Ulimwengu watoa wito wa amani
25 Desemba 2014Kwa mara ya kwanza salamu za Krismasi za papa huyo mzaliwa wa Argentina zimetangazwa na kusambazwa moja kwa moja kwa teknolojia ya 3D.
"Je, tunao ushujaa wa kuyapokea kwa moyo mmoja matatizo na magumu ya wale walio karibu yetu, au tunapendelea zaidi masuluhisho ya kibifasi, ambayo hata kama yana ufanisi lakini yamejitenga na wito wa Injili?" Papa aliwauliza waumini 5,000 waliokusanyika kwenye uwanja maarufu wa Mtakatifu Petro, Basilica.
Kiongozi huyo wa waumini bilioni 1.2 wa madhehebu ya Katoliki pia aliwatolea wito wale waliowaita "watu wenye viburi, wanaoringa na wale waliofunga milango yao dhidi ya wengine" kuyapokea maisha kwa "wema na uadilifu."
Katika ujumbe wake wa siku ya Alhamisi (Disemba 25) unaofahamika kama "urbi et orbi" - yaani ujumbe kwa mji na dunia - Papa alizungumzia masaibu ya Wakristo na makundi mengine ya dini za wachache katika eneo la Mashariki ya Kati, hasa wale walio kwenye maeneo yanayoshikiliwa na kundi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS).
Papa Francis alizungumza kabla ya hapo na wakimbizi wa Iraq kwa njia ya simu, akiwafariji kwa masaibu yanayowapata.
Malkia wa Uingereza awasifu madaktari wa Ebola
Papa Francis pia amezungumzia vita nchini Syria, mgogoro baina ya Israel na Palestina, maradhi ya Ebola, ghasia za Waislamu wenye siasa kali kaskazini mwa Nigeria na mzozo wa Ukraine.
Ujumbe wa Malkia Elizabeth II wa Uingereza kwenye sikukuu ya Krismasi ya mwaka huu uliwalenga madaktari na wafanyakazi wa misaada ambao wamejitolea maisha yao kupambana na maradhi thakili ya Ebola.
Malkia huyo alisema kwamba madaktari na wafanyakazi hao ni mashujaa walioshinda hisia za ubinafsi na kujitolea maisha yao kuwaokoa wengine.
Kwenyewe mjini Bethlehem, Ukingo wa Magharibi, mji anaominika kuzaliwa Yesu Kristo, waumini mbalimbali wamehudhuria ibada ya mkesha wa Krismasi kwenye Kanisa la Uokovu, miongoni mwao akiwa Rais Mahamoud Abbas wa Palestina. Kote kulisikikana wito wa kuwepo kwa amani, usawa na kuheshimiana kufuatia ghasia za hivi karibuni kati ya Waisraili na Wapalestina.
Krismasi kwa ajili ya amani
Nchini Ufasansa, kipindi chenye pirika nyingi cha Krismasi kimetandwa na mkururo wa mashambulizi yaliyopelekea kifo cha mtu mmoja na kuwajeruhi wengine 25.
Nchini Marekani, maafisa waliendelea kupigania kudhibiti hali ya mambo baada ya ghadhabu mpya ya umma kuzuka kufuatia kuuawa kwa kijana mwengine mweusi na afisa polisi mzungu katika kitongoji cha Mtakatifu Louis, siku ya Jumanne (Disemba 23).
Huko Australia, viongozi wa makanisa walitumia misa za Krismasi kuakisi misiba ambayo iliikumba nchi hiyo kwenye mwaka 2014, ikiwemo kutekwa kwa mkahawa wa Lindt mjini Sydney, tukio lililomalizika kwa vifo vya watu watatu, akiwemo mtekaji nyara, kuuawa kwa watoto wanane kwenye mji wa Cairns na mkasa wa kuanguka na kupotea kwa ndege za Malaysia MH370 na MH17, ambazo zote mbili zilikuwa na raia wengi wa nchi hiyo.
Nchini Sierra Leone, sherehe zote za Krismasi zilifutwa kutokana na maradhi ya Ebola, huku wanajeshi wakitumwa mitaani kuzuia watu ambao wangelijaribu kukaidi amri hiyo ya serikali.
Nchini China, mji wa mashariki wa Wenzhou ulipiga marufuku sherehe zozote za Krismasi, kwa madai kuwa ni mila za kigeni ambazo zina lengo la kuiharibu jamii ya China. Nchi hiyo ina kiasi cha waumini milioni 60 wa Kikristo.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Sekione Kitojo