1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya kuwekeza Amerika ya Kusini na Karibiki

17 Julai 2023

Umoja wa Ulaya umekutana na viongozi wa Amerika ya Kusini na visiwa vya Karibiki huku kukiwa na matumaini ya kurejesha upya uhusiano ulioingia doa kufuatia mgawanyiko juu ya biashara na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Rais wa Halmashauri kuu ya Ulaya, Ursula von der Leyen sambamba na rais wa Brazil Luis Inacio Lula da Silva katika mkutano wa kilele wa CELAC, mjini Brussels.
Brazil inataka washirika wake wa karibu kusimama upande wao katika nyakati hizi za sintofahamu.Picha: EMMANUEL DUNAND/AFP

Uwekezaji wa Ulaya kwenye maeneo hayo, unachukuliwa kama unaojibu uwekezaji wa China kwenye mataifa yanayoendelea kiuchumi. 

Mkutano huo wa kilele uliosubiriwa kwa muda mrefu na wa kwanza kati ya Brussels na jamii ya Amerika ya Kusini na Visiwa vya Karibiki, CELAC tangu mwaka 2015, umelenga kuangazia masuala kadha wa kadha yaliyodhoofisha mahusiano baina ya pande hizo.

Rais wa Brazil Luis Inacio Lula da Silva amesema alipokaribishwa mjini Brussels mapema leo na rais wa Halmashauri kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen kwamba katika nyakati hizi za sintofahamu, Brazil inataka marafiki zao wa karibu kusimama upande wao. Alisema hayo kabla ya kuanza kwa mkutano huo wa kilele.

"Kwa miaka sita nchi yetu imejiweka mbali na siasa za kimataifa, na kupuuza umuhimu wa uhusiano mzuri wa kidiplomasia, biashara na hata uwekezaji wa nje. Na tumerudi serikalini ili kuirejesha Brazil kama muhusika mkuu katika nyanja ya kimataifa. Na muhimu zaidi tunataka kuimarisha mjadala na Umoja wa Ulaya juu ya sio tu maendeleo ya viwanda na ukuaji, bali pia suala la hali ya hewa."

Von der Leyen kwa upande wake ameahidi Umoja wa Ulaya utawekeza yuro bilioni 45 katika uchumi wa Amerika ya Kusini chini ya programu ya Global Getaway, hatua inayochukuliwa kama inayoijibu China na mpango wake wa maboresho ya miundombinu ya barabara wa Belt and Roads, inaoutekeleza kwenye mataifa yanayoendelea kiuchumi.

Ulaya imekubali kuwekeza mamilioni ya yuro kwa mataifa ya Amerika ya Kusini na Visiwa vya karibiki ili kurejesha uhusiano ulioharibikaPicha: YVES HERMAN/REUTERS

Amesema fedha hizo zitapelekwa hadi ifikapo mwaka 2027, chini ya mipango ya uwekezaji kwa washirika wake hao pamoja na Visiwa hivyo vya Karibiki. Washirika hao wamekubaliana kwamba fedha hizo zitaelekezwa kwenye miradi ya nishati safi na malighafi muhimu za afya na elimu, hii ikiwa ni kulingana na Von der Leyen.

Soma Zaidi:Scholz: Nimefurahi kuona Brazil imerejea katika jukwaa la kimataifa 

Miradi hiyo ni pamoja na upanuzi wa mitandao ya mawasiliano katika eneo la Amazon nchini Brazil, na kuimarisha mtandao wa 5G nchini Jamaica, umeme kwenye usafiri wa umma huko Costa Rica na uwekezaji katika migodi ya Lithium nchini Argentina na Chile.

Lula da Silva ataka mkataba wa biashara utakaowezesha mataifa kushughulikia changamoto.

Kwa upande mwingine, mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell alisema kabla ya kuanza kwa mkutano huo wa kilele kwamba hatarajii makubaliano yaliyosimama ya biashara huria kati ya Umoja wa Ulaya, Brazil, Argentina, Uruguay na Paraguay kuhitimishwa haraka, ingawa anaamini pande zote zitashirikiana ili kufikiwa kwa msimamo wa pamoja hadi itakapofika mwishoni mwa mwaka huu. Makubaliano hayo yamesimama tangu mazungumzo yalipomalizika mwaka 2019.

Rais Lula da Silva ametoa fikra zake juu ya suala hilo akisema wangependelea kuwa na makubaliano yatakayowezesha pande mbalimbali kushughulikia changamoto za sasa na siku zijazo, huku akisisitizia umuhimu wa kuzingatiwa kwa suala la manunuzi ya umma katika mahusiano hayo ya kibiashara.

Viongozi hao wa Ulaya na CELAC wamekutana mjini Brussels, huku wanadiplomasia wakiwa wanapambana kukubaliana namna ya kuandika taarifa ya pamoja ya mwisho, ambayo Ulaya inataka itoe msimao mkali dhidi ya Moscow. Ikumbukwe kwamba mataifa hayo 33 ya Amerika ya Kusini na Karibiki hayana msimamo mmoja kuelekea vita vya nchini Ukraine, wakati baadhi yakitaka kulinda ushirikiano wao na Urusi ama kufikiwa makubaliano ya amani.

Soma Zaidi: Lula ahimiza upatanishi wa pamoja kumaliza mzozo nchini Ukraine

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW