Ulinzi wa misitu wapata msukumo mpya Kenya
7 Aprili 2026
Taarifa rasmi ya Idara ya misitu nchini Kenya, KFS, imeuelezea mfumo huo huo mpya kuwa hatua muhimu katika harakati za usimamizi wa dijitali wa mbao na magogo mintarafu ukataji wa miti.
Mfumo huo mpya unajumuisha appu ya simu ya mkononi, maelezo ya matumizi kwenye vituo vya ukaguzi, mafunzo ya kitaifa kwa maafisa wa misitu na ushirikiano maalum na idara ya misitu ya Tanzania. Dhamira ni kuimarisha usimamizi, uangalizi na uwazi wa mchakato mzima wa kusafirisha mbao namagogo kutokea misituni hadi sokoni.
Mfumo huo mpya umeandaliwa Kwa ushirikiano na Idara ya kimataifa ya kupambana na mihadarati ya Marekani na shirika la kudhibiti biashara haramu ya wanyamapori la traffic International.
Dhamira ni kuimarisha uwazi katika sekta ya mbao sokoni
Mwakilishi wa Traffic International aliyekuwako wakati wa uzinduzi William Mauya anasisitiza kuwa lengo ni kuimarisha uwazi kwa kubana mapengo yaliyopo ya ufuatiliaji ili kuhakikisha kuwa kinachotoka misituni kinaweza kuthibitishwa. Dhamira ni kuimarisha uangalizi, utendaji na uwazi katika sekta ya mbao na magogo sokoni.
Kulingana na idara ya misitu ya Kenya, KFS, mfumo huo mpya utajumuisha pia matumizi ya appu ya simu ya mkononi, usambazaji wa maelezo ya majarida maalum kwenye vituo vya ukaguzi, mafunzo ya kitaifa kwa maafisa wa misitu na kuunganisha idara ya misitu ya nchi jirani ya Tanzania chini ya makubaliano ya pande mbili ya utekelezaji.
Pindi mpango utakapoanza kufanya kazi, mfumo utafuatilia wafanyabiashara wa mbao, spishi, viwango na idadi ya bidhaa zinazosafirishwa kutokea misituni hadi sokoni, kuimarisha mifumo ya sheria na uwajibikaji katika sekta hiyo. Waziri wa Mazingira nchini Kenya, Debra Mulongo anaafiki kuwa ajenda ya serikali ya kuiongeza idadi ya miti misituni bado inapewa uzito.
Itakumbukwa kuwa Kenya iliweka marufuku ya kukata miti mwaka 2018 baada ya jopo kazi kubaini kuwa biashara haramu ilikuwa inafanyika na ni kitisho kikubwa kwa uhifadhi wa misitu. Marufuku hiyo ilizuwia ukataji wa miti kwenye misitu ya umma na ile inayosimamiwa na jamii, hatua iliyoipa idara ya misitu ya KFS muda wa kuandaa mikakati madhubuti ya udhibiti. Kwa sasa Rais William Ruto alifulitilia mbali marufuku hiyo na kuruhusu ukataji wa miti iliyokomaa.