Ulinzi mkali waimarishwa katika maombi ya kitaifa ya Odinga
17 Oktoba 2025
Maelfu ya waombolezaji wamehudhuria maombi ya kitaifa ya kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga leo, huku ulinzi mkali ukiimarishwa baada ya hapo jana maafisa kufyatua risasi kutawanya umati wa watu waliojitokeza katika uwanja wa michezo wa Kasarani kuaga mwili wake.
Odinga, mwanasiasa mkongwe katika siasa za Kenya ambaye wakati mmoja alikuwa mfungwa wa kisiasa na kugombea urais mara tano bila mafanikio, alifariki dunia siku ya Jumatano akiwa na umri wa miaka 80 nchini India, ambako alikuwa akipatiwa matibabu. Odinga aliongoza kundi kubwa la wafuasi katika taifa hilo la Afrika Mashariki na umati mkubwa wa watu uliingia barabarani kuanzia mapema siku ya Alhamisi, na kuvamia uwanja mkuu wa ndegewakati ndege iliyokuwa imebeba mwili wake ilipowasili.
Vikosi vya usalama vilifyatua risasi hewani na polisi wakatumia gesi ya kutoa machozi kutawanya umati huo na hadi sasa polisi wanasema watu watatu wameuawa.