Ulaya itayari kwa dhima kuu katika NATO
12 Februari 2026
Kumekuwa na hofu kuwa Marekani imeiwacha Ulaya pekeyake pamoja na Canada, wakiwa na dhima kubwa ya kuilinda Ulaya.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth hakuhudhuriamkutano wa leo wa mawaziri wa ulinzi wa NATO uliofunguliwa rasmi na Katibu Mkuu Mark Rutte na uliofanyika katika makao makuu ya jumuiya hiyo huko Brussels.
Kutowasili kwake kunakuja baada ya waziri wa mambo ya kigeniwa Marekani Marco Rubio kukosa kuhudhuria kikao kilichopita cha mawaziri wenzake wa kigeni wa NATO Desemba iliyopita.
Rutte kuridhika na hatua ya Ujerumani
Ni jambo la nadra sana kwa mawaziri wa serikali ya Marekani kukosa kuhudhuria mkutano wa ngazi ya juu kama wa mawaziri wa NATO, wachilia mbali mikutano miwili mfululizo.
Lakini naibu waziri wa ulinzi wa Marekani Elbridge Colby aliyehudhuria, amesema anaridhika na juhudi za Ulaya kugawana jukumu la ulinzi la NATO na Marekani.
Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte pia ameelezea kuridhika kwake hasa na mpango wa serikali ya Ujerumani kuongeza matumizi yake ya ulinzi kufikia chini ya yuro bilioni 153 ifikiapo mwaka 2029, hiyo ikiwa ni ongezeko la mara tatu ikilinganishwa na mwaka 2021.
Rutte vile vile amesema kuwa wakati Marekani inapostahili kuangalia zaidi masuala ya eneo la Pacific katika siku zijazo, Ulaya na Canada zinastahili kuchukua jukumu zaidi.
Kikubwa kilichojitokeza katika mkutano wa leo ni tangazo kwamba NATO itazindua mpango wa Arctic Sentry ambao ni jaribio la kumzuia Rais Donald Trump asikichukue kisiwa cha Greenland.
Mgogoro kuhusu Greenland umekwisha
Washirika wa Marekani katika NATO baada ya kupitishwa kwa mpango huo, wanasema wanaamini mzozo kuhusu Greenland umekwisha na huu ni wasaa wa kusonga mbele kutokana na mzozo huo na kujikita katika kipau mbele cha usalama wa Ulaya ambacho ni vita vya Urusi nchini Ukraine.
"Na ndio sababu tumezindua Arctic Sentry kwa kuzingatia ongezeko la shughuli za kijeshi za Urusi na nia ya China inayoongezeka ya eneo la kaskazini. Tutajadiliana pia kuhusu kuendelea kuiunga mkono Ukraine. Marekani inaendelea kuendesha juhudi za kuvimaliza vita hivyo kabisa, ila Urusi inaendelea kuyalenga maeneo wanakoishi raia, ikiwemo miundo mbinu ya nishati," alisema Rutte.
Ujerumani, Ufaransa na Denmark watashiriki katika shughuli za kijeshi zitakazofanyika chini ya mpango wa Arctic Sentry, ila hawajasema ni kwa njia gani. Finland na Sweden huenda pia wakahusika na Ubelgiji nayo inatafakari ni dhima gani itakayokuwa nayo kwenye mpango huo. Haijajulikana bado kjukumu itakalokuwa nalo Marekani.
Kitisho cha Trump mwezi uliopita cha kuitwaa Greenland, kisiwa chenye utawala wa ndani kilicho chini ya Denmark, kimeitikisa mno NATO. Dhima kuu ya NATO ni kuilinda mipaka ya wanachama wake 32.
Chanzo: AP/DPA