1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya kuwachukuwa watoto 400 wa wakimbizi walioko Ugiriki

11 Septemba 2020

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Horst Seehofer amesema Umoja wa Ulaya umekubali kuwachukua takribani watoto wakimbizi 400 walioachwa bila makaazi baada ya moto mkubwa kwenye kambi ya wakimbizi Ugiriki.

Deutschland Seehofer PK Moria Lager
Picha: picture-alliance/dpa/J. Carstensen

"Ujerumani na Ufaransa ndizo zitakazochukuwa nusu ya wakimbizi hao, ambapo kila nchi ikitoa makaazi kwa wakimbizi 100 au 150," alisema Seehofer alipokuwa akizungumza na waandishi habari, akiwa pamoja na Makamu wa Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Margaritis Schinas, aliyesema kuwa janga hilo limeongeza "umuhimu wa Umoja huo kufanyia marekebisho sera yake ya uhamiaji."
 

"Moria ni jambo linalotukumbusha sote kuwa tunapaswa tubadilike,” alisema Schinas, huku akithibitisha kuwa Halmashauri hiyo itatoa mapendekezo ya makubaliano mapya mnamo Septemba 30 juu ya uhamiaji na waomba hifadhi. 

Mpango huo umesimamishwa mara kwa mara kutokana na tofauti iliyojitokeza ya kugawanya wakimbizi au waomba hifadhi katika mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya, ambapo mataifa kama Poland, Hungary, Jamhuri ya Czech na Slovakia yamekataa kulazimishwa kuchukua wakimbizi, kitu ambacho kimetatiza juhudi za kufanyika mabadiliko katika Umoja huo. 

Kambi ya Moria kwenye kisiwa cha Lesbos iliyoteketea kwa moto.Picha: picture-alliance/dpa/S. Baltagiannis

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani alisema imani yake ni kuwa "mataifa wanachama ya Umoja wa Ulaya watakubali jukumu la kugawana wakimbizi."

Ujerumani ambayo kwa sasa inashikilia urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya ilisema imekubali kuchukua wakimbizi hao kufuatia ombi kutoka kwa serikali ya Ugiriki.

Uholanzi nayo kuchukuwa sehemu ya wakimbizi

Siku ya Alkhamis (Septemba 10), Uholanzi ilisema ingelichukuwa wakimbizi walio chini ya miaka 18 pamoja na familia zilizo na watoto. Waziri wa Nje Ankie Broekers-Knol alisema wakati kama huu "hatua zisizotarajiwa zinapaswa kuchukuliwa ili kuwasaidia wale walio na mahitaji."

Baadhi ya wakimbizi katika kambi ya Moria iliyoteketea kwa moto.Picha: picture-alliance/dpa/K. Ntantamis

Kwa ujumla wakimbizi 13,000 wamekuwa wakiishi katika kambi hiyo ya Moria ilioko nchini Ugiriki, ambayo ni kubwa kabisa barani Ulaya.

Kambi hiyo iliteketezwa kwa moto mapema wiki hii na kuwaacha maelfu ya wakimbizi wakiwa na mahitaji makubwa ya kupata makaazi mapya. 

Kisiwa cha Lesbos iliko kambi hiyo ni eneo muhimu la kuingia Ugiriki iliyo mwanachama wa Umoja wa Ulaya. Kutokana na ukaribu wake na Uturuki, kambi ya Moria imekuwa na wakimbizi wengi kupita idadi inayopaswa kuwa nayo. 

Serikali ya Ugiriki imesema moto huo ulianzishwa kwa makusudi na wakaazi wa eneo hilo waliokasirishwa na masharti ya kukaa karantini yalionuwia kudhibiti maambukizi zaidi ya virusi vya corona baada ya watu 35 kuambikizwa virusi hivyo katika kambi hiyo. 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW