1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yaongeza vikwazo Belarus

15 Novemba 2021

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya wameufanyia marekebisho mfumo wa vikwazo ambavyo umoja huo unaweza kuviweka dhidi ya utawala wa Belarus na kutanua vikwazo, wakati ambapo mzozo wa wahamiaji ukiendelea.

Belarus | Grenze zu Polen | Grenzübergang Kuznica
Picha: State Border Committee of the Republic of Belarus/TASS/picture alliance

Taarifa iliyotolewa Jumatatu na Umoja wa Ulaya imeeleza kuwa Baraza Kuu la umoja huo limerekebisha mfumo wake wa vikwazo kwa kuzingatia hali katika mpaka wa nchi za Umoja wa Ulaya na Belarus, ili kukabiliana na namna utawala wa Belarus unavyowatumia binaadamu kwa madhumuni ya kisiasa.

Umoja wa Ulaya unamshutumu Rais wa Belarus, Alexander Lukashenko kwa kuwapeleka wahamiaji, wengi wao wakiwa kutoka Mashariki ya Kati, kwenye mpaka wa Belarus na Poland ambako wanajaribu kuingia kwenye maeneo ya umoja huo.

Ulaya yasimama pamoja

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell amesema uamuzi wa leo unaonesha nia ya umoja huo kusimama pamoja kupinga wahamiaji kutumiwa kwa malengo ya kisiasa. Borrell amesema wanapinga mfumo huo wa kinyama na usio halali.

''Vikwazo siku zote huwa na ufanisi, kwa sababu vinawaathiri watu, utajiri wao na uwezo wao wa kutembea. Na leo tunaidhinisha aina mpya ya vikwazo dhidi ya watu wa Belarus wanaohusika na kile kinachoendelea kwenye nchi hiyo,'' alisema Borell.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep BorrellPicha: David Dee Delgado/REUTERS

Hatua hiyo inamaanisha kuwa vikwazo hivyo vitajumuisha safari za ndege na mawakala wa usafiri wanaodaiwa kuhusika katika mzozo wa wahamiaji kwenye mpaka wa Belarus na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya za Poland, Latvia na Lithuania. Umoja wa Ulaya umesema sasa utaweza kuwalenga watu binafsi na kampuni zinazoandaa au kuchangia kwenye shughuli zinazofanywa na serikali ya Lukashenko ambazo zinawawezesha wahamiaji kuvuka kinyume cha sheria mipaka ya nchi za Umoja wa Ulaya. Majina ya watu walioathirika na vikwazo hivyo yatatangazwa katika siku zijazo.

Siku zijazo za maamuzi

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen amesema vikwazo vya umoja huo vitahusisha hatua za kuchukua dhidi ya mashirika ya ndege. Von der Leyen amewaambia waandishi habari mjini Munich kwamba siku zinazokuja zitakuwa za kufanya maamuzi. Amesema pia Rais wa Urusi, Vladmir Putin ana ushawishi kuhusu Belarus na anahitaji kuutumia ushawishi wake.

Wakati huo huo, Lithuania, Latvia na Estonia zimesema Jumatatu kuwa Belarus inawalazimisha wahamiaji kuvunja sheria za mipaka ya Umoja wa Ulaya na serikali ya Rais Lukashenko inapaswa kuwajibishwa kwa usafirishaji haramu wa binaadamu.

Taarifa ya pamoja ya mataifa hayo matatu ya Baltic imeeleza kuwa yanalaani hatua zinazochukuliwa na utawala wa Lukashenko kuwatumia wahamiaji kwa madhumuni ya kisiasa. Taarifa hiyo wameitoa baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Poland, Andrzej Duda kwa njia ya video.

(DPA, AP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW