1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yauvalia njuga uraibu wa dawa za kuongeza ufanisi

Daniel Gakuba
10 Julai 2019

Uokozi wa wahamiaji wazamao baharini, kitisho cha chama cha Mbadala kwa Ujerumani kwa utawala wa sheria na kuongezeka kwa uraibu wa dawa za kuongeza ufanisi, ni mada kuu katika magazeti ya Ujerumani leo (10.07.2019).

Russland Moskau Dopingkontrollen
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Zemlianichenko

Operesheni kubwa iliyofanyika kote barani Ulaya, ambamo tani za madawa haramu ya kuongeza ufanisi wa mwili zilinaswa, na kuwakamata wachuuzi 234 juzi Jumatatu, zimeangaziwa na baadhi ya magazeti.

Aachener Nachrichten linasema tatizo la uraibu limekuwa kubwa mno, na kwa hivyo, mahitaji ya dawa hizo yanapanda sambamba na wingi wa watumiaji. Linasema hivi sasa sio tu wachezaji na wanariadha wanaotaka kutunisha misuli yao na kuiongezea nguvu, bali pia katika maisha ya kawaida watu wanazidi kutafuta urembo wa bandia, kuongeza nguvu zao za kiume na kadhalika.

Suluhisho, anasema mhariri wa gazeti hilo, ni kubadilisha mawazo ya watu, kwa kuwapatia elimu tangu utotoni, ili waelewe ubaya wa madawa hayo katika maisha yao ya baadaye.

Mvutano juu ya uokoaji wa watu baharini

Kuhusu operesheni za uokozi wa baharini, gazeti la Mittelbayerische Zeitung linagusia kuimarika kisiasa kwa waziri wa mambo ya ndani wa Italia Matteo Salvini, kunakotokana na msimamo wake mkali dhidi ya wahamiaji.

Linasema kiongozi huyo ambaye pia ni naibu waziri mkuu, amenufaika kutokana na hofu ya Wataliano kuhusiana na kuongezeka kwa wahamiaji mnamo miaka ya hivi karibuni. Mhariri wa gazeti hilo anasema Salvini anapata umaarufu huo, kwa sababu raia wa Italia wakijitazama, wanajiona katika taswira isiyo sahihi.

Kuhusu mada hiyo hiyo, mhariri wa gazeti la Südwest Presse anashangaa kwamba ingawa meli za uokozi wa wahamiaji katika bahari nzima ya Mediterania hazifiki hata sita, lakini bado suala hilo limegeuzwa kuwa la kisiasa barani Ulaya.

Anaandika kuwa hali hii inatokana na kujidanganya kwa wanasiasa wa Ulaya, kwamba wanaweza kupata muafaka na serikali zinazoongozwa na vyama vya siasa kali za kizalendo juu ya hatua za kuchukua. Gazeti hilo linashauri kwamba Ulaya inabidi itambue ukweli, kwamba haihitaji ridhaa ya kila mmoja, kuanza kusimamia tena tena uokozi wa wakimbizi baharini, kwa sababu haiwezi kuwaacha wote waangamie.

Berliner Morgenpost ni gazeti jingine lililolitazama tatizo hilo, likitoa mfano wa kitongoji cha Marzahn-Hellersdorf cha mjini Berlin, ambako uraibu wa dawa za kuongeza furaha umefika katika kiwango cha kutisha miongoni mwa watoto wa kati ya miaka 11 na 14. Linasema dawa zinazowalenga wateja watoto zinauzwa katika rangi za kuwavutia, zikipatikana kwa bei ndogo ya kuanzia yuro 1.50.

Uongozi wa kitongoji hicho umeingilia kati, na kuwatumia ujumbe wazazi kuwaonya watoto wao juu ya madhara ya muda mrefu kwa watumiaji wa madawa ya aina hiyo.

AfD kitisho kwa utawala wa sheria, au mhanga wa njama?

Magazeti mengine yamejishughulisha na kitisho kilichotolewa na wafuasi wa chama cha Mbadala kwa Ujerumani, AfD kwa tume ya uchaguzi katika jimbo la Saxony lililoko Mashariki mwa Ujerumani. Kitisho hicho kilitolewa baada ya theluthi mbili ya wagombea wake katika uchaguzi wa bunge la jimbo, kuenguliwa, kwa hoha ya kutokidhi masharti.

Kölner Stadt-Anzeiger linasema vitisho vya chama hicho kinachofuata sera za mrengo mkali wa kulia, ni ushahidi tosha kwamba hakiheshimu utawala wa sheria. Mhariri wake anasema wanachama wachache wenye busara ndani ya chama hicho, wametambua kuwa makosa yalifanyika ndani ya chama, lakini wengine bado wanashikilia kuwa kilichofanyika ni hila ya vyama vikongwe dhidi ya chama hao.

Gazeti la Mitteldeutsche Zeitung pia linaujadili kasa huo ambao umewalazimu polisi kuipatia ulinzi mikutano ya tume ya uchaguzi katika jimbo hilo. Linasema chama cha AfD kilikiuka utaratibu sahihi wa kikatiba, wa kuwasajili wagombea wake, lakini anaongeza kuwa suala la uwajibikaji, ni kazi isiyowezekana kwa chama hicho.

 

dpae, inlandspresse

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW