1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu waadhimisha siku ya kimataifa ya lugha ya ishara

22 Septemba 2023

Kila inapofika Septemba 23 kila mwaka ulimwengu unaadhimisha siku ya kimataifa ya lugha ya ishara. Watu wenye ulemavu wa kutosikia au kusikia kwa shida wangali wanapata changamoto katika nchi nyingi barani Afrika.

Juba
Mwalimu akiwafundisha wanafunzi wasiosikia kutumia Lugha ya ishara JubaPicha: Light for the World

Baraza kuu la Umoja la Umoja wa Mataifa mnamo 2017 liliitangaza Septemba 23 kama siku ya kimataifa ya lugha ya ishara ili kuangazia haki za binadamu za watu wenye ulemavu wa kutokusikia na wanaosikia kwa taabu. Lugha za ishara zimetafsiriwa katika mtazamo wa kiisimu kama lugha, na wale wanaotumia lugha ya ishara wameelezwa kama kundi la wachache kiisimu, kwa mujibu wa Shirika la kimataifa la watu wenye ulemavu wa kutokusikia, WFO.

Soma pia: Wakalimani, wabebaji ujumbe mbalimbali

Hata hivyo kuWakalimani, wabebaji ujumbe mbalimbalipata haki zao kuheshimiwa au kutambuliwa inabaki kuwa changamoto kwa watu wengi ambao ni viziwi na wenye changamoto ya kusikia kote ulimwenguni, ikiwemo barani Afrika. Na lugha mbalimbali za ishara barani Afrika zinaongezea changamoto zilizopo.

Ambrose Murangira, ambaye huwasiliana kwa lugha ya ishara ambayo ni maalumu sana nchini Uganda, ameelezea kwa nini kila nchi ina lugha yake ya ishara. Ameiambia DW kupitia mkalimani wa lugha kwamba tofauti inatokana na mienendo ya tamaduni na tamaduni tofauti tofauti zina njia mbalimbali za kuishi.

"Lugha ya ishara ni mojawapo ya lugha za kitaifa kwa mujibu wa katiba ya Uganda. Kwa hivyo imekubaliwa mashuleni, hata mahakama ya juu, na katika bunge la Uganda. Kwa hiyo barani Afrika, serikali zinatumia fedha nyingi katika usalama kulipia helikopta na bunduki. Kwa kuzingatia sera na utunzi wa sheria sisi ni wazuri kwa sababu tuna sheria nyingi na Uganda inaongoza mbele ya nchi nyingine. Lakini linapokuja suala la utekelezaji, nahisi nchi nyingine zinafanya vyema zaidi. "

Mwanafunzi akisoma Quran kwa kutumia lugha ya isharaPicha: Juni Kriswanto/AFP/Getty Images

Murangira amesema wanapambana kupata huduma za afya Uganda, kupata ajira na pia kama mtu anataka kuanzisha familia ni changamoto.

Kuna watu zaidi ya milioni 70 wenye ulemavu wa kutokusikia kote ulimwenguni, zaidi ya asilimia 80 kati yao wanaishi aktika nchi zinazoendelea kwa mujibu wa shirika la kimatiafa la viziwi. Kwa ujumla wanatumia zaidi ya lugha 300 tofauti tofauti za ishara.

Murangira anasema suala lengine linalowakabili watu wengi wanaopata shida kuwasiliana ni mtazamo kutoka kwa watu wengine. Kwa mfano, watu wengi wanaotumia lugha ya ishara mara nyingi hupuuzwa, hususan katika sekta ya afya.

Afrika Kusini ilitambua lugha ya ishara kama lugha yake ya 12 rasmi mnamo mwezi Julai na hivyo kuwa nchi ya nne ya Afrika kufanya hivyo baada ya Kenya, Uganda na Zimbabwe. Kuna nchi angalau 41 ambazo sasa zinatambua lugha ya ishara kama lugha rasmi.

Unajua kutumia lugha ya ishara?

04:32

This browser does not support the video element.

Afrika Kusini ina mfumo wa elimu ulioimarika kwa watu viziwi na wenye matatizo ya kusikia. Licha ya kuwa na shule zaidi ya 40 za viziwi Afrika Kusini, bado kuna fursa kubwa ya kufanya vyema zaidi kwa mujibu wa Claudine Storbeck, Mkurugenzi wa kitivo cha mafunzo kuhusu viziwi katika chuo kikuu cha Wits mjini Johannesburg. Storbeck ameiambia DW kwamba ilichukua miaka 25 kwa lugha ya ishara kufanywa kuwa lugha rasmi Afrika Kusini, lakini watoto bado hukamilisha masomo yao wakiwa hawajui kusoma wala kuandika kwa sababu waalimu wao hawawezi kuwasiliana nao.

Nchini Sudan Kusini kabla kuanza kwa lugha ya ishara ya nchi hiyo, watu walitumia mchanganyiko wa lugha asili, mbali na lugha za ishara za Kenya, Uganda na kiarabu. Sophia Mohammed, mkurugenzi wa kitaifa wa shirika la Light for the World katika mji mkuu, Juba anasema ni vigumu kutoa mchango chanya kutokana na vita ambavyo vimekuwa vikiendelea Sudan Kusini.

"Hali ya watu wenye ulemavu bila shaka ni ya changamoto kwa sababu nchi imekuwa vitani kwa miaka 25 au 26. Kwa hiyo huduma hazipatikani na uhamasishaji kuhusu kuwajumuisha watu wenye ulemavu pia haujatangazwa sana bado ni mada mpya Sudan Kusini. Hasa akina mama na watoto wadogo ndio wanaotengwa zaidi na kufichwa katika jamii kutokana na unyanyapaa na ubaguzi."

Kurasa ya kutoka kamusi ya lugha ya ishara ya Sudan KusiniPicha: Light for the World

Nchini Nigeria watu viziwi wa jamii ya Hausa wanatumia "maganar hannu", lugha ya ishara ambayo imefanyiwa utafiti vizuri sana na kuandikwa na inatumika katika majimbo ya kaskazini, kwa mujibu wa Constanze Halima Schmaling, mwanaisimu wa lugha ya ishara katika chuo kikuu cha Ludwig Maximillian mjini Munich, kusini mwa Ujerumani.

"Nigeria ni nchi yenye lugha 500 zinazozungumzwa. Haijabainika wazi kama kuna lugha moja ya ishara ya Nigeria au zipo tofauti tofauti. Kuna utafiti mchache sana kuhusu hili."

Schmaling amesema vyuo kote Nigeria hupendelea kufunza lugha ya ishara ya Marekani, hali ambayo husababisha mchanganyiko wa lugha na tofauti baina ya lugha za ishara za Kihausa kati ya wazee na vijana au kati ya wale ambao waliwahi kwenda shule au waliofanikiwa tu kuhuduria madarasa ya kujifunza kusoma na kuandika kwa ajili ya watu viziwi.

Kwa taifa kubwa lenye tamaduni na lugha mbali mbali kama Nigeria, kuwa na lugha moja ya ishara itakuwa kazi kubwa na ambayo kwa bahati mbaya si miongoni mwa vipaumbele vyake vikubwa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW