Ulimwengu waukaribisha mwaka 2023 kwa sherehe na fashifashi
1 Januari 2023Mwaka mpya ulikaribishwa kwanza kwenye kisiwa kidogo cha Kiribati na kisha kwenye mataifa ya mashariki ya mbali, Asia, Afrika na Ulaya huku mataifa ya bara la Amerika yamekuwa ya mwisho kuuona mwaka mpya saa chache zilizopita.
Kundi la maelfu ya watu walikusanyika kwenye lango mashuhuri la Brandenburg mjini Berlin kwa sherehe za mwaka mpya.
Usiku wa manane ulipotimu, kulifyetuliwa fashifashi kwenye eneo hilo la historia. Maeneo mengi ya mji huo mkuu wa Ujerumani pia yalifanya sherehe mbalimbali za kuukaribisha mwaka.
Saa chache baadaye, mjini New York, sherehe kubwa ya jadi ilifanyika kwenye viunga vya Times Square na kuhudhuriwa na idadi kubwa ya watu. t
Mamia kwa maelfu walishuhudia matukio ya kuhesabu sekunde kabla ya saa sita usiku na kuangushwa kwa puto kubwa.
Sherehe za kuukaribisha mwaka mjini New York ni miongoni mwa zile kubwa kabisa duniani. Historia yake inarudi nyuma hadi mwaka 1904 zilipoanza kwa mara ya kwanza.
Brazil na Uingereza nazo zafanya sherehe za kuukaribisha mwaka
Huko Rio de Janeiro nchini Brazil mji huo ulifanya sherehe kubwa za kuukaribisha mwaka mpya katika fukwe za Copacabana ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuondolewa vizuizi vya kukabiliana na UVIKO-19.
Mamia kwa maelfu ya watu walitizama fashifashi zilizofyetuliwa kutoka kwenye maboya yaliyo baharini huku wanamuziki wakitumbwiza kwenye jukwaa la burudani hapo Copacabana.
Mjini London, zaidi ya watu 100,000 walikusanyika kushuhudia onesho la aina yake la fashifashi kwenye bembea kubwa la duara ambalo ni maarufu kwenye mji huo.
Kwa mara ya kwanza tangu 2019, wageni wameruhusiwa kusherehekea kwenye ukingo wa kusini mwa mto Thames mjini London. Kengele kubwa iitwayo Big Ben iligongwa ilipotimu saa sita usiku kuukaribisha mwaka 2023.
Kwa jumla sherehe za mwaka huu zimerejea katika hali ya kawaida baada ya mataifa mengi kuondoa kabisa vizuizi vya kupambana na janga la virusi vya corona ambavyo kwa miaka miwili vilivyotatiza shamrashamra za kufungua mwaka.
Nchini China taifa ambalo linashuhudia wimbi jipya la maambukizo ya UVIKO-19, maelfu ya watu waliingia mitaani kwa sherehe za mwaka mpya na mamlaka zimewahakikishia kuwa maradhi hayo yatadhibitiwa.
Mwaka mpya waanza kwa furaha na machungu Afrika Mashariki
Sherehe pia zilishuhudiwa pia kwenye mataifa ya Afrika Mashariki. Matamasha yalijumuisha muziki na ufyetuaji fashifashi mjini Dar es Salaam, Nairobi, Kampala na Kigali.
Baada ya kutimia saa sita usiku watu walikumbatiana na kutakiana kheri na fanaka kwa mwaka unaoanza.
Hata hivyo nchini Uganda sherehe za mwaka mpya zimeanza kwa simanzi.
Watu wasiopungua 9 wamepoteza maisha kufuatia mkanyagano uliotokea wakati wa sherehe za kuukaribisha mwaka mpya kwenye mji mkuu Kampala.
Polisi imesema mkanyagano uliotokea dakika chache baada ya ufyetuaji fashifashi za kuukaribisha mwaka kwenye viunga vya mtaa wa maduka na biashara wa Freedom City.
Mbali ya watu tisa waliopoteza maisha, wengine 5 wamejeruhiwa na walipelekwa hospitali na waota msaada wa huduma za dharura.
Sherehe za kuukaribisha mwaka mpya 2023 zilikuwa za kwanza kufanyika kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki baada ya kuitishwa kwa miaka mitatu kutokana na vizuizi vya kupambana na janga la corona na sababu za kiusalama.