Ulaya yakodowa macho Ujerumani na Italia jumapili inayokuja
2 Machi 2018
Marchi nne, au jumapili inayokuja mengi yatabainika kuhusu Ulaya: Italia wapiga kura kulichagua bunge jipya na Ujerumani itafahamika kama serikali ya muungano wa vyama vikuu au GroKo kati ya wahafidhina na wana Social Democrat itaendelea kutawala. Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya inajiandaa pindi hali mbaya ikitokea" alisema hayo mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya Jean-Claude Juncker wiki iliyopita. Wasi wasi wake mkubwa unasababishwa na matokeo ya uchaguzi wa bunge nchini Italia: Ukosefu wa wingi madhubuti unaweza kuifanya nchi hiyo isitawalike.
Zoezi la uchaguzi miongoni mwa wanachama wa SPD linatia hofu
Jean Claude Juncker amelitaja pia zoezi la uchaguzi wa wanachama wa SPD kuwa ni sababu nyengine ya kuingiwa na hofu: Bila ya ridhaa ya wanachama wa SPD, itamaanisha serikali ya muungano wa vyama vikuu au Groko haitoundwa na kwa hivyo nchi inayoongoza barani Ulaya itakuwa haina serikali pia.
Kansela Angela Merkel anayatambua yote hayo. Katika hotuba yake ya hivi karibuni bungeni kuhusu sera ya Ujerumani kuelekea Umoja wa ulaya, kansela Merkel alisema "wanahitaji mapambazuko barani Ulaya."Na hivyo ndivyo ilivyotajwa katika mkataba ya kuunda serikali ya muungano kati ya wahafidhina na wana Social Democrat, uliochapishwa mapema mwezi uliopita. "Mwaka 2018 ni mwaka unaobidi kufungua njia za mageuzi" alisema katika hotuba yake bungeni.
Wataalam hawaoni kishindo kikubwa kutokea
Ndo kusema zahma itapiga mjini Brusels ikiwa serikali ya muungano wa vyama vikuu haitoweza kuundwa mjini Berlin? Janis Emmanouillidis wa kituo cha sera za Ulaya mjini Brussels anasema anasemay "Haamini kama kutatokea patashika. Bila ya shaka hali hiyo haitowafanya watu wapumuwe. Watu wanaamini serikali ya muungano wa vyama vikuu itaundwa. Kama haitokuwepo basi itamaanisha, aina fulani ya wasi wasi utatanda barani Ulaya kwasababu mmojawapo wa wadau muhimu angekuwa hana serikali ambayo itakuwa na uwezo wa kudhamini maamuzi muhimu."
Lakini hata kama serikali ya muungano itaundwa, Angela Merkel hatoangaliwa tena kama "kiongozi asiyebishika barani Ulaya" kama alivyokuwa kabla ya uchaguzi mkuu wa September 2017. Jarida la Marekani Times linamtaja rais wa Ufaransa Emmanuel Macron "kuwa mshika bendera mpya wa ulaya. Katika wakati ambapo chama cha kansela Merkel CDU kilipoteza zaidi ya asili mia 7 katika uchaguzi mkuu uliopita, Macron aliibuka na ushindi mkubwa katika uchagizi wa rais mwaka huo huo wa 2017 nchini Ufaransa.
Macron anyemelea nafasi ya Merkel kama mshika bendera barani Ulaya
Katika wakati ambapo Macron anawakaribisha mjini Paris viongozi washupavu mfano wa Donald Trump, Putin na Erdogan, Merkel amekuwa kwa miezi sasa akijaribu kujadiliana na viongozi wa vyama vya kisiasa ili kuunda serikali ya muungano.
Macron hawezi kumifikia daraja ya Merkel anasema Stefan Seidendorf, ambae ni naibu mwenyekiti wa taasisi ya uhusiano kati ya Ujerumani na Ufaransa mjini Ludwigsburg. Anahoji hata hivyo Macron anayatumia kikamilifu madaraka ya jamhuri ya tano, naiwe kidiplomasia au kijeshi ili kuimarisha ushawishi wa Ufaransa barani Ulaya na ulimwenguni kwa jumla.
Mwandishi: Hasselbach,Christoph/ Hamidou Oummilkheir
Mhariri:Josephat Charo