1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya kuanza kutoa chanjo pamoja

17 Desemba 2020

Ujerumani itaanza kutoa chanjo ya corona kuanzia Desemba 27 huku watu katika vituo vya kuwahudumia wazee wakipewa kipaumbele. Pamoja na Ujerumani, mataifa ya Ulaya pia yataanza kutoa chanjo kwa wakati mmoja.

Deutschland Coronavirus Impfzentrum Nürnberg Spahn Söder
Picha: Daniel Karmann/dpa/picture alliance

Waziri wa afya nchini Ujerumani Jens Spahn ametangaza hayo mnamo wakati Umoja wa Ulaya ukitarajia nchi zote wanachama wake zitaanza kutoa chanzo siku sawa pamoja. 

Kwenye taarifa, mawaziri wakuu wa majimbo 16 ya Ujerumani wamesema waziri wa Afya Jens Spahn ametangaza kuidhinishwa kwa chanjo iliyotengenezwa na kampuni ya BioNTech na usambazaaji wake utaanza kabla ya mwisho wa mwaka.

Ikizingatiwa kuwa Ujerumani ndiyo inashikilia kwa sasa urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya, ina maana kuwa huenda nchi zote za umoja huo zikaanza kutoa chanjo hiyo pia Desemba 27. Jens Spahn amesisitiza kuwa chanjo ni muhimu hasa wakati huu ili kukabiliana na virusi hivyo hatari.

Soma Zaidi: Pfizer na BioNTech: Chanjo ya Covid-19 ina ufanisi wa 90%

Spahn: Utoaji chanjo ndiyo njia pekee

"Katika siku hizi ngumu, siku ambazo virusi vinatuonesha jinsi vinavyoweza kushambulia, hasa kwenye nyumba za wazee na kuwahudumia wasiojiweza. Utoaji chanjo ndiyo njia pekee ya kumaliza janga hili na tumejitayarisha barabara kuchukua njia hiyo." Amesema Spahn. 

Rais wa kamisheni ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema huenda wakaanza kutoa chanjo siku moja.Picha: REUTERS/ O. Hoslet

Hapo jana, Waziri Mkuu wa Ufaransa Jean Castex alisema, huenda Ufaransa itaanza kuwachanja raia wake wiki ya mwisho ya Disemba, ikiwa masharti yote yatatimizwa.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, amesema mataifa yote kwenye umoja huo huenda yakaanza kutumia chanjo hiyo siku sawa, punde tu chanjo hiyo iliyotengenezwa na kampuni ya BioNTech kwa ushirikiano na Pfizer itakapoidhinishwa.

Kamisheni ya EU kutoa tangazo kuhusu idhini kwa chanjo

Kamisheni hiyo itatoa tangazo la mwisho punde tu mamlaka ya Ulaya inayosimamia chanjo na dawa (EMA) itakapotoa uamuzi wake wa mwisho, unaiotarajiwa kufanyika Disemba 21.

Nchi za Umoja wa Ulaya zimeapa kuanzisha kampeni za kutoa chanjo dhidi ya virusi vya corona kabla ya mwaka kumalizika mnamo wakati visa vya maambukizi vinazidi kuongezeka katika nchi kadhaa wanachama.

Ufaransa imesema itapokea dozi milioni 1.16 ya chanjo hiyo ifikapo mwisho wa mwaka na dozi nyingine tena milioni 2.3 baada ya miezi miwili ijayo
 
Mataifa ya EU yaimarisha masharti kupunguza maambukizi

Vifo kutokana na COVID-19 barani Ulaya, vinakaribia watu 500,000. Hapo jana, Ujerumani ilirekodi idadi ya juu zaidi ya vifo vya watu 952 ndani ya saa 24.

Inahofiwa huenda idadi ya vifo zaidi itaripotiwa ikizingatiwa takwimu kutoka jimbo la Saxony ambalo limeathiriwa zaidi hazikujumuishwa kwenye takwimu jumla ya kuanzia siku ya Jumanne.

Ujerumani tayari imeanza kutekeleza vizuizi vya kufunga shughuli ili kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona.Picha: Sean Gallup/Getty Images

Hapo jana, Ujerumani ilianza kutekeleza masharti zaidi ya kuzuia virusi kuenea ikiwa ni Pamoja na kufunga shule na maduka yanayouza bidhaa ambazo si lazima kwa matumizi ya kila siku.

Denmark, Ufaransa, Uturuki na UholanziUlaya yaimarisha vizuizi kukabiliana na corona pia zimeimarisha vikwazo vya kukabili virusi vya corona, huku Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez akitoa tahadhari kufuatia kuongezeka kwa idadi ya maambukizi.

Shirika la Afya Duniani , tawi la Ulaya, limeonya kuhusu maambukizi zaidi barani Ulaya mapema mwaka ujao na limezihimiza hatua maalum za tahadhari kuchukuliwa msimu wa sherehe za Krismasi na mwaka mpya.

Biden na Pence kupewa chanjo hadharani

Kwingineko rais mteule wa Marekani Joe Biden na makamu wa rais wa Marekani Mike pence wanatarajiwa kuchanjwa hivi karibuni.
Kulingana na maafisa wawili wanaofahamu mikakati hiyo, Biden atapewa chanjo yake hadharani wiki ijayo. Maafisa hao hawakutaka kutambulishwa kwa sababu hawaruhusiwi kuzungumzia hayo kwa umma.

Naye Mike Pence na mkewe wanatarajiwa kupewa chanjo ya corona hadharani siku ya Ijumaa kama hatua ya kuwapa wananchi Imani kuhusu chanjo hiyo. Ikulu ya Marekani imesema hayo.

Hatua hiyo inajiri katika wiki ya kwanza ya chanjo hiyo kutolewa kwa umma Marekani, taifa ambalo janga la corona limewaua zaidi ya Wamarekani 300,000.

(AFPE)

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW