Ukweli mtupu badala ya hotuba za Jumapili kwenye mkutano wa Berlin
23 Februari 2009Masoko ya fedha ya kimataifa sharti yasimamiwe vizuri. Atakayeshindwa kufanya hivyo anapaswa kuadhibiwa. Hayo ndiyo maamuzi yaliyofikiwa kwenye mkutano wa nchi za Ulaya zilizo wanachama wa jumuiya ya nchi 20 zilizoendelea zaidi kiuchumi duniani, G20 uliofanyika jana mjini Berlin hapa Ujerumani. Makubaliano hayo pia ni ushindi kwa mwenyeji kansela wa Ujerumani Angela Merkel na mwito wake wa kutaka kuwepo uchumi endelevu.
Ni nadra kwa viongozi wa kisiasa kuwa washauri wazuri, lakini baada ya mkutano wa siku ya Jumapili mjini Berlin, inaonekana pendekezo hilo limeanza kujidhihirisha. Kwani kama kansela Merkela pamoja na viongozi wenzake wa kiume wangekutana mwaka mmoja kabla, sio tu Ulaya bali ulimwengu mzima, haungekabiliwa na shakashaka kuhusu ubepari.
Lakini baada ya kuporomoka kwa mifumo ya fedha na kuzuka mgogoro mkubwa wa kiuchumi, ni vigumu kutoutazama mkutano wa Berlin kuwa mkutano wa dharura uliochelewa na wa viongozi waliozembea majukumu yao. Hususan yakizingatiwa yaliyosikika yakisema na kuweza kusomwa katika muda wa saa chache za mkutano huo.
Bila shaka kila lililosemwa halikuwa jipya. Na tayari mtu anajiuliza kwa nini mambo haya hayakuzungumzwa wakati dalili za kwanza za kuporomoka kwa uchumi zilipoanza kujitokeza.
Juhudi za dhati za dakika za mwisho zinazofanywa na wanasiasa ni dhihirisho la wao kutofahamu kabisa au zinayapa ukweli madai kwamba mataifa yamesukumwa kwenye kona na mabenki na wanauchumi wanaowashawishi wabunge. Kwa kuwa sasa mambo yanajitokeza, kwanza kabisa kwa kuporomoka kwa kasi kubwa uchumi wa dunia na mabenki yanarajia msaada kutoka kwa wanasiasa walio dhaifu.
Kwa kulinganisha pengine bado viongozi hawajachelewa. Angalau hakukutolewa hotuba za Jumapili kwenye mkutano wa Berlin, bali maneno ya wazi yalizungumzwa. Bila kujitatanisha kansela Angela Merkel alikiri wazi mpango uliofikiwa mjini Washington Marekani mnamo mwezi Novemba mwaka jana wenye vipengee 47 unaolenga kuunda upya mifumo ya masoko ya fedha.
Mpango huo unajumulisha usimamizi makini usio kuwa na mianya, mfumo wa benki utakaoziwezesha kuwa na mitaji yake yenyewe kama kinga na kuimarisha sarafu za kimataifa iwapo uwezo wa taifa moja moja hautatosha kukabiliana na mgogoro wa kiuchumi.
Hatimaye, ingawa kwa kusitasita, mwenyeji wa mkutano huo Angela Merkel amesaidiwa katika juhudi zake za kuwa na mfumo wa kiuchumi wa masoko huru unaotilia maanani maswala ya kijamii. Angalau viongozi wenzake kutoka Uholanzi na Uhispania waliyashangilia mawazo ya kansela Merkel ya kuunda muongozo mpya wa uchumi endelevu, ambao angependelea usimamiwe na baraza la kiuchumi la Umoja wa Mataifa.
Rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy amesema mjini Berlin atapiga vita maeneo yanayopendwa na watu wanaopenda kukwepa kodi na wafanyakazi wa benki wanaotaka kujitajirisha kwa kujilipa marupurupu makubwa makubwa. Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown ameona uwezakano wa kuunda mfumo wa kiuchumi utakaohakikisha viwango vya chini vya gesi ya carbon angani katika siku za usoni.
Tusubiri kuona kitakachojitokeza kwenye mkutano wa jumiya ya nchi 20 zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani, G20, utakaofanyika Aprili 2 mwaka huu mjini London Uingereza.
Hata matokeo ya mkutano huo yatategemea bara la Ulaya, kwani nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wanakutana katika juma moja lijalo mjini Brussels kujadili na kukubaliana maswala ya mwisho ya umuhimu mkubwa. Pengine kwa matumaini ya kutokataa kuyazingatia makubaliano ya mkutano wa Berlin.