1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya katika juhudi mpya za amani Ukraine

Admin.WagnerD5 Mei 2014

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanashinikiza juhudi mpya za amani nchini Ukraine wakati nchi hiyo ikizidi kutumbukia katika kile ambacho rais wake wa mpito ameonya siku ya Jumatatu kuwa tayari ni vita.

Ukraine Donezk 3.5.14
Picha: Reuters

Rais Oleksander Turchynov ameiambia televisheni ya Ukraine kuwa vizuwizi vya barabarani vimewekwa kwenye maeneo ya karibu na mji mkuu kujihadhari na hila za Urusi tarehe 9 Mei, wakati Ukraine itakapoadhimisha kumbukumbu ya ushindi katika vita vikuu vya pili vya dunia.

Turchynov ambaye amevitayarisha vikosi vya Ukraine kwa ajili ya mapambano, na kurudisha utumishi wa laazima wa jeshi kutokana na hofu ya kuvamiwa na Urusi, amesema vita vimeanzisha dhidi ya nchi yake, na kwamba laazima wawe tayari kukabiliana na uvamizi huo.

Onyo hilo la rais Turchynov limekuja wakati taifa hilo la zamani la kisovieti likizidi kutumbukia katika ghasia, ambazo wengi wanahofu zinaweza kugeuka vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Wanamgambo wanaoiunga mkono Urusi wakilikagua gari katika mji wa Luhansk, mashariki mwa Ukraine.Picha: Reuters

Ujerumani yataka mkutano wa pili wa amani

Katika juhudi za dakika za mwisho kuepusha machafuko zaidi, mwenyekiti wa shirika la usalama na ushirikiano barani Ulaya OSCE Didier Burkhalter, anatarajiwa kufanya ziara mjini Moscow, wakati ambapo miito inazidi kutolewa kwa kundi lake kufanya upatanishi kati ya serikali mjini Kiev na waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine.

Ziara hiyo ya Burkhalter, ambaye pia ni rais wa Uswisi ilikubaliwa katika mazungumzo ya simu kati ya rais wa Urusi Vladmir Putin na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel Jumapili jioni.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier, amekiambia kituo cha Televisheni cha Ujerumani kuwa alikuwa katika mazungumzo na Warusi, Marekani, Umoja wa Ulaya na OSCE, kufanya mkutano wa pili wa amani mjini Geneva.

Juhudi za kwanza kuutatua mgogoro huo zilikubaliwa nchini Uswisi April 17. Lakini Urusi ilitangaza wiki iliyopita kuwa makubaliano hayo yamekufa baada ya Ukraine kuzidisha operesheni za kijeshi ambazo Moscow iliziita vita dhidi ya watu wake.

Wakaguzi wa shirika la OSCE wakiwasili katika uwanja wa ndege wa Berlin, baada ya kuachiliwa huru na wanamgambo wa Ukraine wanaotaka kujitenga.Picha: Reuters

Marekani yaitishia adhabu kali Urusi

Wakati vita vya maneno vikizidi kupamba moto, Urusi imeikosoa pia mipango ya kufanyika kwa uchaguzi wa rais kwa kuzingatia hali ya vurugu zinazoendelea nchini Ukraine. Msimamo wa Urusi umeweka uwezekano wa nchi hiyo kuwekewa vikwazo zaidi na Marekani dhidi ya sekta nzima nzima za uchumi wake ambao tayari umeanza kudorora.

Rais wa Marekani Barack Obama alionya kuwa mataifa ya magharibi yatachukuwa hatua kali za adhabu ikiwa Moscow itaendeleza kile alichokiita kuivuruga Ukraine. "Kuna njia hapa ya kutatua tatizo hili. Lakini Urusi bado haijaamua kusonga mbele, na vikwazo hivi vinawakilisha hatua inayofuata, na juhudu za maksudi kuibadili tabia ya Urusi," alisema Obama.

Serikali mjini Kiev na magharibi zinaituhumu Urusi kwa kuchochea vurugu katika taifa hilo la zamani la Kisoviet, madai ambayo Moscow inayakanusha. Wakati Ukraine inajiandaa na uchaguzi wa Mei 25, wanaotaka kujitenga nao wanaendelea na mipango yao ya kuitisha kura ya maoni kuhusu uhuru Jumapili ijayo.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,ape
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW