1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu waungana kuadhimisha siku ya wanawake duniani

8 Machi 2023

Ulimwengu hii leo unaadhimisha siku ya Wanawake ukaiangazia nyanja kuanzia mafanikio, changamoto na hata mustakabali wao, sio tu kwa wanawake bali pia wasichana.

Internationaler Frauentag 2023 | Themenbild | Philippinen, Manila
Picha: Jam Sta Rosa/AFP/Getty Images

Ulimwengu hii leo unaadhimisha siku ya Wanawakeukaiangazia nyanja kuanzia mafanikio, changamoto na hata mustakabali wao, sio tu kwa wanawake bali pia wasichana. Umoja wa Mataifa umekiri kwamba makundi haya yanakabiliwa na vikwazo vingi, na kutoa mwito kwa ulimwengu kuchukua hatua na kusimama pamoja na wanawake ili wapate haki zao za msingi na kuwalinda dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia. 

Kote ulimwenguni, kaskazini hadi kusini, wanawake wanaungana hii leo kuadhimisha siku hii, kwa kuwasilisha madai yao na kujadiliana kwa kina namna watakavyojikwamua kutoka kwenye vizingiti na vikwazo vinavyowazuia kushamiri. Maandamano yamehanikiza kwenye maeneo mbalimbali, wanawake wakitoa miito ya kupitiwa upya kwa sheria kandamizi na zinazowanyima uhuru, malipo sawa mahali pa kazi na kupambana na aina zote za unyanyasaji na ubaguzi unaotokana na jinsia.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa antonio Guterres amekiri alipokuwa akitoa salamu za maadhimisho haya kwamba ingawa ulimwengu unasherehekea mafanikio ya wanawake, lakini ni lazima kila mmoja kutambua kwamba bado kuna changamoto zinazowakabili ambazo zinamuhitaji kila mmoja kushiriki ili kuzizuia ama kuziondoa kabisa.

Wanawake na wanaume wakifanya maandamano mjini Seville huko Uhispania kuadhimisha siku ya wanawake dunianiPicha: Ángel García/Pacific Press/picture alliance

"Ubaguzi wa kijinsia unamuumiza kila mtu ...wanawake, wasichana, wanaume na wavulana. Siku ya Kimataifa ya Wanawake ni mwito wa kuchukuliwa hatua. Hatua ya kusimama pamoja na wanawake wanaodai haki zao za kimsingi kwa gharama kubwa na za kibinafsi. Hatua za kuimarisha ulinzi dhidi ya unyonyaji na unyanyasaji wa kijinsia. Na hatua ya kuchochea ushiriki kamili wa wanawake pamoja na uongozi. Hebu tushirikiane kuanzia serikalini, sekta binafsi na mashirika ya kiraia, kujenga ulimwengu jumuishi zaidi, wa haki, na ustawi kwa wanawake, wasichana, wanaume na wavulana kila mahali," alisema Guterres.

Maudhui ya mwaka huu yanasisitiza haja ya teknolojia na uvumbuzi ili kuendeleza usawa wa kijinsia.Maoni: Siku ya Wanawake haina mengi ya kuadhimisha Afrika

Huko Afghanistan, hali ni tete wakati serikali ya Taliban ikiendelea kulaumiwa vikali kwa vitendo vyake dhidi ya wanawake na kutajwa kama moja ya serikali kandamizi zaidi ulimwenguni. Tangu ilipoingia madarakani serikali ya Taliban imechukua hatua kadha wa kadha zinazolenga kuwabakisha wanawake nyumbani bila ya shughuli yoyote.

Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan Roza Otunbayeva amesema kwenye taarifa yake ya maadhimisho ya siku hii ya wanawake kwamba kumekuwepo na hatua za makusudi na za kupangwa za kuwaficha wanawake. Amesema hatua kali zinazochukuliwa na serikali zimefanikisha kuwaondoa na kuwazuia kabisa wanawake kufanya kazi na wengine wanalipwa sehemu ya mshahara wao wa zamani ili wabakie nyumbani.

Pengo la usawa katika malipo ni moja ya changamoto ambayo inawakabili wanawake wengi duniani Picha: NurPhoto/picture alliance

Wanawake wamezuiwa hata kwenda kwenye bustani za kupumzika ama kwenye maeneo yoyote ya umma ya burudani na kuagizwa kujifunika wanapokuwa hadharani. Lakini hatua kali zaidi ni ile ya kuwazuia wasichana kujiunga na shule za sekondari na taasisi ya elimu ya juu.

Hii leo, karibu wanawake 20 waliandamana katika mitaa ya Kabul, wakitoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa kuwalinda.

Mapema leo, waziri wa mambo ya familia wa Ujerumani, Lisa Paus ameiambia DW kwamba Ujerumani na Ulaya wanasimama bega kwa bega na wanawake wa taifa hilo na Syria. Paus alisema hayo baada ya kikao cha tume ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa huko New York Marekani ambako alizungumzia masuala ya usawa katika ulimwengu wa kidijitali.Wafungwa waadhimisha siku ya wanawake Kenya

Aliiambia DW kwamba ulimwengu unaadhimisha siku hii wakati kukiwa bado hakuna usawa wa kijinsia na sasa wanaitumia fursa hiyo kulimulika suala hilo kwa mtizamo wa kijinsia. Aidha aligusia suala la pengo lililopo kwenye malipo kati ya wanaume na wanawake na kusema hata hayo yanazingatiwa kwa upana wake katika ajenda za mkutano huo wa Umoja wa Mataifa.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW