1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwaka Mpya 2022 katikati ya wimbi jipya la corona

1 Januari 2022

Ulimwengu umeadhimisha Mwaka Mpya wa 2022 wakati mataifa mengi yakiwa na sherehe za kimyakimya kutokana na kupamba moto kwa janga la COVID-19, ingawa maeneo mengine yamepuuzia kabisa hadhari za kuzuwia maambukizo. 

Silvester I Neujahr 2022 in London
Picha: Rob Pinney/Getty Images

Miji ya London na Paris ilipiga marufuku mikusanyiko mingi mikubwa na uwashaji fashifashi, huku Madrid ikiagiza sherehe hizo kufanyika kwa kiwango cha wastani.

Mjini Berlin hakukuwa na fashifashi kwenye Lango la Brandenburg kama ilivyozoeleka, ambapo maelfu kwa malaki ya watu hukusanyika. Polisi katika mji mkuu huo wa Ujerumani waliwataka watu kutosogelea eneo hilo.

Mjini Rome, polisi walifunga baadhi ya maeneo ya katikati ya mji.

Lakini mjini Moscow, licha ya baridi kali mamilioni ya watu walijitokeza mitaani kuuaga mwaka 2021 na kuukaribisha 2022, wakirusha fashifashi na serikali ikiondowa marufuku kubwa za mikusanyiko. 

Maadhimisho ya mwaka mpya wa 2022 nchini China.Picha: Wang Jianwei/XinHua/dpa/picture alliance

Barani Asia, maadhimisho yalifanyika kwa tahadhari katika miji ya Beijing, Hong Kong, Jakarta na Bangkok. Rais Xi Jinping wa China alitumia hotuba yake ya Mwaka Mpya kuwataka wananchi kuweka mkakati makini na kuchukuwa tahadhari dhidi ya kitisho dhidi ya lengo la muda mrefu la Chama cha Kikomunisti cha kuigeuza China kuwa taifa kubwa duniani.

Mjini Dubai, jengo refu kabisa duniani la Burj Khalifa liliwasha mataa na mionzi huku fashifashi zikirushwa kuukaribisha mwaka 2022.

Afrika yaadhimisha kama kawaida

Nchini Afrika Kusini, taifa la kwanza kabisa kuripoti aina mpya ya kirusi cha corona ya Omicron, marufuku ya kutotoka nje nyakati za usiku iliondolewa ili kuruhusu shamrashamra za Mwaka Mpya.

Fursa kama hiyo hawakuipata watu wa Morocco, ambako marufuku dhidi ya mikusanyiko na sherehe iliendelea kama kawaida.

Makaribisho ya mwaka mpya wa 2022 nchini PakistanPicha: Akhtar Soomro/REUTERS

Nchini Marekani, jiji kubwa la New York lilirejea kwenye sherehe zake za kila mwaka katika Viwanja vya Times, licha ya maafisa wa afya kuonya dhidi ya mikusanyiko kama hiyo inayoweza kusambaza kwa haraka virusi vya corona.

Mamlaka za jiji hilo lenye watu wengi zaidi nchini humo zilisema kwamba zimedhibiti idadi ya watu wanaofurika kwenye sherehe kama hizo hadi kufikia 15,000 tu.

Katika mji wa Rio de Janeiro nchini Brazil, sherehe ambazo kawaida huwaleta pamoja zaidi ya watu milioni tatu katika fukwe za Copacabana ziliendelea kama kawaida.

Maadhimisho ya kwanza ya Mwaka Mpya yalianza kwa wakaazi wa visiwa vya Samoa na Kiribati kusini mwa Bahari ya Pasifiki, na baadaye New Zealand.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW