Ulaya kuipa Tunisia msaada wa kupiga jeki miradi ya kiuchumi
11 Juni 2023Mkuu wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema wakati wa ziara yake ya pamoja na Mawaziri Wakuu wa Italia na Uholanzi kuwa Umoja wa Ulaya uko tayari kuipa Tunisia kifurushi cha Euro milioni 900 pamoja na euro milioni 150 katika msaada wa haraka. Amesema kando na biashara na uwekezaji, msaada huo utaisaidia Tunisia na usimamizi wa mipaka na kupambana na usafirishaji haramu wa binaadamu, pamoja na msaada wa kiasi cha euro milioni 100 mwaka huu.
Soma pia: Viongozi wa Ulaya wapo nchini Tunisia kujadili tatizo la uhamiaji
Von der Leyen, baada ya mazungumzo na Rais Kais Saied, amesema anatumai makubaliano ya Umoja wa Ulaya na Tunisia yatasainiwa katika mkutano ujao wa kilele wa Ulaya baadae mwezi huu.
Nchi hiyo ya Afrika Kaskazini, ambayo ina madeni makubwa na inayofanya mazungumzo na Shirika la Fedha la Kimataifa - IMF ya kupewa mkopo wa uokozi, ni mlango wa wahamiaji na waomba hifadhi wanaojaribu kuingia Ulaya kwa kufunga safari hatari baharini.