Ulaya, China, Urusi kujadili makubaliano mapya na Iran
20 Mei 2018Mazungumzo hayo yana matumaini ya kuokoa makubaliano ya kinyuklia ya mwaka 2015, limesema gazeti la Ujeruamni leo Jumapili(20.05.2018).
Maafisa watakutana mjini Vienna katika wiki zijazo chini ya uongozi wa mwanadiplomasia mwandamizi wa Umoja wa Ulaya Helga Schmid kujadili hatua inayofuata baada ya uamuzi wa Mei 8 wa rais wa Marekani Donald Trump kujitoa kutoka katika makubaliano ya mwaka 2015 na Iran, gazeti la kila Jumapili la Welt am Sontag limeandika , likinukuu vyanzo za maafisa waandamizi wa Umoja wa Ulaya.
Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Urusi na China zitashiriki katika mkutano huo, lakini Marekani haitashiriki, limesema gazeti hilo. Haikufahamika mara moja iwapo Iran, ambayo imekuwa ikikataa miito ya kuzuwia mpango wake wa makombora hapo kabla , iwapo itashiriki.
Chini ya makubaliano ya mwaka 2015, Iran ilikubali kuzuwia mpango wake wa kinyuklia ili kuweza kuondolewa vikwazo vingi vya mataifa ya magharibi.
Moja kati ya malalamiko makubwa ya utawala wa Trump ilikuwa kwamba mkataba huo haukuhusisha mpango wa makombora wa Iran ama uungwaji wake mkono makundi yenye silaha katika mashariki ya kati ambayo mataifa ya magharibi yanayaona kuwa ni magaidi.
Kumshawishi Trump kufuta vikwazo dhidi ya Iran
Kukamilisha makubaliano mapya ambayo yataendeleza vifungu vya kinyuklia na kuzuwia juhudi za kuendeleza utengenezaji wa makombora pamoja na shughuli za Iran katika kanda hiyo kunaweza kumshawishi Trump kuondoa vikwazo dhidi ya Iran , gazeti hilo limesema.
"Tunapaswa kujiondoa kutoka katika jina la "makubaliano ya kinyuklia ya Vienna" na kuongeza vitu vichache vya ziada. Ni hivyo tu ambapo vitamshawishi rais Trump kukubali na kuondoa vikwazo tena," gazeti hilo limemnukuu mwanadiplomasia mwandamizi wa Umoja wa Ulaya akisema.
Hakuna maelezo ya haraka yaliyopatikana kutoka katika wizara ya mambo ya kigeni ya Ujerumani.
Mkuu wa masuala ya nishati wa Umoja wa Ulaya alitaka kuihakikishia Iran Jumamosi kwamba kundi la mataifa 28 ya Umoja huo yanaendelea kuwa na dhamira ya kuyaokoa makubaliano ya kinyuklia, na kuimarisha biashara na Iran.
Maafisa kutoka Umoja wa Ulaya, Ujerumani na mataifa mengine ambayo yamebakia katika makubaliani wamesema itakuwa maafa iwapo juhudi za EU zitashindwa kuyalinda makubaliano hayo.
Wawekezaji wameshindwa kuwekeza Iran
Iran imehangaika kufanikisha manufaa ya kifedha kutokana na makubaliano hayo, kwa sababu kwa sehemu vikwazo vilivyobaki vya Marekani kuhusiana na mpango wake wa makombora vimezuwia wawekezaji wakuu wa mataifa ya magharibi kufanya biashara na Iran.
Maafisa wanatafuta njia mpya kutokana na kufahamu kwamba itakuwa vigumu kwa makampuni ya Ulaya kuepuka vikwazo vipya vya Marekani, gazeti hilo limeripoti.
Gazeti hilo limesema makubaliano mapya yanaweza kujumuisha mabilioni ya dola ya msaada wa kifedha kwa Iran, sambamba na makubaliano ya Umoja wa Ulaya ambayo yanatoa mabilioni kama msaada kwa Uturuki kwa kuwachukua mamilioni ya wahamiaji na kufunga mipaka yake, hatua iliyosaidia kufikisha mwisho mzozo wa wahamiaji.
Iran na mataifa makubwa ya Ulaya zimeanza vizuri mazungumzo kuhusiana na jinsi ya kuokoa makubaliano hayo ya mwaka 2015 lakini itategemea juu ya nini kitatokea katika wiki chache zijazo, waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Mohammed javad zarif amesema wiki iliyopita.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Daniel Gakuba