1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yaanza biashara ya mabadilishano na Iran

1 Aprili 2020

Iran na Umoja wa Ulaya zimekamilisha mauziano ya kwanza chini ya mfumo wa ubadilishanaji bidhaa na huduma uliowekwa ili kukikiuka vikwazo vya Marekani dhidi ya Jamhuri hiyoya Kiislamu.

Iran Josep Borrell und Mohammed Javad Zarif
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Naroozi

Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zimefanya mauzo ya mwanzo kabisa kwa kutumia mfumo wa kubadilishana bidhaa uliowekwa ili kuvikwepa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, na mataifa hayo ya Ulaya yameweza kutuma vifaa vya matibabu kwenye taifa hilo la Kiislamu.

Taarifa iliyotolewa jana na wizara ya mambo ya kigeni ya Ujerumani inasema kwamba hatua hiyo ni matokeo ya majaribio ya muda mrefu ya Ulaya kuuzindua mpango huo uitwao INSTEX, ambao unahusisha biashara halali na Iran licha ya kuwepo vikwazo vya Marekani.

Ofisi hiyo ya mambo ya kigeni ya Ujerumani imesema kuwa bidhaa hizo tayari zimewasili Iran, ikiongeza kuwa mfumo huo wa INSTEX utatumika pia kwenye mauziano mengine na mfumo kama huo wa upande wa Iran uitwao STFI.

Vipi INSTEX inafanya kazi?

Rais Donald Trump wa Marekani aliitoa nchi yake kwenye mkataba wa nyuklia na Iran mwaka 2018.Picha: Getty Images/W. McNamee

Mfumo huo ulibuniwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita baada ya Marekani kurejesha upya vikwazo vikali dhidi ya sekta ya mafuta ya Iran kufuatia hatua ya Rais Trump kujiondowa kwenye makubaliano ya kimataifa kati ya Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani juu ya mpango wake nyuklia. 

Chini ya mfumo INSTEX, bidhaa na huduma zinabadilishwa badala ya kuuzwa kwa fedha, jambo linalokwepa matumizi ya moja kwa moja ya fedha na vikwazo vya Marekani. 

Awali, kampuni za Ulaya hazikuwa na la kufanya zaidi ya kusitisha biashara na Iran na kufuta miradi ya pamoja kwa hofu ya kuadhibiwa na Marekani. 
Kwa mujibu wa makubaliano ya nyuklia na Marekani, China, Urusi, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, mwaka 2015 Iran iliamuwa kuiunda upya programu yake ya nyuklia ili isiweze kutengeneza bomu la atomiki.

Iran ilivyoelemewa

Rais Hassan Rouhani wa Iran anasema nchi yake imekumbwa na majanga matatu makubwa ndani ya miongo minne: vita na Iraq, vikwazo vya Marekani na kirusi cha corona.Picha: picture-alliance/AA/PRESIDENCY OF IRAN

Matokeo yake vikwazo vingi vikaondolewa na biashara na Tehran ikarejea, lakini mwezi Mei 2018, Trump aliiondoa kwenye makubaliano hayo, na mwaka mmoja baadaye, Iran ikaanza kujivua taratibu majukumu yake kwenye mkataba huo.

Taifa hilo la Ghuba ya Uajemi ni moja ya maeneo yenye maambukizi mengi sana ya ugonjwa wa COVID-19 duniani, likiwa na wagonjwa takribani 45,000 na likipoteza watu 2,900 kutokana na kirusi hicho cha corona, kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni kabisa zilizotolewa na wizara ya afya ya nchi hiyo.

Rais Hassan Rouhani wa Iran alisema hapo jana kwamba hali ya tahadhari nchini humo - ambayo imesababisha shule na maduka kufungwa na kuzuwia watu kutembea ovyo - huenda ikaongezewa muda baada ya tarehe 8 mwezi huu wa Aprili. 

Kiongozi huyo amelielezea janga hili kuwa mgogoro wa tatu kuikumba Iran ndani ya miongo minne iliyopita: la kwanza likiwa vita vyake na Iran baina ya mwaka 1980 na 1988 na la pili likiwa kurejeshwa upya kwa vikwazo vya Marekani mwaka juzi, 2018.