Ulinzi waimarishwa Cairo
23 Novemba 2012Ulinzi mkali umeimarishwa nje ya jengo la bunge, ofisi ya baraza la mawaziri na karibu na makao makuu ya wizara ya mambo ya ndani wakati ambapo waandamanaji wakianza kuungana katika uwanja wa Tahrir.
Rais Morsi jana amesaini marekebisho ya katiba ambayo yanayompa kinga ya maamuzi yake kutopitiwa na mahakama. Morsi ambaye amekuwa rais wa kwanza wa Misri kuchaguliwa kiraia pia amembadilisha mwendesha mashitaka mkuu ambaye naye aliteuliwa katika utawala wa sasa uliomwondoa madarakani Hosni Mubarak.
Mamlaka mapya kwa rais
Kanuni hiyo iliyotolewa jana inalipatia kinga bunge linaloongozwa kwa wingi na chama cha kiislamu na kumpatia mamlaka mapya rais ambayo ndiyo yaliompa nguvu za kumfukuza mwendesha mashitaka mkuu na kumteua mwengine.
Kanuni hiyo inaeleza kuwa maamuzi yoyote yatakayochukuliwa na rais Morsi mpaka wakati wa uchaguzi mpya wa bunge hayapaswi kuingiliwa kisheria.
Kanuni hiyo mbali ya kuonekana kama ya kimabavu lakini pia inaelekeza kurejewa kwa mashitaka ya maafisa wa utawala
Kauli ya upinzani
Upinzani wameita amri hiyo kama ukiukwaji wa uhuru wa mahakama na kudai kwamba inamkinga Morsi ambaye tayari anao ushawishi wa mamlaka ya wabunge na nguvu za kidikteta.
Hatua hiyo ni kama inaonekana muhimu katika kulinda mapinduzi ambapo chama cha rais Morsi cha udugu wa kiislamu na washirika wenzake wamesifu amri hiyo wakisema ni ''Mageuzi'' na kuitisha maandamano makubwa hii leo kwa ajili ya kumuunga mkono rais Morsi.
Hata hivyo upo ukosoaji katika utawala wa rais Morsi ambapo wale wasiokuwa waislamu wanalalamika sauti zao kutosikika.
Katiba ni kipengele muhimu katika kipindi cha nchini Misri katika kuimarisha demokrasia. Uchaguzi wa bunge jipya hautakuwepo hadi hati hiyo itakapokamilika na kupitishwa kwa kura ya maoni maarufu.
Kanuni hiyo inatoa muda miezi miwili zaidi kwa tume kumaliza kazi yake ikimaanisha kwamba kazi ya kutengeneza rasimu inaweza ikafikia mwezi februari na hivyo kusogeza nyuma uchaguzi mpya.
Mwandishi:Sylvia Mwehozi/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman