1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yakumbuka miaka 75 tangu kumalizika WWII

8 Mei 2020

Ulaya inaadhimisha kumbukumbu ya miaka 75 tangu kumalizika Vita Kuu ya Pili ya Dunia katika hali ya huzuni kutokana na janga la virusi vya corona ambavyo vimesababisha kufutwa kwa maadhimisho ya kumbukubmu hiyo. 

Berlin Brandenburger Tor, Ansicht Kriegszerstörungen
Picha: picture-alliance/akg-images

Kwa mara ya kwanza Ujerumani imeitangaza siku hiyo kwa mwaka kuwa ya mapumziko ya umma. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ataungana na Rais Frank-Walter Steinmeier kuweka mashada ya maua kwenye eneo la kumbukumbu la wahanga wa vita na utawala wa kidikteta la Neue Wache, na kufuatiwa na hotuba kutoka kwa rais.

Tofauti na kwengineko barani Ulaya, ambako Mei 8 huadhimishwa kila mwaka kama Siku ya Ushindi Ulaya, kumbukumbu ya utawala wa Manazi nchini Ujerumani kusalimu amri bila masharti yoyote kwa washirika wao, siku zote imekuwa siku ya kufanya kazi nchini humo.

Hata hivyo, mji wa Berlin umetangaza leo kuwa siku ya mapumziko ya umma ili kukumbuka miaka 75 iliyopita wakati vita ambavyo vilisababisha mauaji ya zaidi ya watu milioni 50 vilimalizika barani Ulaya.

Kansela Angela Merkel na Rais Frank-Walter Steinmeier Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Hatua hiyo imesababisha baadhi kutoa wito siku hii itangazwe kuwa ya mapumziko ya umma ya kudumu, hali iliyozusha mjadala mkali nchini Ujerumani. Akiupinga wito wa kuipa siku hii umaarufu, kiongozi wa chama kinachofuata siasa kali za mrengo wa kulia na kinachopinga wahamiaji, AfD, Alexander Gauland amesema siku hii ina utata.

Magwaride yafutwa Ulaya

Aidha magwaride ya kuadhimisha siku hii yamefutwa kote barani Ulaya, katika wakati ambapo dunia inapambana na janga la COVID-19 ambalo limesababisha maambukizi kwa zaidi ya watu milioni 3.7 kote ulimwenguni, ukiwa mzozo mkubwa tangu kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Awali, Urusi ilipanga kufanya maonyesho makubwa ya gwaride Mei 9 ambayo ni Siku ya Ushindi ya nchi hiyo, huku viongozi wa dunia akiwemo Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron wakiwa kwenye orodha ya wageni waalikwa.

Urusi ikiwa inaelekea kuwa na maambukizi makubwa ya virusi vya corona, Rais Vladmir Putin ataweka maua kwenye kaburi la kumbukumbu la mwanajeshi asiyejulikana, kabla ya kulituhubia taifa.

Rais wa Urusi, Vladmir PutinPicha: picture-alliance/ZUMAPRESS/A. Druzhinin

Katika Jamhuri ya Czech, ambako masharti yaliyowekwa kuzuia kuenea kwa virusi vya corona yameondolewa kabisa, wanasiasa watawasili kwa nyakati tofauti kuweka mashada ya maua kwenye eneo la Viktov Hill mjini Prague, ili kuzuia mawasiliano.

Huko Ufaransa maadhimisho yamepunguzwa, ingawa Rais Macron atahudhuria tukio la kumbukumbu kwenye Ikulu ya nchi hiyo. Nchini Uingereza, magwaride ya mitaani ambayo hufanywa na maveterani yamefutwa.

Wakati huo huo, maveterani wanane wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia wataungana na Rais wa Marekani, Donald Trump kuweka mashada ya maua katika kumbukumbu ya miaka 75 tangu kumalizika vita hivyo barani Ulaya.

(AFP, AP)