1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu walaani mapinduzi ya kijeshi Guinea

6 Septemba 2021

Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya ECOWAS, Marekani na Ufaransa zimeshutumu na kulaani vikali mapinduzi ya kijeshi nchini Guinea na kutaka Rais Conde kuachiliwa huru mara moja. 

Videostill | Guinea Conakry - Militärputsch: Doumbouya hält Ansprache
Picha: AFP

Kufuatia tukio la kitengo maalum cha jeshi la Guinea kutangaza kuupindua utawala wa Rais Alpha Conde na kumshikilia rais huyo, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Marekani, Ufaransa na jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za magharibi mwa Afrika (ECOWAS) zimeshutumu vikali mapinduzi hayo na kutaka Rais Conde aachiliwe huru mara moja. 

Taarifa kutoka kwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi pamoja na mkuu wa kamisheni ya umoja huo Moussa Faki Mahamat, imelitaka Baraza la Usalama nchini Guinea kufanya kikao cha dharura ili kutathmini hali ilivyo na lichukue hatua muafaka.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia ameshutumu vikali hatua hiyo ya jeshi kuchukua madaraka kwa nguvu. Kupitia ukurasa wa Twitter, Guterres ametaka Rais Conde kuachiliwa huru mara moja.

Mnamo Jumapili, milio ya risasi ilisikika karibu na Ikulu Conakry.

Vikosi maalum vya jeshi nchini humo vilidai kuupindua utawala wa Rais Alpha Conde ambaye ametawala nchi hiyo kwa muda mrefu. Na kwamba wanamshikilia rais huyo.

Hatima ya Rais Conde wala aliko haijulikani?

Wakuu wa mapinduzi hayo wametangaza marufuku ya kuwa nje nchini kote hadi watakapotoa maelezo zaidi. Wamesema pia kwamba nafasi za magavana sasa zimechukuliwa na wanajeshi. Kwenye hotuba yao, wamesema Conde yuko salama na hajajeruhiwa.  

Vidio ambayo haijathibitishwa ambayo inasambaa kwenye mitandao ya kijamii inamuonesha Rais Conde akiwa amekamatwa na kikosi maalum cha jeshi.Picha: AFP

"Tumeamua kuivunja katiba. Tutavunja pia taasisi. Serikali yetu imevunjwa. Tutafunga mipaka yetu ya ardhini kwa wiki nyingine kisha tutaona cha kufanya na mipaka yetu ya angani. Pamoja na wenzetu wote, tutapata suluhisho la kutuondoa kwenye machafuko haya," amesema mkuu wa vikosi hivyo maalum Luteni Kanali Doumbouya.

Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS pia imeshutumu tukio hilo na imetaka utawala wa sheria na demokrasia urejeshwe nchini Guinea. Jumuiya hiyo imetishia kuwekea Guinea na viongozi hao wa kijeshi vikwazo.

ECOWAS yatishia kuwekea Guinea vikwazo

Kupitia taarifa, mwenyekiti wa ECOWAS ambaye pia ni rais wa Ghana Nana Akuffo-Addo ameshutumu kile alichokitaja kuwa jaribio la mapinduzi. Ametaka Rais Conde kuachiliwa huru bila masharti yoyote.

Marekani na Ufaransa pia zimeshutumu mapinduzi hayo na kutoa wito wa kurejeshwa kwa utawala wa kikatiba.

Hali ni ya wasiwasi mjini Conakry baada ya jeshi kutangaza mapinduzi, lakini baadhi ya raia wamejitokeza mitaani kushangilia hatua hiyo.Picha: Cellou Binani/AFP/Getty Images

Kwenye taarifa iliyotangazwa katika kituo cha televisheni kinachomilikiwa na serikali, kitengo hicho maalum cha jeshi kimesema kitaandaa kikao cha mawaziri pamoja na wakuu wengine wa serikali Jumatatu asubuhi mjini Conakry. Mawaziri wote wametakiwa kuhudhuria. Wametahadharisha kuwa kutohudhuria kutachukuliwa kama uasi.

Mapinduzi hayo yanajiri baada ya kipindi kirefu cha mvutano wa kisiasa nchini Guinea. Mgogoro huo ulichochewa mwanzo na upinzani mkali dhidi ya hatua ya Rais Conde kuwania muhula wa tatu wa urais mwaka uliopita.

Tangu wakati huo, Conde amekuwa akikabiliwa na ukosoaji mkubwa na hata kusababisha maandamano mitaani.

Hali bado ni tete nchini humo. Haijabainika ikiwa wanajeshi ambao ni wapambe wa Conde watajitokeza kukabiliana na walioongoza mapinduzi dhidi yake au la.

Alpha Conde aliingia madarakani mwaka 2010 katika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia nchini humo tangu ilipojipatia Uhuru kutoka kwa wafaransa mnamo mwaka 1958.

(RTRE, AFPE, APAE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW