Ulaya kuwekeza mabilioni Ukraine
19 Septemba 2025
Ulaya imeamua kuwekeza mabilioni katika sekta ya utengenezaji wa silaha za Ukraine ili iweze kujilinda vyema. Ikiwa mkakati huu utafanikiwa, sekta ya silaha ya Ukraine hatimaye itaweza kusaidia pia wanajeshi wa Marekani na Ulaya katika vifaa vya kisasa, kama droni na teknolojia nyingine za kijeshi zinazotengenezwa wakati vita vinaendelea dhidi ya Urusi.
Ulaya imeanza kukitazama kitisho cha Urusi kwa uzito zaidi tangu utawala wa pili wa Trump ulipoanza kutoa ujumbe unaoonesha kwamba wanachama wa Jumuiya ya kujihami ya NATO hawapaswi kuitegemea Marekani kuwalinda. Kwa upande wake, Ukraine inatafuta uwekezaji ili kuzidisha mara tatu uzalishaji wa silaha zake, kupunguza utegemezi wa washirika wa Magharibi katika vita dhidi ya Urusi, na pia kuzuia migogoro ya baadaye.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky anasema Ukraine ina uwezo wa kutengeneza silaha angalau za dola bilioni 30 kwa mwaka na kwamba haihitaji msaada wa kifedha pekee, bali pia inatarajia makubaliano ya leseni na ushirikiano wa utengenezaji silaha na makampuni ya Magharibi.
Trump akerwa na msimamo wa Putin
Rais wa Marekani Donald Trump amesema amekerwa Rais wa Urusi Vladimir Putin kutokubali kumaliza vita vya Ukraine, licha ya uhusiano wake wa karibu na kiongozi huyo wa Urusi.
Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Marekani, Fox News, Trump pia alikosoa wanachama wa Ulaya wa Jumuiya ya NATO kwa kuendelea kununua mafuta ya Urusi, akipendekeza kuwa Moscow ingeweza kuwa tayari zaidi kujadiliana kuhusu makubaliano ya amani kama Ulaya ingetumia nishati kidogo kutoka Urusi.
"Sikufurahishwa na Umoja wa Ulaya, au tuseme NATO, nilipowaona wakinunua mafuta kutoka Urusi. Namaanisha, inapaswa kuwa sisi Marekani tunakuja na msimamo mkali."
"Na, unajua, nilichukua msimamo mkali, kama unavyojua, dhidi ya India, kwa sababu walikuwa wikinunua mafuta. Na hatimaye, kama bei ya mafuta itashuka au ikiwa Urusi haitauza mafuta, hawana budi ila kukubali makubaliano."
"Wakati nchi za Umoja wa Ulaya au nchi za NATO, zinanunua mafuta kutoka Urusi, si jambo zuri kabisa. Hayo si makubaliano tunayoyataka."
Trump pia alisisitiza kuwa Marekani itasaidia katika mchakato wa amani baada ya vita vya Urusi nchini Ukraine kumalizika.
Wakati huo huo, Mkuu wa shirika la ujasusi la Uingereza, MI6, Richard Moore, amesema hana ushahidi wowote unaoonyesha kuwa Rais Putin ana nia ya kufikia makubaliano ya amani isipokuwa Ukraine ikikubali kushindwa.
Moore alisema Putin "amechukua jukumu kubwa kuliko anavyoweza kushughulikia" na aliidharau Ukraine katika vita hivi vinavyoendelea.