1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yaanza kuona afueni Marekani yatapatapa na Corona

Saumu Mwasimba
5 Mei 2020

Marekani inakabiliwa na hali ngumu ya kuudhibiti ugonjwa wa Covid-19 lakini kwa upande mwingine inapambana katika vita vya maneno na China kuhusu vilikoanzia virusi vya Corona

Spanien Barcelona | Coronavirus | Sport im Freien
Picha: Reuters/N. Doce

Kwa kuanza kuitupia jicho hali hapa barani Ulaya,nchi nyingi zimeondowa kwa kiwango fulani vizuizi vilivyowekwa kudhibiti kusambaa kwa virusi vya Corona,yakiwepo matumaini katika nchi hizo kwamba maradhi hayo huenda yamevuka kilele chake.

Ni baada ya nchi zilizoathirika zaidi barani humo kuanza kuona idadi ya wanaokufa inapungua ikiwa ni baada ya miezi takriban miwili ya kufungwa kwa nchi nyingi.

Picha: picture-alliance/Winfried Rothermel

Nchini Ujerumani kiwango cha kusambaa kwa maambukizi kimekadiriwa kufikia asilimia 0.71 hii ikiwa na maana kwamba katika watu 100 walioambukizwa wanaweza kuwaambukiza kwa wastani watu wengine 71 na mana yake ni kwamba idadi ya maambukizi mapya itashuka kadri muda unavyokwwenda.

Takwimu rasmi zinaonesha Ulaya ni bara lililoathirika zaidi likiwa na vifo 145,000.Marekani waliokufa wanakaribia 68,700.Kwa ujumla hiyo ni zaidi ya asilimia 85 ya vifo vilivyotokea duniani kufuatia janga hilo. Lakini licha ya Marekani kuwa katika hali ngumu ya kupambana kuudhibiti ugonjwa huo ikulu ya White House imeongeza mapambano yake dhidi ya China.

Waziri wa mambo ya nje Mike Pompeo amesema kuna ushahidi mkubwa unaoneesha virusi vya Corona vilitokea kwenye maabara moja ya Wuhan huko China,mji ulikotokea kisa cha kwanza kabisa na mripuko wa virusi vya Corona. 

Madai ya Pompeo aliyoyatowa Jumapili yalipingwa vikali jana Jumatatu na shirika la afya duniani WHO pamoja na mtaalamu wa Marekani wa  magonjwa ya mripuko na mshauri wa serikali Anthony Fauci.Rais Donald Trump kwa upande wake amekiri kwamba hali ni mbaya nchini mwake na watakaokufa ni kati ya watu 75,000 mpaka 100,000 nchini humo.

Picha: Reuters/C. Barria

Ingawa anakubaliana na hilo rais huyo wa Marekani alijitenga na mkutano wa kimataifa uliofanyika jana uliotishwa na WHO wa kuunga mkono juhudi za kimataifa za kutafuta na kutengeneza chanjo kupunguza maambukizi ya virusi hivyo.

Nchi zenye nguvu barani Ulaya,Japan na Canada zilichangishwa kiasi kikubwa kabisa cha fedha katika mkutano huo uliofanikiwa kuchangisha dola bilioni 8. Umoja wa Ulaya ukizungumzia vita vya China na Marekani umesema hawajawahi kuwa wajinga  linapokuja suala la kuishughulikia China na jana Uingereza ilisema China ina masuli ya kujibu kuhusu maelezo iliyotowa kuhusu mripuko wa virusi vya Corona.

Kwengineko barani Asia,India imeanza operesheni kubwa inayuhisha meli na ndege kuwarudisha mamia kwa maelfu ya raia wake waliokwama nchi za nje kufuatia janga hili.India ilisimamisha safari zote za ndege za  kimataifa za kuingia nchini humo mwishoni mwa mwezi March. Nchi hiyo sasa imepeleka meli mbili kuelekea Maldives na Umoja wa falme za kiarabu ambako kuna raia wake milioni 3.3.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Josephat Charo