Ulimwengu wakumbuka mauaji ya Holocaust miaka 81 baadaye
27 Januari 2026
Kulingana na baadhi ya wanasiasa, kumbukumbu ya mwaka huu inajiri mnamo wakati kuna ongezeko la chuki ulimwenguni, kitisho kinachopaswa kutokomezwa kabisa.
Kuanzia Ujerumani, Uholanzi, Ubelgiji, Jamhuri ya Czech na kwingineko duniani, wengi walijitokeza katika miji mbalimbali wakiwemo manusura wa maangamizi hayo, wanasiasa, na watu wa kawaida, kuyakumbuka maangamizi hayo yaliyoacha ulimwengu ukiwa umeduwaa kwa mshtuko na huzuni miaka 81 iliyopita.
Mjini Berlin, mishumaa iliwashwa alfajiri katika makumbusho ya mji huo, maua meupe ya waridi pia yaliwekwa kwenye makumbusho hayo, huku watu wakitafakari mauaji ya mamilioni yaliyofanywa na utawala wa Manazi wa Ujerumani katika lililokuwa jaribio lake la kuangamiza kabisa Wayahudi barani Ulaya chini ya Adolf Hitler. Takwimu zinasema, Wayahudi milioni sita waliuawa katika mauaji hayo ya Holocaust, na kwa Ujerumani hilo limesalia kuwa majuto makubwa.
Manusura wasema walinyang'anywa ubinadamu wao
Mjini London Uingereza, Mala Tribich, mmoja wa manusura wa maangamizi hayo alifika mbele ya baraza la serikali ya Uingereza na kusimulia madhila mazito yaliyoacha makovu yasiyofutika akilini na maishani mwake:
"Katika kambi tulivuliwa nguo tukawa uchi wa mnyama, tukanyolewa nywele, tukalazimishwa kuoga kwa maji baridi shadidi na hata tukapewa kazi ya wafungwa. … Hawakutunyang'anya tu uhuru wetu, bali pia utambulisho wetu, heshima yetu, na ubinadamu wetu. … Ilikuwa kuzimu au akhera duniani," amesema Tribich.
Katika eneo la kumbukumbu la Auschwitz, lililoko kusini mwa Poland iliyokuwa chini ya utawala wa Kijerumani wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, wafungwa wa zamani waliweka mashada ya maua mahali ambapo majeshi ya Kijerumani yaliwaua maelfu ya watu, wengi wao Wapoland.
Petr Pavel: Kumbukumbu ya Holocaust ni wito wa kuyatafakari yaliyopita
Katika Jamhuri ya Czech, maandamano ya watu watakaokuwa na mishumaa inayowaka, yamepangwa kufanyika jioni huko Terezin, katika eneo la kambi ya zamani ya mateso ya Wanazi ya Theresien. Maelfu ya Wayahudi walikufa huko au walitolewa huko na kupelekwa hadi Auschwitz na kambi nyinginezo ili kuuawa.
Rais wa Jamhuri ya Czech Petr Pavel, amesema siku ya kimataifa ya kumbukumbu ya Holocaust ni "wito wa kuyatafakari yaliyopita na wajibu wetu kama jamii, hasa katika ulimwengu wa sasa. Kwa bahati mbaya, hata leo kuna watu wanaopuuza itikadi za Manazi Mamboleo yenye chuki, au wengine hata huishangilia".
Mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, ameonya kwamba dunia kwa sasa inashuhudia viwango vya juu vya chuki dhidi ya Wayahuditangu Mauaji ya Kimbari ya Wayahudi na kwamba baadhi ya vitisho sasa vinatia wasiwasi.
Kallas, ambaye ni mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, amesisitiza matumizi mabaya "ya maudhui yaliyotengenezwa kutumia akili mnemba kupotosha ukweli wa kihistoria, na kudhoofisha kile alichokitaja kuwa kumbukumbu yetu ya pamoja.
Inakadiriwa kuwa wapo takriban waathiriwa 196,600 wa Kiyahudi wa Mauaji ya Kimbari ambao bado wako hai duniani kote. Idadi hiyo imepungua kutoka kwa waathirika 220,000 waliokadiriwa kuwa hai mwaka uliopita.
(APAE)