1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu washtushwa na mauaji nchini Myanmar

Josephat Charo
16 Machi 2021

Jumuiya ya kimataifa imetoa wito wa utulivu na kujizuia baada ya waandamanaji wapatao 20 kuuliwa Jumatatu (15.03.2021) katika maandamano ya kupinga mapinduzi ya kijeshi Myanmar.

TABLEAU | Myanmar Yangon | nach Militärputsch | Protest
Picha: AFP/Getty Images

Shirika linalofuatilia matukio ya mauaji na watu kukamatwa Myanmarlimesema watu wasiopungua 20 waliuwawa siku ya Jumatatu, kufuatia machafuko na maandamano dhidi ya utawala wa kijeshi, wiki sita tangu jeshi lilipotwaa madaraka. Muungano unaowasaidia wafungwa wa kisiasa umesema idadi ya vifo inaongezeka kwa kasi kubwa, ukiongeza kuwa watu zaidi ya 180 wameuliwa tangu mapinduzi ya Februari mosi. Idadi hii ya vifo inatofautian ana ile iliyotolewa na Umoja wa Mataifa ambao umesema waandamanaji wapatao 138 wameuwawa tangu mapinduzi.

Shirika hilo limesema ingawa idadi kubwa ya waliouliwa Jumatatu walikuwa waandamanaji, baadhi wengine walikuwa raia ambao hata hawakuwa wakishiriki maandamano hayo. Wengi waliuawawa katikati mwa Myanmar, huku watatu wakiuliwa katika mji wa Yangon. Vifo vya Yangon vinawajumuisha wanawake wawili katika nyumba zao waliopigwa risasi wakati maafisa wa usalama walipofyetua risasi barabarani. Shirika la habari la AFP limethibitisha vifo 11.

Mtu mmoja aliyeshuhudia kutoka mji wa Aunglan eneo la Magway katikati mwa Myanmar ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wanaume wawili waliuliwa kwa risasi na wengine sita kujeruhiwa, akiongeza kuwa mmoja alipigwa risasi kifuani. Vifo sita pia viliripotiwa jana Jumatatu katika mji wa Myingyan. Kwa mujibu wa mkazi mmoja wa Myingyan, miongoni mwa waliouliwa ni watu watatu akiwemo mwanamke mmoja aliyeuliwa kwa risasi. Wote wawili walioshuhudia na kuzungumza na shirika la habari la AFP hawakutaka kutajwa majina kwa hofu ya kusakwa na kuadhibiwa. Televisheni ya taifa ilithibitisha Jumatatu kwamba afisa mmoja wa polisi alipigwa risasi na kuuwawa katika mji wa Bago, kaskazini mashariki mwa Yangon wakati wa maandamano.

Mazishi kufanyika leo

Familia za waliouwawa zinajiandaa kufanya mazishi leo Jumanne baada ya kukesha wakifanya ibada ya wafu usiku kucha. Mama huyu kwa jina Kyi Kyi Kyi alimpoteza mtoto wake wa kiume. "Ni unyama ulioje waliomfanyia mwanangu. Nataka niwaulize ana kwa ana, kama wana roho. Je, hawana watoto kama mimi? Moyo wangu unauma, moyo wangu unararuka kwa uchungu na huzuni."

Waandamanaji wakishiriki maandamano ya usiku kona ya Hledan mjini YangonPicha: REUTERS

Umoja wa Mataifa, Marakani China na Uingereza zimeyalaani vikali machafuko hayo ya Myanmar. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterresameitaka jumuiya ya kimataifa wakiwemo wadau wa kanda, washirikiane kuonyesha mshikamano na watu wa Myanmar na ari yao ya kupigania demokrasia.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Jalina Porter amewaambia waandishi habari mjini Washington jana Jumatatu kwamba utawala wa kijeshi umetumia risasi kujibu miito ya kutaka kurejeshwa kwa demokrasia. Amesema Marekani inaendelea kutoa wito nchi zote zichukue hatua madhubuti kuyapinga mapinduzi hayo na machafuko yanayoendelea kuchacha.

China imesema inafuatilia kwa karibu hali inavyoendelea Myanmar na ina wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa taasisi zake na wafanyakazi. Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa China Zhao Lijian amesema China ina matumaini Myanmar itachukua hatua kuwalinda Wachina. "China itaendelea kuihimiza Myanmar ichukue hatua madhubuti kukomesha matukio yote ya machafuko, kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wahusika na kuhakikisha usalama wa mali na maisha ya raia wa China."

Wakati huo huo Japan imesema si jambo la kusameheka kwa Myanmar kutumia bunduki dhidi ya waandamanaji wa amani. Waziri kiongozi wa Japan, Kato Katsunobu ameihimiza Myanmar iache mara moja kutumia nguvu za kupitiliza dhidi ya raia.

(afpe,rtre)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW