofisha mshindani wao wa kisiasa.

Kwa vyovyote vile, ukuta huo hauonekani kuidhuru AfD. Kinyume chake, uungwaji mkono wa chama hicho katika kura za maoni unaendelea kuongezeka—licha ya ukuta huo au pengine kwa sababu yake.

AfD ikiwa na nguvu kubwa, kama ilivyo katika sehemu nyingi za mashariki mwa Ujerumani, mara nyingi vyama vingine vyote hulazimika kuungana ili kuzuia serikali ya jimbo inayoongozwa na chama hicho.

Hali hii inaweza kuathiri uaminifu wa vyama vyenye itikadi zinazotofautiana sana. Mashariki mwa Ujerumani, kwa mfano, Die Linke—mrithi wa chama tawala cha zamani cha Ujerumani Mashariki, SED—imeonyesha kuwa tayari kushirikiana na CDU ya kihafidhina.

Ingawa CDU inakataa rasmi kushirikiana na Die Linke kama inavyokataa AfD, katika majimbo kadhaa inazidi kuwa vigumu kuzuia serikali ya AfD bila ushirikiano wa aina hiyo.

Wanasayansi wa siasa pia wanaonya kuhusu upungufu wa kidemokrasia iwapo matakwa ya wapiga kura wa AfD yataendelea kupuuzwa.

Hivi karibuni, Sahra Wagenknecht alisema kuhusu Saxony-Anhalt: "Si jambo la kidemokrasia kukitenga daima chama kinachochaguliwa na takriban asilimia 40 ya wapiga kura. Ukuta wa kisiasa umeshindwa.”

Muda mfupi kabla ya uchaguzi wa Saxony-Anhalt, AfD ya mgombea mkuu Ulrich Siegmund (kushoto) inaongoza kwa mbali dhidi ya CDU ya Waziri Mkuu Sven Schulze.Picha: Klaus-Dietmar Gabbert/dpa/picture alliance

Baadhi ya wana CDU wanataka ukuta ubomolewe
 

Baadhi ya wanasiasa wa CDU mashariki mwa Ujerumani wanatilia shaka umuhimu wa ukuta huo.

Hivi karibuni, jumuiya ya wafanyabiashara wadogo na wa kati ya CDU katika jimbo la Brandenburg iliwasilisha pendekezo la kutaka chama katika ngazi ya taifa kufuta au kulifanyia marekebisho makubwa azimio linalokataza ushirikiano na AfD. Pendekezo hilo liliondolewa baada ya kukosolewa vikali na uongozi wa chama.

Waziri Mkuu wa jimbo la Saxony, Michael Kretschmer wa CDU, ambaye anaongoza serikali ya wachache mjini Dresden, hivi karibuni aliliambia gazeti la Handelsblatt: "Yeyote ambaye bado anazungumzia kuta za kisiasa hajaelewa mabadiliko ya nyakati. Tunapaswa kuzungumza na kila mtu aliye tayari kuzungumza.”

Hata hivyo, Kretschmer bado anasisitiza kutoshirikiana na AfD.

Uongozi wa CDU katika ngazi ya taifa ungependa mijadala hiyo ikome. Thorsten Frei, mwenyekiti mpya wa kundi la wabunge wa CDU na CSU katika Bunge la Ujerumani, amesema hatavumilia matawi ya majimbo kwenda kinyume na msimamo wa chama.

Watu wengi wanaitaka CDU kuweka wazi msimamo wake dhidi ya AfD, lakini mashariki mwa Ujerumani upinzani dhidi ya kushirikiana na chama hicho ni mdogo zaidi.Picha: picture-alliance/dpa/ZB

"Marufuku ya kushirikiana na AfD ni uamuzi wa msingi wa CDU. Haiwezi kutafsiriwa tofauti katika kila jimbo,” Frei aliyaambia magazeti ya kundi la Funke.

Kansela Merz pia anaendelea kushikilia msimamo huo. Licha ya shinikizo kubwa na hali ngumu ya kisiasa katika majimbo ya mashariki mwa Ujerumani, anakataa ushirikiano na AfD pamoja na Die Linke.

Hata hivyo, swali bado linabaki: Katika siku zijazo, vyama vingine vitapataje wingi wa kuunda serikali bila kushirikiana na AfD?

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW