Ulaya 'yamfokea' Trump mkutano wa Davos
21 Januari 2026
Uwepo wa Trump mjini Davos unatajwa na wachambuzi kuwa "onesho la kutunishiana misuli" kati yake na viongozi wa Ulaya, wakati tishio lake la kukitwaa kisiwa cha Greenland likielekea kuugawa muungano wa kijadi wa Bahari ya Atlantiki vipande vipande.
"Nakwenda kwenye eneo zuri sana nchini Uswisi, ambako nina hakika nangojewa kwa hamu kubwa. Nadhani tutafanikisha jambo huko ambapo NATO itafurahia na sisi tutafurahia sana. Ngoja uone nitakachofanya kuhusiana na Greenland." Alisema kiongozi huyo wa Marekani muda mfupi kabla ya kuondoka Ikulu ya White House kuelekea Davos siku ya Jumanne (Januari 20).
Hotuba ya Trump kwenye jukwaa hilo la kilimwengu ilitazamiwa kutolewa saa 8:30 kwa majira ya Ulaya ya Kati, na baada ya hapo alisema angelikuwa na vikao kadhaa vya pembezoni juu ya kadhia ya Greenland.
Trump, anayesisitiza umuhimu wa Greenland kwa usalama wa Marekani dhidi ya Urusi na China kwenye eneo la theluji la Aktiki, alisema ameshaifanyia mengi NATO kuliko mtu mwengine yeyote na kwamba ni wakati wa washirika wa NATO kuisaidia Marekani kwenye suala hili.
Ulaya yafoka kuhusu Greenland
Huko Davos kwenyewe, viongozi mbalimbali wa Ulaya wamekuwa wakitowa kauli kali dhidi ya kitisho cha Trump kuitwaa Greenland, kisiwa ambacho kisiasa na kijamii ni sehemu ya Denmark, licha ya kuwa kwake kijiografia ndani ya Amerika ya Kaskazini.
Rais Gitanas Nauseda alisema "kwa Marekani kuchukuwa hatua kama hiyo dhidi ya mwanachama mwenzake wa Muungano wa Kijeshi wa NATO ni sawa ni kuuwa Muungano huo."
Utabiri kama wa Nauseda ulitolewa pia na Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Bart De Wever, ambaye alisema Trump "amechupa mipaka mingi kwenye suala la Greenland."
"Kuwa mshirika mtiifu ni kitu kimoja na kuwa mtumwa dhaifu ni jambo jengine. Mukirejea nyuma leo, mutapoteza heshima yenu. Tukigawika hapa, ndio mwisho wa miaka 80 ya Uatlantiki." Alisema waziri mkuu huyo wa Ubelgiji, ambaye kwa kutumia neno Uatlantiki alimaanisha Muungano wa Kijeshi wa NATO unaoyakusanya pamoja mataifa ya Ulaya na Marekani.
Kanada yaashiria khofu kwa Trump
Si viongozi wa Ulaya pekee waliopaza sauti zao kupingana na sera za Marekani Kwanza zinazopigiwa chapuo na Trump.
Waziri Mkuu wa Kanada, Mark Carney, aliliambia jukwaa hilo la uchumi la Davos kwamba mfumo wa kilimwengu unaoendeshwa na Marekani "umekabiliwa na mpasuko unaotokana na ushindani wa mataifa yenye nguvu na kufifia kwa utawala wa sheria."
Bila kumtaja kwa jina Trump, Carney alisema kinachojengeka sasa ni "mfumo wa mwenye nguvu kutimiza matakwa yake kwa kutumia vitisho vya kiuchumi na kijeshi."
Trump alianza kuzungumzia mipango ya kuitwaa Kanada kama jimbo la 53 la Marekani muda mrefu, lakini mazungumzo hayo yalififia, hadi usiku wa Jumanne alipochapisha kwenye mtandao wake wa kijamii ramani inayozionesha Kanada na Venezuela zimefunikwa bendera ya Marekani, ikimaanisha kutwaliwa nchi hizo na Marekani.