1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya kuheshimu haki za binadamu au kulinda mipaka yake?

24 Novemba 2023

Licha ya juhudi za miongo kadhaa za kuurekebisha, mfumo wa uhamiaji wa Ulaya unasalia kuwa mbovu na usiofanya kazi ipasavyo.

Wakuu wa nchi za Umoja wa Ulaya
Wakuu wa nchi za Umoja wa UlayaPicha: Fabrizio Bensch/REUTERS

Mitazamo kuhusu wahamiaji na wakimbizi barani Ulaya inazidi kuwa mikali katika wakati ambapo nchi zinapitia wakati mgumu kuamua iwapo ziilinde mipaka yake au ziheshimu haki za binadamu. 

Chini ya saa 24 baada ya kuwasili katika bandari ya kusini mwa Italia, watu 60 walioponea safari hatari ya boti kutoka Libya, walipewa amri za kuikuondoka nchini humo. Baadhi walitokea Bangladesh, wengine Syria na Misri.

Walikuwa baharini kwa muda wa saa 10 katika boti mbili zilizokuwa zimejaa kupita kiasi, ambapo jumla ya watu 258 walikuwa wamebebwa.

Waliokolewa na meli ya uokozi ya shirika la msaada wa kiutu la Madaktari wasio na Mipaka, kilomita 50 kutoka pwani ya Libya mnamo Oktoba 6.

Walipofika katika nchi kavu mjini Salerno, eneo lililo kusini mwa mji wa Napoli, walipelekwa katika kituo cha kuwasajili wahamiaji na wakaambiwa wasaini makaratasi.

Soma pia:Ujerumani inaangazia kusaka suluhu ya uhusiano kati yake na Uturuki ambao mara zote umekuwa mgumu

Baadae wakakusanyika nje ya kituo cha treni, wakiwa wamechoka na wamechanganyikiwa.

Wafanyakazi wa shirika la misaada la Kikatoliki la Caritas waliposikia kwamba wahamiaji hao wako katika kituo cha treni na wanafukuzwa nchini humo, walikwenda kwa haraka katika kituo cha Salerno pamoja na mawakili na wafanyakazi wa kujitolea mapema asubuhi, wakawapa chakula, majina ushauri wa kimsingi wa kisheria.

Walipofika katika eneo hilo, wafanyakazi hao waliwauliza wahamiaji hao iwapo walifahamu kile walichokuwa wanakitia saini ila kwa pamoja walisema hawakufahamu na wakasema pia hakuna aliyewauliza iwapo wanataka kuwasilisha ombi la kutaka kulindwa kimataifa.

Taarifa muhimu bado changamoto kwa wahamiaji

Wahamiaji na wanaotafuta hifadhi waliowasili kwa mara ya kwanza katika fukwe za Ulaya.

Wakiwa wamepewa ushauri mbaya na jamaa na marafiki, taarifa finyu au huduma mbaya za tafsiri, wengi wao huishia kufanya maamuzi ya haraka na ambayo hayawezi kubadilishwa tena.

Ujerumani: Rasimu ya kuwarudisha watu katika mataifa yao

01:45

This browser does not support the video element.

Mara nyingi wahamiaji hawana taarifakuhusiana na haki zao, kwa sehemu fulani kutokana na ukosefu wa wakalimani wakati wa mchakato wa kuwatambua.

Kulingana na utafiti uliofanywa na shirika lisilo la kiserikali la International Rescue Committee, ni asilimia 17 tu ya wahamiaji wanaowasili Italia, wanapokea taarifa za kutosha kuhusiana na haki zao.

Soma pia:Uingereza yaandaa mkataba mpya wa kupeleka wahamiaji Rwanda

Chini ya sheria za Umoja wa Ulaya zilizopewa jina Dublin Regulation, wahamiaji wanastahili kuwasilisha maombi ya kutafuta hifadhi katika taifa la kwanza la Umoja wa Ulaya wanaloingia.

Iwapo watasafiri katika nchi nyengine ya Umoja wa Ulaya na kuchukuliwa na mamlaka, wanastahili kurudishwa katika nchi waliyowasili au kusajiliwa kwa mara ya kwanza.

Sheria hii inaziwekea mzigo mzito nchi ambazo zimewapokea wahamiaji wengi kwa njia ya bahari kama vile Ugiriki, Italia, Malta na Uhispania.

Lakini Desemba mwaka 2022, Italia ilisimamisha kutumika kwa sheria hiyo, hii ikimaanisha kwamba, iwapo mhamiaji atakwenda kwa mfano Ujerumani na akamatwe huko, basi hatoweza kurudishwa Italia, ambayo ndiyo nchi ya kwanza aliyoingia Ulaya.

Badala yake atalazimika kuanza kuwasilisha ombi la kwanza la kutafuta hifadhi nchini Ujerumani.

Meloni akiri mzigo wa wahamiaji

Waziri Mkuu wa Italia Georgia Meloni, ambaye ndiye kiongozi wa kwanza wa siasa kali za mrengo wa kulia nchini Italia tangu Vita vya Pili vya Dunia, amekiri kwamba uhamiaji umekuwa changamoto yake kubwa katika mwaka wake wa kwanza serikalini.

Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni akiwa na Kansela wa Ujeruma Olaf ScholzPicha: Fabrizio Bensch/REUTERS

Mnamo mwezi Aprili, serikali yake ilipitishasheria nyengine mpya ya kuwafuatilia wahamiaji ambapo wanaowasilisha maombi ya kutafuta hifadhi wanawekwa katika vituo vya kuwashikilia wakimbizi hadi wanapopata vibali vya kuishi n chini humo.

Wasiowasilisha maombi au wale ambao maombi yao yanakataliwa katika hatua ya kwanza, wanapewa amri za kuondoka nchini humo na wanapewa siku saba kufanya hivyo.

Soma pia:Ujerumani huenda ikawatimua maelfu ya waomba hifadhi wa Nigeria

Huku shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR  hivi majuzi lilitoa taarifa likisema hatua nzito na za haraka zinahitajika katika maeneo ya mipakani.

Shirika hilo limesisitiza pia kwamba watu wanastahili kupewa fursa ya kueleza hali binafsi ya ukosefu wa usalama wanayokabiliwa nayo, licha ya nchi wanayotoka.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW