1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya haitonunua gesi ya Urusi kwa sarafu ya taifa hilo

26 Machi 2022

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amepuuzilia mbali takwa la rais wa Urusi, Vladimir Putin la kuyataka mataifa ya Ulaya kununua gesi kwa sarafu ya Kirusi,.

Belgien | Russland-Ukraine Kriegsgipfel Emmanuel Macron und Olaf Scholz
Picha: Markus Schreiber/AP/picture alliance

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amepuuzilia mbali takwa la rais wa Urusi, Vladimir Putin la kuyataka mataifa ya Ulaya kununua gesi kwa sarafu ya Kirusi, huku akimshutumu rais huyo kuwa mwenye nia ya kutaka kuvikwepa vikwazo alivyowekewa kutokana na uvamizi wake wa Ukraine.

Macron aliwaambia waandishi wa habari baada ya Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya wa mjini Brussels kwamba hatua ya Urusi haipo katika makubaliano na haoni sababu ya kutekelezwa kwa jambo hilo. Rais Putin alitoa takwa hilo juma hili katikia kipindi hiki ambacho serikali yake inakabiliwa na vikwazo vikali vinavyoathiri uchumi wa taifa hilo, kutokana na hatua yake ya kuingia kijeshi nchini Ukraine.

Biden amemwambia Putin ameshindwa kuyatenganisha mataifa ya Magharibi.

Rais Joe Biden akimsalimia mwanajeshi wa MarekaniPicha: Evelyn Hockstein/REUTERS

Rais Joe Biden wa Marekani amesema Rais Vladimir Putin wa Urusi ameshindwa kuyagawanya mataifa ya Magharibi kwa vita vyake vya Ukraine. Umoja wa Kujihami wa NATO haujawahi kuwa pamoja kama ilivyo katika kipindi hiki. Rais Biden ambae alitua katika eneo la mpakani mwa Poland na Ukraine alisema Rais Putin amepata taswira tofauti kabisa baada ya uvamizi wake huo na kuongeza kwa kusema NATO itajibu mapigo kama Urusi itatumia silaha za kemikali.

Urusi yakiri wanajeshi wake zaidi ya 1,350 wauwawa katika mapigano Ukraine.

Kifaru kichochomwa moto mjini MariupolPicha: Mikhail Tereshchenko/TASS/dpa/picture alliance

Katika uwanja wa mapambano, jeshi la Urusi limesema idadi ya wanajeshi wake waliouwawa nchini Ukraine imefikia 1,351, waliojeruhiwa 3,825 na kuongeza kuwa limefanikiwa kuwaokoa raia 400,000. Akiyaeleza hayo mwakilishi wa mkuu wa majeshi wa Urusi, Sergei Rudskoi ameyahamakia mataifa ya Magharibi kwa kusema kupelekwa kwa silaha nchini Ukraine kunasababsisha kurefushwa kwa muda wa operesheni yao ya kijeshi.

Pamoja na kauli hiyo lakini silaha za nyongeza kutoka Ujerumani zimewasili nchini Ukraine. Silaha hizo ni pamoja na zana za kujikinga na makombora ya anga 1,500 aina nyingine ya MG, machine Gun 100. Kadhalika katika mzigo huo kuna aina milioni nane za silaha ndogondogo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Ujerumani DPA misaada mingine zaidi kutoka Ujerumani imeripotiwa kuingia katika ardhi ya taifa hilo ikiwemo madawa, makasha 350,000 ya chakula na magari ya kuwabebea wagonjwa.

Taarifa za kuuwawa kwa Jenerali Yakov Ryazantsev wa Urusi kwenye mapambano.

Kwa upande wake serikali ya Kyiv imesema vikosi vyake vimemuuwa kamanda wa jeshi la Urusi, Jenerali Yakov Ryazantsev. Mshauri wa rais wa Ukraine Oleksiy Arestovych amesema mauwaji hayo yamefanyika katika mapambano yaliotokea kusini mwa taifa hilo karibu na Kherson.

Maafisa katika mji wa kimkakati wa bandari wa Mariupol wanasema kiasi ya watu 300, walikuwa wamepewa hifadhi katika jengo la utamaduni wanaweza kuwa wameuwawa katika shambulizi la juma lililopita.

Katika hatua tofauti Marekani na Umoja wa Ulayaumetangaza kikosi kazi chenye lengo la kupunguza Ulaya kutegemea nishati asilia ya Urusi. Mpango huo unaoratibiwa na Rais Joe Biden na rais wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen una shabaha ya kusambaza katika eneo la Ulaya mita za ujazo bilioni 15 kwa mwaka huu pekee.

Chanzo: AFP/DPA

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW