1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu wataka Mashariki ya Kati isitumbukie vitani

25 Septemba 2024

Viongozi mbali mbali wa dunia wamehutubia mkutano wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa wakiutahadharisha ulimwengu kutokana na kuanza kutanuka kwa vita vya Mashariki ya Kati.

Mkutano wa 79 wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa.
Mkutano wa 79 wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa.Picha: Shannon Stapleton/REUTERS

Mbali na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres, Rais wa Marekani, Joe Biden, na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, takribani viongozi wote ambao wamekuwa wakizungumza tangu kufunguliwa kwa mkutano huu wa 79 waHadhara Kuu ya Umoja wa Mataifasiku ya Jumanne (Septemba 24) wamekuwa wakijielekeza kwenye mzozo huo wa Asia ya Magharibi ama Mashariki ya Kati kwa umaarufu wake.

Rais Luiz Inacio Lula da Silva, ambaye nchi yake huwa ya kwanza kuzungumza kutokana na utamaduni wa muda mrefu wa Umoja wa Mataifa, aliyakosowa mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza na Lebanon, akisma haki ya kujilinda imegeuka kuwa haki ya kisasi ambayo inazuwia "kufikiwa makubaliano ya kuachiliwa mateka na kusitisha mapigano."

Soma zaidi: Guterres, atahadharisha juu ya Lebanon kugeuka Gaza nyingine

Kiongozi wa Qatar, Sheikh Tamin bin Hamad Al-Thani, ambaye nchi yake miongoni mwa waongozaji wa mazungumzo ya kusaka amani, aliishutumu moja kwa moja Israel kwa kuwa kizuizi cha mazungumzo ya kusitisha mapigano kwenye Ukanda wa Gaza, akisema kwamba "hakuna mshirika amani" ndani ya serikali ya Benjamin Netanyahu. 

Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel, alisema ingawa Israel ina haki ya kuwepo na kujilinda lakini sio kwa kusababisha mateso ya jumla jamala kwa raia wanaoishi kwenye maeneo yanayolengwa na jeshi lake. 

Iran yaja juu

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran, ambaye nchi yake inaziunga mkono Hizbullah ndani ya Lebabon na Hamas ndani ya Gaza, alilaani kile alichokiita ugoigoi usio maana na usioingia akilini wa Umoja wa Mataifa kwa Israel. 

Rais Masoud Pezekshian wa Iran akihutubia Hadhara Kuu ya Umoja wa MataifaPicha: Seth Wenig/AP Photo/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Uingereza, David Lamy, alielezea pia wasiwasi wa nchi yake kwa machafuko yanayoendelea nchini Lebanon, ambayo alisema yanaelekea kuwa vita vikubwa kwenye eneo zima la Mashariki ya Kati. 

Tayari Uingereza imetangaza kuwatuma wanajeshi wake kwenye kisiwa cha Cyprus kusaidia operesheni ya kuwaondoa raia wake kutoka Lebanon.

Soma zaidi: Viongozi wa dunia kuhutubia Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa

Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan, alitupilia mbali uvumi kwamba nchi yake iko tayari kuwapokea Wapalestina wanaolazimika kuyakimbia makaazi yao kutokana na mashambulizi ya Israel, akisema kitendo hicho kitakuwa sawa na "uhalifu wa kivita."

Kwa upande wake, Balozi wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa aliuita mkutano huo wa Umoja wa Mataifa kuwa ni kituko cha mwaka cha unafiki, huku akisisitiza kuwa nchi yake haina haja ya kutuma wanajeshi wake wa ardhini kwenye nchi ya kigeni, akimaanisha Lebanon. 

Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka yaPalestinaalikikalia kiti chake kwenye ujumbe wa Palestina, ambacho kwa mara ya kwanza kimewekwa kwenye utaratibu wa alfabeti baada ya ujumbe huo kupandishwa hadhi ndani ya Baraza hilo mwezi Mei. Hotuba yake inatarajiwa kesho, Alkhamis, huku Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akipangiwa kuzungumza keshokutwa, Ijumaa.

Awali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, aliiambia Hadhara hiyo Kuu wakati wa hotuba ya ufunguzi kwamba hali ya uhalifu kutokuchukuliwa hatua, ukosefu wa usawa na ukosefu wa uhakika yanaufanya ulimwengu wa sasa kuelekea kwenye mkwamo mkubwa.

Guterres alisema dunia haiwezi kwenda kama ilivyo sasa, ambapo changamoto za vita vya Mashariki ya Kati, Sudan, Ukraine na maeneo mengine hazipatiwi majibu wala kutatuliwa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW