Ulaya, Arabuni wakutana kuijadili Syria
13 Januari 2025Mkutano huo wa Jumapili (Disemba 12) uliitishwa na Saudi Arabia, ambayo inapigania kuondoshwa kwa vikwazo ilivyowekewa Syria wakati wa utawala wa Assad, ikihoji kwamba kuendelezwa kwa vikwazo hivyo kutarejesha nyuma juhudi za ujenzi mpya wa Syria.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan Al-Saud, alisema mkutano huo uliwajumuisha pia washirika wa kimataifa na Uturuki, ambayo ni muhusika mkubwa wa kile kinachoendelea ndani ya Syria.
Soma zaidi: Mawaziri wa EU wajadili kulegeza vikwazo dhidi ya Syria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Ahmed al-Shaibani, pia alishiriki kwenye mkutano huo kwa kile ambacho al-Saud alisema ni ishara kwamba kusanyiko hilo lina ridhaa ya watu wa Syria wenyewe.
Al-Saud alisema washiriki wa mkutano huo walielezea kufurahishwa na hatua zinazochukuliwa na utawala mpya wa Syria katika eneo la kurejesha taasisi za nchi, kufuata mtazamo wa majadiliano na pande zote za Syria.
"Utawala wa Syria umetoa pia hakikisho la kukabiliana na ugaidi na kuanza mchakato wa kisiasa unaowajumuisha watu wote wa Syria ili kuhakikisha utulivu wa Syria na ulinzi wa mamlaka yake, na kwamba Syria si chanzo cha kitisho kwa nchi nyengine katika ukanda huu." Aliongeza.
Ulaya yasaka mustakabali mpya Syria
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock, alirejelea wito wake wa ushirikishwaji wa wote kwenye uendeshaji wa Syria na pia kuwepo kwa muafaka wa kitaifa.
Kandoni mwa mkutano huo, Baerbock alitowa wito wa kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua kwa vitendo vyote vya uhalifu vilivyotokea wakati wa utawala wa Assad, ingawa huku akionya kwamba fursa ya kuijengea Syria mustakabali mwema haipaswi kuachwa ikapotea licha ya wasiwasi uliopo katika jumuiya ya kimataifa.
Soma zaidi: Wanadiplomasia wa nchi za Kiarabu na Ulaya wakutana Saudia kuisaidia Syria
"Licha ya wasiwasi wote wenye mashiko uliopo, sisi - kama jumuiya ya kimataifa - hatutakiwi kuiwacha fursa ya mustakabali mwema kwa Syria kutupita. Ndio maana sisi kama Ujerumani na kama Ulaya tunachukuwa hatua za awal i na madhubuti: vikwazo dhidi ya ukoo wa Assad na wapambe wao, ambao wametenda makosa makubwa ya kihalifu wakati wa vita vya kusikitisha vya wenyewe kwa wenyewe, lazima viendelee." Alisema Baerbock.
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, alisema baada ya mkutano huo wa Riyadh kwamba mawaziri wa kigeni wa Umoja huo watakutana mwishoni mwa mwezi huu wa Januari kujadili jinsi ya kulegeza vikwazo ilivyowekewa Syria.
Hata hivyo, Kallas alisema uamuzi huo utategemeana na jinsi watawala wapya wa Syria wanavyotekeleza majukumu yao katika kipindi cha mpito cha kisiasa kinachojumuisha makundi mbalimbali baada ya kuangushwa kwa Assad.