1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uli Hoeness apata zawadi ya mwaka mpya

2 Januari 2015

Aliyekuwa rais wa Bayern Munich Uli Hoeness amepewa kibali cha kumruhusu kuondoka jela saa za mchana wakati akiendelea kutumikia kifungo cha kupatikana na hatia ya kukwepa kulipa kodi

Uli Hoeneß ARCHIV Mai 2014
Picha: picture-alliance/dpa/Rene Ruprecht

Chini ya masharti ya kuwachiwa kwake, Hoeness ataruhusiwa kufanya kazi saa za mchana kabla ya kurejea gerezani saa za jioni. Anatarajiwa kufanya kazi katika timu ya vijana ya mabingwa hao wa Bundesliga Bayern.

Hoeness ambaye Jumatatu ijayo atafikisha umri wa miaka 63, alianza kifungo chake cha miaka mitatu na nusu jela karibu miezi mitatu iliyopita baada ya kuhukumiwa na mahakama moja ya Munich mwezi Machi kwa kukwepa kulipa kodi ya kiasi cha euro milioni 28.5

Dutt aondoka Bremen

Kwingineko katika Bundesliga, Robin Dutt yuko huru kuchukua wadhifa wa mkurugenzi wa spoti katika klabu ya VfB Stuttgart baada ya Werder Bremen kukubali kusitisha mkataba wake.

Dutt alipigwa kalamu na Bremen mwishoni mwa mwezi Oktoba lakini alikuwa chini ya mkataba na klabu hiyo hadi Juni 30, 2016. Na sasa Dutt mwenye umri wa miaka 49 amefikia makubaliano na mahasimu wa Bremen katika Bundesliga, Stuttgart kuchukua wadhifa wa mkurugenzi wa spoti.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Gakuba Daniel