1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya na mataifa mengine yakabiliwa na wimbi la joto kali

18 Julai 2023

Ulaya sambamba na mataifa mengine duniani yanakabiliwa na viwango vya juu vya joto na viongozi wameonya juu ya hatari za kiafya na kuwataka watu kuchukua tahadhari kwa kunywa maji kwa wingi na kujikinga na jua kali.

Jahr 2022 heißeste Sommer in Europa | Hitzewelle Paris
Picha: Francois Mori/AP/picture alliance

Viwango vya joto vimevunja rekodi Jumanne hii barani Ulaya na maeneo mengine duniani kutoka Jimbo la California huko Marekani hadi nchini China. Wimbi hilo la joto kali halionyeshi dalili zozote za kupungua. Viwango vikubwa vya joto vitakavyoshuhudiwa barani Ulaya, ni katika visiwa vya Italia vya Sardinia na Sicilia ambako kutashuhudiwa zaidi ya nyuzi joto 48.8 katika kipimo cha Celsius.

Ugiriki inakabiliwa na mioto ya misitu iliyowalazimu watu kuyakimbia makazi yao. Kaskazini-magharibi mwa mji mkuu Athens, wingu kubwa la moshi lilitanda kwenye msitu wa Dervenohoria na katika mji wa bahari wa Kouvaras, huku huduma za dharura zikipambana na mioto ya misitu katika maeneo mbalimbali karibu na mji mkuu na kwa siku ya pili mtawalia. Mji maarufu wa pwani wa Loutraki unakabiliwa pia na mioto ya misitu, ambapo Meya wa mji huo amesema watoto 1,200 wamehamishwa jana kutoka sehemu za mapumziko.

Mamlaka ya afya nchini Italia imetangaza kuanzia jana Jumatatu, hali ya tahadhari kwa miji 20, kutoka kusini mwa Napoli hadi kaskazini mwa Venice ambapo viwango vya joto vinatarajiwa kufikia nyuzi joto 44°C huko Catalonia na katika visiwa vya Balearic. Huko Lanusei karibu na pwani ya mashariki ya Sardinia, hatua kadhaa zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na watoto kuruhusiwa tu kucheza ufukweni nyakati za asubuhi wakati jua halijawa kali.

Soma pia: Mamilioni ya watu wapambana na ongezeko la Joto duniani

Mjini Roma ambako kunatarajiwa hadi nyuzi joto 42 katika kipimo cha Celsius, watu wamebadili mfumo wa mavazi na hata chakula, wakipendelea kuvaa nguo nyepesi na kula vyakula laini kama kachumbari. Baadhi ya wakazi huko Cagliari wameripotiwa kupatwa na presha ya kushuka kutokana na joto kali.

Wito wa shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa

Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa Duniani (WMO) limekumbushia kuhusu athari za ongezeko la joto duniani na kusema ulimwengu unapaswa kujiandaa kwa mawimbi yanayoongezeka ya joto kali. John Nairn, mshauri mkuu katika shirika hilo la WMO amesema:

Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Petteri TaalasPicha: FABRICE COFFRINI/AFP

"Tunashuhudia ongezeko la matukio haya mara kwa mara na viwango vya juu vya joto. Na hii inaendana na tafiti zote kuhusu ongezeko la joto duniani. Matukio haya yataendelea kuongezeka kwa kasi na dunia inapaswa kujiandaa kikamilifu kukabiliana na mawimbi ya joto kali."

Soma pia: Karibu watu 100 wafariki kutokana na joto kali India

Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Petteri Taalas amesema hali hii mbaya ya hewa ina athari kubwa kwa afya ya binadamu, mifumo ya ikolojia, uchumi, kilimo, nishati na hata usambazaji wa maji, huku akisisitiiza kuwa hali hii inadhihirisha kuwa tunapaswa haraka iwezekanavyo na kwa usahihi kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi kwa mazingira.

(Chanzo: AFPE)