Ulaya inatafuta njia ya kuijenga upya Libya
25 Agosti 2011Mkuu wa masuala ya mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, katika mkutano wa waandishi wa habari mjini Brussels, ametoa sura ya namna anavoufikiria mustakbali wa Libya utakavokuwa. Lakini amefanya hivyo kwa tahadhari. Msimamo wa pamoja wa Ulaya kuhusu Libya hauko. Madola makuu ya Umoja wa Ulaya, kila moja, lina maslahi yake yenyewe katika Libya. Umoja wa Ulaya unachechemea nyuma ya misimamo hiyo.
Wakati mkuu wa masuala ya kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, anangoja kuweko uhakikisho rasmi wa mabadiliko ya madaraka huko Libya, wanasiasa wa mataifa yalio wanachama wa Umoja wa Ulaya tayari wameshajionea ukweli wa hali ya mambo. Waziri wa mambo ya kigeni wa Italy, Frattini, amewataka waasi wa Libya wahakikishe kwamba mikataba iliofungwa na kampuni ya mafuta ya Italy, UNI, pamoja na utawala wa Gaddafi, sasa itaendelea kufanya kazi. Naye rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, anajaribu kutoa sura kwamba yeye ameyawezesha mapinduzi ya Libya yafanikiwe kutokana na uamuzi wake wa NATO iongoze harakati za kijeshi huko Libya. Pia yeye, bila ya shaka, anataka kupata uhakikisho kwamba makampuni ya Kifaransa yataendelea kupata kandarasi zenye minofu huko Libya. Pia Ujerumani imelipa baraza la taifa la mpito huko Libya mkopo wa kujishikiza wa dola milioni 100, hata kabla Umoja wa Ulaya haujazungumzia juu ya kuondosha vikwazo dhidi ya Libya. Pia waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki, Davutoglu, anajitia pia kimbelembele. Alikuweko Benghazi na leo ameitisha mkutano wa kwanza mjini Istanbul wa kikundi cha nchi zenye kuwasiliana na Libya.
Na vipi juu ya Umoja wa Ulaya? Umoja huo ulikuwa likizoni. Kama ilivyo kawaida huko Ubelgiji, tume ya Ulaya na baraza la mawaziri la nchi wanachama wa Umoja huo huenda likizoni katika mwezi wa Agosti. Huwachwa nyuma tu maafisa wa vyeo vya chini wenye kuangalia mambo, ambao pindi kuna dharura wanaweza kuchukuwa hatua. Lakini tangu mwisho wa wiki iliopita wafanya kazi wenye dhamana wameamriwa warudi Brussels. Catherine Ashton mwenyewe amerejea ofisini kwake na anashughuklika kupiga simu huku na kule. Lazima kabla ya kukutana na waandishi wa habari na kutangaza juu ya mipango ya kuijenga upya Libya akubaliane na mawaziri wa mambo ya kigeni muhimu wa nchi za Umoja wa Ulaya.
Mawaziri hao pia wako mapumzikoni. Kwanza watakutana Septemba 12 katika kikao cha kawaida kijacho. Kabla ya hapo kutafanyika mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni katika nchi inayoshikilia sasa urais wa Umoja huo, na mara hii ni Poland, hapo Septema 2. Catherine Ashton atauwachia Umoja wa Mataifa kazi ya kuijenga upya Libya, na umoja huo umetoa mwaliko kwa mkutano wa kilele mjini New York.
Umoja wa Ulaya, kama kitu cha kwanza, unataka fedha za Libya zilizozuiliwá katika mabenki kote duniani ziwachiliwe, na fedha hizo zipewe Baraza la taifa la mpito. Catherine Ashton amesema kuisaidia kifedha Libya ilio tajiri ni jambo muhimu. Licha ya hayo anataka sasa utungwe mpango juu ya namna ya kuijenga dola ya kidemokrasia huko Libya. Lakini nini kimefanyika katika ofisi ya Bibi Ashton mnamo miezi sita ilopita? Kwanini hakuna mpango wa aina hiyo makabatini? Hapo kabla Umoja wa Ulaya ulikuwa na ofisi ndogo ya mawasiliano mjini Benghazi, na pia nchi za umoja huo zilikuwa na ofisi za aina hiyo. Ofisi hizo sasa zinahitaji kuhamia Tripoli na kufungua hasa balozi.
Bibi Ashton ameyataja matatizo ya kuyashughulikia katika huo mpango unaotungwa: kuwapatia huduma za afya wananchi wa Libya, kukusanya silaha walizo nazo watu binafsi, kurejea tena harakati za kiuchumi na kuzijenga taasissi za kidimokrasia na vyama vya kisiasa. Katika mambo yote hayo manne Umoja wa Ulaya unataka kusaidia kwa haraka, japokuwa Bibi Ashton hajasema kwa namna gani. Hata hivyo, yeye anaona jukumu lake ni kuowanisha mipango ya misaada ya nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya. Hata sasa hivi yaonesha, kama vile ilivotokea katika mikasa iliolingana na huu wa sasa, huko Afghanistan au Iraq, kwamba nchi nyingi za Ulaya zinafanya yale zinayoyaona kuwa muhimu, bila ya kuowanisha harakati zao. Hasa Italy, kama mkoloni wa zamani wa Libya, na Ufaransa, kama mshirikia muhimu sana wa kiuchumi wa utawala wa zamani wa Gaddafi, zinataka kuhakikisha ushawishi wao unabakia Libya. Licha ya hayo, Umoja wa Ulaya na nchi zilioko katika Bahari ya Mediterranean zina masalahi muhimu kwamba Libya inaibakisha mipaka yake iwe salama. Wakimbizi kutoka Afrika wasiwachiwe kuweza kuitumia Libya ilio tulivu kuwa ndio njia yao ya kukimbilia hadi Ulaya. Utawala wa Gaddafi baada ya kutia saini mkataba na Italy uliuzingira mwambao wake na kuwaweka wakimbizi katika makambi. Hivyo hivyo ndivyo zinavotaka sasa nchi za Ulaya zilioko katika Bahari ya Mediterranean ifanyike.
Umoja wa Ulaya, kupitia jumuiya yake ya ECHO, inaendesha shughuli za kutoa misaada ya kiutu katika mpaka wa Libya na Tunisia. Huko wakimbizi 90,000 wanaangaliwa. Umoja huo umeshasaidia kuwarejesha makwao wafanya kazi wa kigeni 24,000 kutok Misrata. Ukishirikiana na Shirika la kimataifa la msalaba Mwekundu na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwasidia wakimbizi, UNHCR, Umoja wa Ulaya tangu miezi sita sasa umetoa misaada ya kifedha katika eneo hilo. Hadi sasa Umoja wa Ulaya na nchi wanachama zimetoa dola milioni 150 kama misaada ya kiutu na katika shughuli za juwahamisha watu..
Misaada hiyo sasa lazima iendelezwe kwa nguvu, mkono kwa mkono na shughuli za kisiasa. Kuna wasiwasi wa kweli kama Bibi Catherine Ashton yuko katika hali ya kuweza kuonesha uwezo wake wa kuongoza na kung'ara pale anapokweko. Tangu hapo, mwezi Machi mwaka huu alilaumiwa na Bunge la Ulaya huko Brussels kwamba hafai kwa wadhifa huo anaoushikilia.
Mwandishi Bernd Riegert/Othman Miraji/ZR
Mhariri Yusuf Saumu