1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umeme bado ni mashaka makubwa tu Tanzania

George Njogopa4 Machi 2021

Licha ya serikali Tanzania kudai kuwa imeimarisha ugavi wa umeme kwa kusambaza huduma hiyo katika maeneo mbalimbali ikiwamo vijijini, sehemu kubwa zimekumbwa na tatizo la ukosefu wa umeme katika wiki za karibuni.

Argentinien Stromausfälle
Picha: picture-alliance/Zuma/A. Aveledo

Ikiwa imebakiza kwa wastani asilimia 18 kufikisha huduma ya umeme katika maeneo yote ya nchi ikiwamo yale ya vijijini, lakini kile kinachoendelea kushuhudiwa sasa ni kama hadithi inayosubiri wasimuliwaji kutokana na namna adha ya ukosefu wa umeme inavyoendelea kuwaweka katika wakati mgumu wananchi wengi.

Ingawa tatizo hili la kukatika umeme mara kwa mara ni jambo lililozoeleka kwa muda mrefu kwa wananchi wengi, lakini ahadi za watendaji wa serikali za kudai kuwa tatizo hilo lingekuwa historia ziliwapa matumaini wananchi hao walioamini kuwa janga hilo la kukosa huduma ya umeme halingewaandama tena.

Hata hivyo, wakati huu karibu maeneo mengi ya nchi hiyo yanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa umeme wa uhakika, na hali hiyo inaelezwa kuvuruga shughuli za wananchi wengi.

Tanzania imekumbwa na ukatikaji wa umeme wa mara kwa mara katika wiki za karibuni.Picha: picture-alliance/Zuma/A. Aveledo

Kumekuwa na sababu mbalimbali zinazotolewa na mamlaka zinazohusika na sekta hiyo, ikiwemo zile zinazodai uchakavu wa miundombinu, matatizo ya dharura yanayoibuka bila kutarajiwa na nyingine ambazo wachambuzi wa mambo wanasema zimekosa mashiko.

Waziri azilaumu TANESCO, Songas

Waziri wa nishati, Merdard Kalemani ambaye amekuwa akizunguka huku na kule kutekeleza miradi ya umeme, ametoa muda wa siku tano kwa shirika la umeme nchini Tanesco pamoja na Kampuni ya Songas inayozalisha umeme kuhakikisha kwamba kero hiyo inamalizika mara moja.

Waziri huyo anazitupia lawama mamlaka hizo kwa kuchukua muda mrefu kuifainyia ukarabati baadhi ya miundombinu yake hali inayosababisha sehemu nyingi kuendelea kupata umeme wa mgao.

Wakati waziri huyo akisema hayo, kilio cha wananchi kuendelea kukosa huduma ya umeme ni kikubwa huku wengine wakilazimika kukutana katika mikutano ya hadhara na wabunge wao kupaza sauti.

Tatizo hili la ukosefu wa umeme limesambaa karibu katika maeneo mbalimbali ya nchi, mfano wakazi hao wa jijini Mwanza wameiambia DW jinsi wanavyoendesha maisha kwa taabu kutokana na ukosefu wa huduma hiyo.

Kwa ujumla nishati ya umeme siyo jambo la anasa tena, ni chaguo ambalo kila mmoja analazimika kulifuata hasa wakati huu ambao shughuli nyingi za mawasiliano ya kidigitali zinategemea umeme.

Huenda kilio hiki cha Watanzania wengi kikapata mwarobaini wa kudumu katika siku chache za usoni hasa kwa vile taifa hili liko katika uchumi wa kati,uchumi ambao muhimili wake mkubwa ni viwanda vinavyohitaji umeme kuendelea kunawiri.