1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiBrazil

Ulimwengu wamuaga mwanasoka maarufu Pele

2 Januari 2023

Brazil imegubikwa na huzuni wakati shughuli za kutoa heshima za mwisho kwa nguli wa kandanda Pele zikiendelea. Mwili wa Pele tayari umewasili katika uwanja wa Santos kwa ajili ya kuagwa.

Brasilien Pele wurde im Stadion von Sao Paulo aufgebahrt
Jeneza la PelePicha: Matias Delacroix/AP Photo/picture alliance

Msafara wa magari ukiwa umebeba jeneza la mchezaji huyo wa zamani maarufu uliwasili Estádio Urbano Caldeira katika wilaya ya Vila Belmiro mapema leo ambako mamia ya mashabiki walikuwa tayari wakisubiri katika uwanja huo wakiwa na bendera zao ili kumuaga yule aliyepewa jina "O Rei" yaani Mfalme.

Msafara huo uliosindikizwa na polisi na vikosi vya zima moto uliondoka mapema kutoka hospitali ya Albert Einstein huko São Paulo, umbali wa karibu kilomita 80, ambako Pele mwenye umri wa miaka 82 alifariki siku ya Alhamisi  baada ya kuugua kwa muda mrefu.

PelePicha: Payel Samanta/DW

Jeneza la mshindi huyo mara tatu wa Kombe la Dunia limewekwa katikati mwa uwanja wa Santos, klabu ambayo Pele aliichezea kwa muda mrefu. Mashabiki watatoa heshima zao za mwisho kwa Pele huku wakitakiwa kuwa na umbali wa takriban mita tano na jeneza la mwanasoka huyo.

Soma zaidi:Nguli wa Brazil Pele aaga dunia 

Mji wa pwani wa Santos wenye watu wapatao 430,000 umejiandaa kwa shughuli za mazishi ya mchezaji huyo aliyetia fora ulimwenguni na kuitangaza vyema Brazil kimataifa.

Mamlaka za mji wa Santos zilisema waandishi wa habari takriban 5,000 kutoka kote ulimwenguni wameidhinishwa kuripoti mazishi ya mchezaji pekee aliyeifungia Santos zaidi ya mabao 1,000.

Rais wa sasa wa Brazil Luiz Inacio Lula da SilvaPicha: Jacqueline Lisboa/REUTERS

Rais mpya wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva anatarajiwa pia kuhudhuria shughuli hiyo ya kuuaga mwili wa Pele ambayo imepangwa kudumu kwa saa 24. Rais wa FIFA Gianni Infantino na Alejandro Dominguez, mkuu wa shirikisho la kandanda la Amerika Kusini CONMEBOL, walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kutoa heshima zao kwenye jeneza lililokuwa limezungukwa na mashada ya maua meupe.

Soma zaidi: Ulimwengu waomboleza kifo cha Pele

Shabiki wa Pele eneo hilo Roberto Santos amesema matarajio ni makubwa, dunia nzima itakuwa hapo, Pele hahitaji utambulisho na kwamba Pele kwao ni kila kitu. Shabiki mwengine Roberto Dos Santos amesema:

"Inasikitisha sana. Ni wakati mgumu mno. Jina langu ni Dos Santos. Mimi si mtu mwenye uzoefu wa mambo ya ulimwengu, lakini dunia inalijua jina hili - Santos - na liko hapa sasa, tunaishi kupitia hili. Ninawakilisha kupitia jina langu taasisi hii kubwa. Edson Arantes do Nascimento alikuwa muhimu kwa sayari na muhimu kwa soka."

Mada inayohusiana: 

Edson Arantes do Nascimento ndilo jina alilopewa Pele alipozaliwa mwaka 1940 katika mji mdogo wa Tres Coracoes, lakini alihamia Santos mwaka wa 1956 na aliishi huko kwa muda mrefu wa maisha yake.

Siku ya Jumanne, kabla ya mazishi, msafara huo utapita jirani na sehemu anakoishi mama mzazi wa Pele mwenye umri wa miaka 100 na kisha mwili wa Pele utapelekwa kuhifadhiwa katika Mnara wa makaburi ya Necrópole Ecumênica.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW