1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu wamlilia nguli wa soka Franz Beckenbauer

Sylvia Mwehozi
9 Januari 2024

Wapenzi na mashabiki wa soka ulimwenguni kote wanaomboleza kifo cha nguli wa soka wa Ujerumani, Franz Beckenbauer, aliyeshinda kombe la dunia kama nahodha na kocha, anachukuliwa kuwa mchezaji mashuhuri wa soka duniani.

Franz Beckenbauer | 1974
Nguli wa soka wa Ujeumani Franz Beckenbauer kombe la dunia 1974Picha: Roland Witschel/dpa/picture alliance

Akijulikana kwa majina ya utani ya "Der Kaiser" yani Mfalme na "Die Lichtgestalt" yani nuru inayong'aa, Beckenbauer alitamba katika miaka ya 60 na 70 kwa aina yake ya uchezaji na uongozi. Mbali ya kupata mafanikio makubwa katika timu ya taifa, nguli huyo wa soka alijizolea heshima lukuki zisizohesabika wakati alipokuwa na klabu yake ya muda mrefu ya Bayern Munich, ikiwemo ushindi wa mataji matatu mfululizo ya kombe la Ulaya na kombe la mabara.

Franz Beckenbauer akiwa amenyanyua kombe la dunia mwaka 1974Picha: imago/WEREK

Kupitia ujumbe aliouchapisha katika ukurasa wake wa Instagram, Rais wa shirikisho la soka ulimwenguni FIFA Gianni Infantino amemtaja Beckenbauer kuwa "nguli wa soka wa Ujerumani na ulimwengu". Naye rais wa shirikisho la soka la Ulaya UEFA, Aleksander Ceferin, amesema kuwa "urithi wa Beckenbauer kama mmoja wa magwiji wa soka wa wakati wote hauwezi kupingwa."

Rais wa shirikisho la soka la Ujerumani DFB Bernd Neuendorf amesema "Franz Beckenbauer anaacha nyuma urithi mkubwa kwa shirikisho hilo na soka kwa ujumla."

Klabu ya Bayern Munich imeelezea kusikitishwa na kifo cha mchezaji huyo ikisema kuwa ulimwengu wao umekuwa "mweusi na wa kimya" na kuongeza kuwa bila ya upekee wa Der Kaiser klabu ya Bayern isingefikia mafanikio iliyo nayo sasa.

Soma pia: Beckenbauer: Mechi ya Bayern na Dortmund itaamua ubingwa

Salaam nyingine za rambirambi zimetolewa na Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier aliyesema kuwa wamepoteza mwakilishi mashuhuri na maarufu katika soka la Ujerumani. Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani kupitia ukurasa wa X, amemtaja Beckenbauer kuwa "alikuwa mmoja wa magwiji wa soka Ujerumani na kwa watu wengi Mfalme huyo wa soka alikuwa chachu ya soka la Ujerumani kwa vizazi".

Franz Beckenbauer akiwa na klabu ya Bayern Munich katika BundesligaPicha: Werek/dpa/picture alliance

Karl-Heinz Rummenigge, mchezaji wa zamani wa Bayern Munich na Mkurugenzi amemwelezea Beckenbauer kuwa; "Alikuwa mchezaji wa kipekee. Alikuwa na umaridadi, hakuwa Mjerumani kwa kawaida. Alikuwa Mbrazil zaidi katika suala la kudhibiti mpira. Ilikuwa ni kiwango cha juu katika ubora aliokuwa nao."

Kati ya mwaka 1965 na 1977, Beckenbauer aliichezea timu ya taifa ya Ujerumani Magharibi mechi 103 na kufanikiwa kufunga jumla ya mabao 14.

Soma kuhusu: Franz Beckenbauer matatani

Akichukuliwa kuwa mmojawapo ya wachezaji bora wa wakati wote, Beckenbauer alishinda Kombe la Dunia kama mchezaji mwaka 1974 na tena kama kocha mwaka 1990, ikiwa ni miongoni mwa watu watatu tu kufikia mafanikio hayo.

Beckenbauer alicheza kando ya gwiji wa Brazil Pele katika klabu ya New York Cosmos, kisha akarejea Ujerumani Magharibi katika klabu ya SV Hamburg kabla ya kustaafu soka.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW