1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulinzi mkali Cologne wakati AfD kikikutana

22 Aprili 2017

Chama cha sera kali za mrengo wa kulia AfD kimekuwa na mkutano wake uliotiwa dosari na mapambano ya kuwania madaraka huku maelfu ya wafuasi wa sera za mrengo wa kushoto wakiandamana kutaka kuuvuruga mkutano huo.

Deutschland Bundesparteitag der AfD in Köln
Picha: Reuters/W. Rattay

Wakati wajumbe wa mkutano huo walipokuwa wakianza kuwasili Jumamosi (22.04.2017) mahala pa mkutano kwenye hoteli ilioko mji wa Golgne magharibi mwa Ujerumani, waandamanaji waliokuwa wakiimba na kupiga mayowe walijaribu kuwazuwiya kupita vizuizi vya usalama na kusababisha mapambano na polisi ambapo poilsi wawili walijeruhiwa.Gari moja la polisi lilitiwa moto.

Waandamanaji 50,000 wanatarajiwa kukusanyika wakati wa mkutano huo wa siku mbili wa chama hicho kinachopinga wahamiaji cha Mbadala kwa Ujerumani huku polisi 4,000 wakimwagwa kuweka amani.

Wakati mkutano huo ukianza kiongozi mwenza wa chama cha AfD Frauke Petry ameshindwa katika jaribio la kutaka uungaji mkono wa wanachama zaidi kwa msimamo wa wastani chini ya msingi wa kutambuwa ukweli kama vile ulivyo wa "Uhalisia wa siasa." kwa nia ya kuzinyamazisha sauti za wale wenye misimamo mikali zaidi katika chama hicho.

Pigo kwa Petry

Maandamano dhidi ya chama cha Afd mjini Cologne.Picha: picture alliance/dpa/O.Berg

Gazeti mashuhuri la Bild limeuita uamuzi huo wa wajumbe wa hata kutoijadili hoja hiyo ya Petry mtaalamu wa zamani wa kemia mwenye umri wa miaka 41 ni pigo kwa mama huyo ambaye ni mja mzito akitegemea kupata mtoto wake wa tano.

Akitowa wito wa hamasa wakati akifunguwa mkutano huo,Petry amesema chama hicho cha AfD bado kinaweza kudhamiria kuwa chama kikuu nchini Ujerumani ifikapo uchaguzi mwengine katika kipindi cha miaka minne iwapo kitaregeza kauli zake kali katika ujumbe wake.

Amesema wajumbe inabidi waamuwe "iwapo na vipi chama hicho cha AfD kinaweza kuchagua uhalisia kushika madaraka kwa wapiga kura ifikapo mwaka 2021 ili kwamba hatuiachilii serikali moja kwa moja kwa vyama vikuu vilivyozoeleka.

AfD ambayo hivi sasa inawakilishwa katika majimbo 11 kati ya 16 ya Ujerumani kinakusudia kusaini mpango ambao utafunguwa njia kwa chama hicho kuingia katika bunge la taifa kwa mara ya kwanza katika hisoria yake ya miaka minne.

Umashuhuri washuka

Polisi wakibuburushana na waandamanaji Cologne.Picha: Reuters/T. Schmuelgen

Kikiwa kimeasisiwa mwaka 2013 kwa ilani ya kuwa na mashaka na Umoja wa UIaya chama hicho kimetumia kwa faida yake uamuzi wa Kansela Angela Merkel wa kuruhusu kuingia nchini kwa zaidi ya watafuta hifadhi milioni moja tokea mwaka 2015 na kubadili ramani ya kisiasa ya Ujerumani.

Lakini neema zake zimeanza kupunguwa kutokana na kupunguwa kwa wanachama wapya na vyama vyote vikuu vya Ujerumani vikifuta uwezekano wa kushirikiana nacho  iwapo kitavuka kiwango cha asilimia tano kupata uwakilishi wakati wa uchaguzi huo  wa tarehe 24 Septemba.

Uchunguzi wa maoni unaonyesha chama hicho cha AfD kikiwa na asilimia kati ya saba na kumi na moja kikiwa kimeshuka sana kutoka asilimia kumi na tano ilizokuwa imepata mwishoni  tu mwa mwaka jana.Merkel anawania muhula wa nne baada ya kuwa madarakani kwa takriban miaka 12 na chama chake cha kihafidhina hivi sasa kinaongoza katika uchunguzi wa kura za maoni.

Kufuatia malumbano ya wiki kadhaa ya ndani ya chama ,Petry ametowa tangazo la fadhaa kwamba hatowania kuongoza kampeni za Afd mwaka huu.Habari hizo zimekiacha chama hicho kikiyumba na kufunguwa medani ya mzozo kati ya wale wa sera kali za mrengo wa kulia na wale wenye siasa kali zaidi ndani ya chama hicho.

Mpinzani wake mkuu Alexander Gauland mwenye umri wa miaka 76 ambaye amekiasi chama cha CDU cha Merkel amewahimiza wajumbe kuishinda hoja ya mama huyo ya "siasa za uhalisia" kwa kusema kwamba inawagawa wanachama.

Mwandishi : Mohamed Dahman

Mhariri .Sylvia Mwehozi

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW