Ulaya yawasilisha mapendekezo kuepusha mzozo mpya wa Brexit
14 Oktoba 2021Umoja wa Ulaya umetoa mapendekezo ya kulegeza ugumu wa ukaguzi wa forodha na usajili wa bidhaa zinazotarajiwa kuingizwa Ireland Kaskazini kutoka nchini Uingereza, huku ukiwa na matumaini kwamba hatua hiyo itasaidia kuepusha mzozo mpya unaohusiana na hatua ya Brexit.
Umoja wa Ulaya umewasilisha mapendekezo hayo ikiwa ni jaribio la kutatua changamoto zilizopo katika mpangilio wa kibiashara wa baada ya Brexit huko Ireland Kaskazini, ambazo London inasema zinachochea hali ya wasiwasi miongoni mwa jamii.
Wajumbe wa majadiliano hayo siku ya Jumatano waliwasilisha mpango huo kwa serikali ya Uingereza ikiwa ni siku moja baada ya waziri wa Brexit wa Uingereza David Frost kusema makubaliano yaliyopo yanayojulikana kama itifaki ya Ireland Kaskazini yanatakiwa kufanyiwa kazi upya.
Kwenye mpango huo bidhaa nyingi za vyakula hazitatakiwa kukaguliwa zinapoingizwa Ireland Kaskazini kutokea Uingereza.
Makamu wa rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya na mjumbe wa Brexit Maros Sefcovic amesema amekuwa akisikiliza na kujadiliana na wadau wa Ireland Kaskazini na hatimaye kuja na mapendekezo hayo mapya yanayoweza kutoa majibu ya maswali yaliyopo.
Amesema, " Na kwa hakika, tumezibadilisha sheria zetu kabisa na kutafuta suluhisho kamili za changamoto iliyopo. Hiyo inajumuisha Umoja wa Ulaya kubadilisha sheria zake katika masuala ya dawa."
Soma Zaidi: Maoni: Licha ya kufikiwa makubaliano, Brexit bado ni hadaa
Amesema wanatarajia kuwa na mazungumzo ya ukweli na ya kina na serikali ya Uingereza, kwa maslahi ya jamii za Ireland Kaskazini.
Ingawa Umoja wa Ulaya unakataa kukubaliana upya itifaki hiyo, taarifa yake imesema mipango ya sasa ni tofauti kwa kuangazia utekelezaji wake na itapunguza changamoto za kibiashara "kwa kiwango kikubwa".
Uingereza imesema itayaangalia mapendekezo hayo kwa umakini mkubwa na kutoa mwito wa pande hizo mbili kuanza mazungumzo ya kina mara moja. Msemaji wa serikali amesema wanatakiwa kuangazia suluhu itakayozipeleka mbele pande zote mbili.
Huku hayo yakiendelea, mkuu wa chama cha Demoratic Unionist, DUP cha Ireland Kaskazini Jeffrey Donaldson amesema hiyo ni hatua ya awali ambayo hata hivyo imekosa mabadiliko muhimu yaliyohitajika.
Donaldson amesema chama chake kitayasoma kwa kina mapendekezo hayo, ingawa amerudia msimamo wa chama kwamba itifaki za Ireland Kaskazini zinawaathiri kikatiba na kiuchumi.
Soma Zaidi: Von der Leyen: Mianya mikubwa ingalipo kuhusu Brexit
Chini ya itifaki hiyo, Ireland Kaskazini inaendelea kufuata sheria za soko la pamoja na forodha za Umoja wa Ulaya, na hivyo kuzuia ukaguzi wa mpakani kati ya jimbo hilo la Uingereza na Jamhuri ya Ireland, ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya.
Kundi linaloshughulikia changamoto za kibiashara zinazohusiana na Brexit upande wa Ireland Kaskazini limeikaribisha hatua hiyo, ambayo limekuwa likisema ni ya muhimu iwapo pande zote mbili zitakuwa na nia ya kupata suluhu ya kudumu.
Kundi hilo limesema kuna mengi ya kupendekeza katika mpango huo wa Umoja wa Ulaya na kuongeza kuwa watayasoma mapendekezo hayo na kuwasiliana na wanachama wake kabla ya kutoa mtizamo wao wa mwisho.
Mashirika: APE/RTRE