1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

UM wasema wafanyakazi wa MONUSCO wameshambuliwa Kinshasa

11 Februari 2024

Mkuu wa ujumbe wa kulinda wa amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, MONUSCO, Bintou Keita, amesema wafanyakazi wa ujumbe huo wameshambuliwa mjini Kinshasa.

Maandamano dhidi ya ujumbe wa MONUSCO
Ujumbe wa MONUSCO unakabiliwa na upinzani kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama mashariki mwa Kongo.Picha: Benjamin Kasembe/DW

Kwenye hujuma hizo pia magari ya MONUSCO yalilengwa. Hayo yamejiri katika wakati hali ya dhaifu ya usalama mashariki mwa Kongo imechochea hasira dhidi ya ujumbe huo wa amani.

Makundi ya watu waliokuwa kwenye pikipiki walikusanyika kwenye wilaya ya ukingoni mwa mto Kongo ya Gombe, eneo ambalo ujumbe wa MONUSCO na ofisi nyingi za ubalozi zinapatikana mjini Kinshasa.

Walichoma moto matairi la magari na kuwashambulia watu. Taarifa hizo ni kulingana na shirika la habari la Reuters.

Imeripotiwa kuwa magari kadhaa ya MONUSCO yamechomwa moto. Taarifa hizo zimethibitishwa na Keita kupitia ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii.

"Ninaalani vikali mkururo huo wa mashambulizi," amesema Keita.

Ubalozi wa Ivory Coast nao umesema moja ya magari yake limeharibiwa mjini Kinshasa na kuelezea jinsi kundi hilo la watu lilivyokuwa likifanya mashambulizi ya ovyo ovyo dhidi ya vyombo vya moto vya ofisi za ubalozi na mashirika ya kimataifa.

Kitisho cha M23 kuukamata mji wa Goma chaongeza hasira nchini Kongo 

Rais Felix Tschisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo alipokutana na mkuu wa ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo, Bintou Keita Picha: Giscard Kusema/Kommunikationsdienst DR Kongo

Polisi ya mjini Kinshasa na serikali ya Kongo hazijazungumza chochote kuhusiana na mkasa huo.

Kusonga mbele kwa kundi la M23 ambako kunatishia kuanguka kwa mji muhimu wa Goma mikononi mwa wapiganaji hao kumefanya hali ya mzozo wa miongo kadhaa unaondelea huko jimbo la Kivu Kaskazini kuzidi kuwa mbaya.

Maelfu ya watu wanapoteza makaazi wakikimbia vita na kitisho cha ukosefu wa usalama kimezidi kuwa kikubwa.

Mapambano kati ya waasi, vikosi vya ulinzi wa taifa na makundi binafsi yanayoliunga mkono jeshi la Kongo yameongezeka katika wiki za karibuni.

Hali ya ukosefu wa usalama yawalazimisha maelfu kukimbia makaazi yao 

Waasi wa M23Picha: Arlette Bashizi/REUTERS

Zaidi ya watu 135,000 wamelazimika kukimbilia maeneo yaliyoanishwa kuwa salama karibu na mji wa Goma.

Taarifa hizo zimetolewa na ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu msaada wa kiutu, OCHA.

Mapigano hayo "yanaweza kuvuruga hali ya upatikanaji chakula na shughuli za uchumi kwenye mji wa Goma na mkoa mzima," imesema taarifa ya OCHA.

Askari wa MONUSCO wamekuwepo mashariki mwa Kongo tangu mwaka 2010 pale walipochukua jukumu hilo kutoka ujumbe mwingine wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Majukumu yao yanajumuisha kusaidia juhudi za serikali ya Kongo kurejesha utulivu kwenye eneo hilo.

Lakini katika miaka ya karibuni uwepo wao umezongwa na maandamano ya vurugu kutoka makundi ya umma wenye hasira ambao unaulaumu ujumbe huo kutosaidia chochote kuifanya mashariki ya Kongo na amani.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW